Saturday, 2 January 2016

MATARAJIO YA MWAKA 2016: Serikali imepania kuongeza fursa za ajira


WAKATI tunaanza mwaka mpya wa 2016 yapo mengi ambayo Watanzania wanatarajia kuona yakitokea na hata kubadilisha maisha yao.


Miongoni mwa mambo hayo ni suala la ajira ambalo limekuwa tatizo sugu hususani kwa vijana. Hata hivyo Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu ina mpango wa kuboresha programu za kukuza fursa za ajira ili kwenda sanjari na kauli mbiu ya Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, Dk John Magufuli maarufu kama “Hapa Kazi Tu.” Kauli mbiu hiyo inaungwa mkono na idadi kubwa ya watu wakiwemo vijana ambao wanatamani kupata ajira ili kuweza kuitekeleza kwa vitendo.
Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Walemavu ni miongoni mwa Wizara zinazofanya shughuli zake ili kuendana na kasi ya Rais Magufuli ambapo hivi karibuni Waziri wa Ofisi hiyo, Jenista Mhagama ametoa tangazo kuhusu waajiri wote nchini kuhakikisha wanafuata sheria za kazi na ajira lakini pia kuhusu vibali vya ajira kwa wageni. Naibu Waziri wa Ofisi hiyo anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde anasema atahakikisha wanaboresha maslahi ya wafanyakazi wa sekta zote kwa kufuata na kuzingatia sheria zilizopo.
Katika kulitekeleza hilo, Mavunde ambaye alikuwa ameambatana na maofisa wa kutoka ofisi yake, Idara ya Uhamiaji, Wakala wa Afya na Usalama Mahali pa Kazi (OSHA) pamoja na maofisa wengine amefanya ukaguzi ili kuona utekelezaji wa tangazo lililotolewa na Waziri Desemba 14, mwaka jana. Mavunde ameanza ziara hizo za ukaguzi katika kampuni za simu na akubaini kuwepo kwa mambo ambayo ni kinyume na sheria. Kampuni hizo zime kuzipigwa faini pamoja na kuwataka kurekebisha mapungufu hayo katika muda mfupi.
Anasema lengo la ukaguzi huo ni kuhakikisha waajiri wote wanafuata sheria za kazi zilizopo lakini pia kuhakikisha wafanyakazi wanafanya kazi katika maeneo ambayo ni salama wakiwa na afya kama sheria inavyoelekeza. Anaeleza agizo la Waziri yake linawataka waajiri wote kuwapa wafanyakazi wao mikataba na kuwaruhusu kujiunga na vyama vya wafanyakazi na kuruhusu uwepo wa matawi ya wafanyakazi hao katika ofisi zao.
Akiwa katika ukaguzi kwenye kampuni hizo, Mavunde amebaini kuwepo kwa kasoro ambazo ameagiza kuzifanyia kazi pamoja na kuwapiga faini kama adhabu ya ukiukwaji wa sheria na kanuni mbalimbali zilizobainishwa katika kampuni hizo. Kuhusu ajira za wageni, Mavunde anasema wageni wanaokuja kufanya kazi nchini katika makampuni ya simu ni lazima kuwe na Mtanzania mmoja anayejifunza kutoka kwake ili mkataba wa mgeni huyo unapomalizika ujuzi huo uwe umerithishwa kwa Mtanzania.
Anasema hakuna sababu ya kuwa na waajiriwa wa kigeni kama wapo Watanzania wenye uwezo wa kufanya kazi hizo, kwani wageni hao wanapokuja ni sawa na kuja kupora ajira ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania. Katika hilo, Mavunde alipokuwa katika ofisi za kampuni ya simu ya Halotel aliweza kumkuta fundi wa kufungu meza na viti vya kukalia vya ofisi vikifungwa na raia wa Vietnam ambaye kibali chake kilikuwa kina siku moja kabla kuisha.
