Tuesday, 24 November 2015

TAMISEMI YAPIGA MARUFUKU MICHANGO YOTE MASHULENI.


Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), imeziagiza halmashauri nchini kuanzisha programu maalumu ya chakula kwa shule zote za msingi zilizokuwa zikichangiwa na wazazi.




Akizungumza jana mjini hapa, Naibu Katibu Mkuu wa Tamisemi (Elimu), Zuberi Samataba alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli la kufuta michango na ada kwa shule za awali, msingi na sekondari nchini.
“Tumeshawaambia waanze na hili kwa kutumia sehemu ya makusanyo yao kupeleka shuleni kwa ajili ya chakula cha wanafunzi waliokuwa wakikipata kutokana na michango ya wazazi,” alisema.

Samataba alisema ili kuongeza makusanyo, halmashauri zinatakiwa kutumia mfumo wa kieletroniki wa kukusanya mapato.
Alisema Tamisemi imetoa taarifa kwa watendaji wote kuacha kutoza michango na ada na atakayebainika kwenda kinyume atafukuzwa kazi. “Wito wangu wazingatie agizo la Rais Magufuli watuachie sisi hayo masuala mengine,” alisema.

Alipoulizwa mpango wa Serikali kufidia fedha zilizokuwa zikitokana na michango mbalimbali kama ya madawati, Samataba alisema mingi ilikuwa ikishia mikononi mwa watu wachache.
“Hebu angalia dawati moja linalochangwa na mwanafunzi wa sekondari linaweza kutumika kwa miaka zaidi ya 10 kama ni imara, lakini kila mwanafunzi akijiunga na shule anaambiwa achangie dawati, hayo madawati gani ambayo hayajai darasa kila mwaka,” alihoji.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!