Sunday 3 January 2016

MNAIGERIA ASHIKWA NAMZIGO WA MAANA UWANJA WANDEGE DAR ES SALAAM

Kamanda wa polisi wa Viwanja vya Ndege
Dar es Salaam. Jeshi la Polisi limemkamata raia wa Nigeria kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA), kwa tuhuma za kukutwa na dawa za kulevya ambazo thamani yake ni kubwa ingawa haijajulikana.


Kamanda wa polisi wa JNIA, Martin Ottieno alisema mtuhumiwa huyo, Ejiofor Ohagwu (33), alikamatwa na kilo nne za dawa hizo ambazo alisema licha ya kutofahamu thamani yake kwa sasa, inaweza kuwa kubwa kwa sababu hawajawahi kukamata dawa za kiwango hicho.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi, kilo moja ya heroin kwa bei ya mitaani ni kuanzia Sh90 milioni.

Ottieno alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa saa 8:00 usiku wa kuamkia jana kwenye sehemu ya ukaguzi ya eneo la wasafiri wanaoondoka.
Alisema awali polisi walipata taarifa za kiintelijensia kuhusu Ohagwu na alipopekuliwa alikutwa na dawa alizodai kuwa ni heroin zilizofungwa katika pakiti sita za plastiki.
“Mtuhumiwa huyo alikuwa anasafiri kuelekea mji wa Lagos, Nigeria, akitumia Shirika la Ndege la Ethiopia,” alisema.
“Dawa hizi alizificha kitaalamu kwa kushonea pakiti zote pembeni mwa mabegi yake mawili ya nguo ili asibainike haraka na vyombo vya dola.”
Alisema polisi bado inamshikilia mtuhumiwa huyo na upelelezi utakapokamilika, atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka.
Pia, alisisitiza kuwa kwa sasa viwanja vya ndege si vichochoro vya kupitisha dawa hizo, kwa kuwa polisi ikishirikiana na wadau wengine, imejipanga kupambana na aina hiyo ya uhalifu.
“Mbali na kuwakamata hawa, pia tumelenga kuwakamata mapapa wanaoagiza dawa hizi, ” alisema Kamanda Ottieno.
Desemba 17 mwaka jana, Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga alikutana na maofisa wa polisi wa Kanda ya Dar es Salaam na kutaka wamueleze mipango ya kukabiliana na dawa za kulevya.
Hili ni tukio la kwanza kutokea tangu mwaka uanze.

MWANANCHI

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!