“Naagiza huyu mtu asipewe kibali kingine, hiki kikiisha aondoke, haiwezekani mtu atoke kwao aje hapa kufunga viti, wakati tuna vijana wa Kitanzania wengi wenye ujuzi wa aina hii, jambo la iana hii haikubaliki,” anasema Mavunde. Mavunde anasema wapo wageni wanaombewa vibali na waajiri wao kuja kufanya kazi nchini wakati huo huo wapo wataalamu wa hapa nchini wana uwezo wa kufanya kazi hizo, kitendo hicho ni kinyume cha taratibu kwani kinawakosesha wataalamu wa hapa nchini fursa.
Anasema hatua ya kuwaleta wataalamu kutoka nje ni iwapo hapa nchini wamekosekana watu wenye uwezo wa kufanya kazi hiyo na wataalamu hao wageni watafanya kazi hiyo huku wakiwafundisha Watanzania ili waweze kurithi baada ya wao kuondoka nchini. Idadi kubwa ya vijana wako majumbani, vijiweni na maeneo mengine wakiwa hawana kazi lakini kumbe kazi ambazo walipaswa wafanye vijana hao zimechukuliwa na wageni kutoka katika nchi mbalimbali.
Mavunde pia anasikitishwa na kitendo cha baadhi ya kampuni kuwalipa mishahara kidogo wafanyakazi wake kiasi cha kutoendana na kima cha chini cha sekta hiyo ya mawasiliano ambapo ametaka jambo hilo lirekebishwe haraka iwezekanavyo, kwani katika sekta ya mawasiliano kima cha chini cha mshahara ni Sh 400,000. “Wafanyakazi ambao hawana mikataba ni vizuri wakapewa mikataba yao ya ajira na wale ambao wanayo wapewe nakala za mikataba wakae nazo wenyewe...kuwe na usawa kwa wafanyakazi wenye elimu na wanaofanya kazi zinazofanana,” Mavunde anasisitiza.
Amewataka waajiri wote nchini kuhakikisha wafanyakazi wao wanafanya kazi katika mazingira ya afya na usalama ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa usahihi, kwani katika baadhi ya maeneo aliyoyatembelea imeonekana kuwa kuna tatizo kubwa katika masuala ya afya na usalama mahali pa kazi. Jambo lingine ambalo Mavunde ameonekana kusisitiza ni waajiri kuhakikisha wanapeleka michango ya wafanyakazi katika mifumko ya hifadhi ya jamii kwa wakati ili kufuata sheria kwani jambo hilo limekuwa ni tatizo sugu, kwani wapo baadhi ya wafanyakazi ambao wakiacha kazi michango yao inakuwa haijalipwa kwa muda mrefu.
Mavunde anasema Serikali inataka kuona waajiri na waajiri wote wanapata kile wanachostahili bila mmoja wao kumuumiza mwingine, kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia kuondoa misuguano ya mara kwa mara baina ya waajiri na waajiriwa. Anasisitiza kuwa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais John Magufuli ya kuwaletea wananchi wake maendeleo si ya kubabaisha bali ni ya dhati ili Watanzania wote waweze kunufaika.
Anasema wapo baadhi ya watu wamekuwa wakibeza kasi hiyo ya Serikali kuwa ni ‘moto wa mabua’, anawaambia kuwa kasi waliyoanza nayo ni ndiyo hiyo hiyo hadi pale watakapohakikisha kuwa malengo ya kuwaletea wananchi maendeleo imekamilika. Hivyo Mavunde anasema matarajio yake ni kuona Sheria ya Kazi inafuatwa na waajiri wote ili kujenga Tanzania ambayo itakuwa haina misuguano baina ya wafanyakazi na waajiri jambo ambalo litasaidia kuleta maendeleo kwa kasi iliyopo.
“Ukaguzi huu si kwa ajili yangu mimi, hapana hii ni kwa faida ya watu wote...hatuwezi tukapiga hatua kama kutakuwa na ubabaishaji, tufanye kazi kwa kufuata sheria,” Mavunde anasisitiza. Kama sheria ikifuatwa inavyotakiwa baadhi ya vijana wanaweza kupata ajira katika sekta mbalimbali kulingana na taaluma zao, hivyo ukaguzi huo utafanyika nchi nzima ili kuhakikisha sheria inafuatwa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!