Friday, 1 January 2016

FUNGUO NNE ZA KULINDA AFYA YAKO

Wataalamu wa afya wanasema utoaji damu ni njia

Ili mtu awe na afya nzuri, anahitaji chakula chenye lishe bora. Mtu anahitaji kula vyakula vya kujenga mwili, kuupa mwili nguvu na kulinda mwili.


Hivyo unapokula tumia matunda, mboga na uwe na kawaida ya kula vyakula vya aina mbalimbali.
Vyakula vya nafaka ambayo haijakobolewa kama vile mkate, nafaka yenyewe mfano dona, tambi au mchele, vina virutubisho na nyuzinyuzi kuliko vyakula vinavyotokana na nafaka zilizokobolewa.
Mafuta yanayopaswa kutumika kupikia vyakula vyako yanafaa yawe ya asili ya mimea kama alizeti na sio ya yenye asili ya wanyama kwa kuwa yana kiwango kikubwa cha lehemu inayohatarisha afya ya mtumiaji.

Pia, chumvi inabidi utumiwe kwa kiasi pamoja na kuendelea kuepuka tabia ya kutumia chumvi ya mezani wakati wa kula kwa maana ni hatari kwa moyo wa mtumiaji.
Ni muhimu nyama ya jamii ya kuku na nyama nyingine zipikwe na kuiva barabara. Viini vya magonjwa huongezeka sana katika chakula chenye uvuguvugu. Kwa hiyo, chakula kiliwe mara moja baada ya kupikwa. Ikiwa itabidi kuhifadhi chakula zaidi ya saa mbili, hakikisha kinahifadhiwa katika hali ya joto au kuwekwa mahali penye baridi kama jokofu.
Pengine swali kuu ni kwa vipi tunaweza kuepuka vyakula visivyofaa? Unashauriwa kusafisha vizuri mboga kabla ya kupika, kwa kuwa mboga hukuzwa katika udongo ambao huenda umewekewa mbolea ya viwandani.
Safisha kwa maji moto yenye sabuni, mikono yako, ubao unaotumia kukatia mboga, vyombo na meza za jikoni kabla ya kuanza kuandaa chakula. Epuka kukiweka chakula safi kwenye sahani au chombo chochote kisichosafishwa kilichokuwa kimetumiwa kuweka mayai mabichi, kuku, nyama au samaki.
Fanya mazoezi
Unahitaji kufanya mazoezi bila kujali umri wako ili kuwa na afya njema. Ni vizuri kuwasiliana na daktari au mtaalamu wa mazoezi, kabla ya kuanza kufanya mazoezi yoyote mapya, kwa maana mazoezi yanayofaa yanategemeana na umri na afya ya mtu.
Kufanya mazoezi kunaweza kukusaidia kulala vizuri, kuwa na furaha zaidi, kuwa na akili makini, kuweza kutembea kwa wepesi, kuwa na mifupa na misuli yenye nguvu, kudumisha au kuwa na uzito wa mwili unaofaa kiafya iwapo. Pia utakula chakula chenye lishe, kupunguza hatari ya kuwa na ugonjwa wa kushuka moyo, kupunguza hatari ya kufa mapema. Ikiwa haufanyi mazoezi huenda ukapatwa na magonjwa ya moyo, kisukari aina ya 2, shinikizo la damu, mwili kuwa na kiwango cha juu cha lehemu na kiharusi.
Watoto chini ya miaka mitano hawapaswi kuzubaa kwa muda mrefu labda wawe wamesinzia. Kutazama luninga na kusafiri mara kwa mara na kwa muda mrefu kutumia basi au treni kunadhoofisha afya ya mtoto na ukuuaji wake.
Mazoezi mepesi kwa watoto ni pamoja na kusimama na kutembea polepole, wakati mazoezi magumu kwa watoto ni kama kutembea haraka, kuogelea, kuruka kamba na kuendesha baiskeli.
Watoto wa miaka mitano hadi 18, wanapaswa kutumia angalau dakika 60 za mazoezi kila siku, ikijumuisha mazoezi rahisi kama kuendesha baiskeli taratibu, wakati mazoezi magumu ni kukimbia haraka na kucheza tenisi.
Watu wazima wa miaka 19 hadi 64 wanahitaji angalau dakika 150 za mazoezi rahisi kama kuendesha baiskeli taratibu na kutembea haraka kwa kila wiki na siku mbili au zaidi kwa wiki, wafanye mazoezi ya misuli kama kubeba uzito mkubwa na pushapu. Njia nyepesi ya kufaulu kutimiza muda uliopendekezwa wa mazoezi ni kufanya mazoezi kwa dakika 30 kila siku kwa siku tano za wiki.
Pumzika kiasi cha kutosha
Mabadiliko ya maisha yameongeza hekaheka za maisha kiasi cha kufanya watu wasiwe na wakati wa kutosha wa kulala.
Kulala na kusinzia ni muhimu kwa ajili ya makuzi na maendeleo ya watoto na vijana, kujifunza na kukumbuka habari mpya, kudumisha usawaziko unaofaa wa homoni zinazosaidia kumeng’enya chakula na uzito wa mwili, kudumisha moyo wenye afya nzuri na kuzuia magonjwa.
Usingizi huimarisha mfumo wa kinga na kupunguza hatari ya kupatwa na maambukizo, kisukari, ugonjwa wa moyo, kansa, kunenepa kushuka moyo na pengine hata ugonjwa wa kukosa kumbukumbu
Kiasi kinachohitajika cha usingizi kinatofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine. Watoto wengi wachanga hulala saa 16 hadi 18 kwa siku, watoto kuanzia umri wa mwaka mmoja hadi mitatu hulala saa 14 na wale wenye umri wa miaka mitatu hadi minne hulala saa 11 au 12 hivi. Watoto walio na umri wa kutosha kwenda shule kwa ujumla wanahitaji kulala kwa saa 10, vijana kwa saa tisa au 10 na watu wazima kwa saa saba hadi nane.
Pima na linda afya yako
Baadhi ya magonjwa huhitaji uchunguzi wa daktari. Kwa kawaida, ugonjwa ukigunduliwa mapema, unaweza kutibiwa kwa urahisi na mtu atatumia gharama kidogo kutafuta tiba. Kwa hiyo, unapojihisi vibaya, badala ya kujaribu kutibu dalili tu, muone daktari ili achunguze kisababishi ni nini.
Epuka kujijeruhi wakati unafanya shughuli. Unashauriwa kufuata sheria za usalama unapofanya kazi, unapoendesha baiskeli, pikipiki au gari. Hakikisha chombo chako cha usafiri ni salama.
Vaa nguo za kujikinga na vifaa vinavyofaa vya kujikinga kama vile miwani, kofia, viatu na pia mikanda ya usalama na vifaa vya kulinda masikio.
Acha kuvuta sigara na kutumia bidhaa za tumbaku. Kuacha sasa kutapunguza hatari ya kupatwa na ugonjwa wa moyo, kansa, mapafu na kiharusi.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!