Moshi. Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoani wa Kilimanjaro, imemhukumu kifungo cha miaka sita jela au kulipa faini ya Sh10.5 milioni raia wa India, Anurag Jain (45) baada ya kupatikana na hatia ya kutaka kusafirisha nje madini ya Tanzanite yenye thamani ya Sh670 milioni kinyume cha sheria.
Hukumu hiyo ilitolewa jana mjini hapa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo, Joachim Tiganga baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.
Mahakama hiyo ilimtia hatiani mshtakiwa huyo katika mashtaka mawili, la kwanza likiwa ni kukutwa na madini hayo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) na lile la pili la kusafirisha madini hayo bila kuwa na kibali na kutokuwa na kampuni inayoruhusiwa kisheria kuyasafirisha.
Katika shtaka la kwanza mahakama ilimhukumu kifungo cha miaka mitatu jela au kulipa faini ya Sh5 milioni na lile la pili kifungo cha miaka mitatu au kulipa faini ya Sh5.5 milioni. Mshtakiwa alilipa faini ya jumla ya Sh10.5 milioni na kuachiwa huru.
Awali Wakili Mwandamizi wa Serikali, Abdallah Chavula alidai mahakama hapo kuwa, mshtakiwa alikutwa na gramu 2,015 za madini hayo yenye thamani ya Dola310,137 za Marekani (sawa na Sh670 milioni).
Alidai kuwa Desemba 15, mwaka huu katika uwanja wa Kia mshtakiwa alipatikana na madini hayo bila kuwa na leseni ya madini, uwakala au kuwa mfanyakazi wa kampuni ya madini. Pia mwendesha mashtaka huyo alidai mshtakiwa huyo alitaka kusafirisha madini hayo kwenda nje ya nchi kupitia uwanja huo bila kuwa na kibali wala leseni.
No comments:
Post a Comment