Wednesday 6 January 2016

DODOMA WAMUAGA POLISI ALIYEKUFA MAJI NA FAMILIA YAKE

Waombolezaji wakiaga miili ya marehemu

Dar/Dodoma. Mji wa Dodoma jana ulizizima wakati polisi walipokuwa wakiaga miili sita ya marehemu ikiwamo ya wenzao wawili waliokufa maji juzi.


Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Galawa aliongoza mamia ya wakazi na maofisa wa Polisi kuaga miili ya Mkaguzi wa Polisi, Gerald Ryoba aliyekuwa msaidizi wa mkuu wa jeshi hilo, Ernest Mangu, familia yake, dereva wake na binti wa kazi.
Mkaguzi huyo alifariki dunia na familia yake yote Jumapili iliyopita, baada ya gari walilokuwa wakisafiria kusombwa na maji ya mafuriko katika eneo la Bwawani, Kibaigwa mkoani Dodoma.
Mbali na Ryoba, familia yake akiwamo mkewe na watoto wawili waliokuwa wakitoka Geita kwenda Dar es Salaam walipoteza maisha baada ya kusombwa na maji yaliyokuwa na kasi kubwa kwenye barabara kuu ya Dodoma -Morogoro.
Galawa alisema Jeshi la Polisi na Taifa kwa ujumla limepata pigo kubwa kumpoteza mtu muhimu kwa wakati huu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime alisema enzi za uhai wake, marehemu Ryoba alikuwa kiunganishi kikubwa kwa askari wa hali ya chini na uongozi.
Akihubiri katika ibada ya kuwaombea marehemu hao, Mchungaji Yohana Chisoma wa Kanisa la Anglikana, aliwataka watu wote kuamini kuwa vifo hivyo ni mpango wa Mungu.
Miili ya Inspekta Ryoba na familia yake inatarajiwa kuzikwa leo katika Mtaa wa Kasamwa, Geita na Mkuu wa Jeshi hilo, IGP Ernest Mangu atahudhuria.
IGP Mangu akiwa safarini kwenda Geita, alisema ipo haja kwa mamlaka ya miundombinu kuweka tahadhari mahali ilipotokea ajali ya familia hiyo ili kupunguza maafa mengine zaidi siku za usoni.

MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!