Wednesday, 25 November 2015

MAGUFULI AFUTA GWARIDE ATAKA USAFI SHEREHE ZA UHURU



Rais Dk. John Magufuli, ameagiza maadhimisho ya siku ya Uhuru ambayo yangefanyika Disemba 9 mwaka huu, kutofanyika badala yake siku hiyo itumike kufanya usafi nchi nzima ili kutokomeza janga la kipindupindu lililoshika kasi.



 
Aidha, Rais Magufuli amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi wote nchini, kuandaa vifaa vya kufanyia usafi kabla ya siku hiyo na kwamba ifikapo Januari mwakani mkoa utakaobainika kuwa mchafu, viongozi wake  watawajibishwa.
 
Agizo hilo la Rais Magufuli, lilitolewa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, wakati akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya kuhitimisha ziara yake katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
 
Balozi Sefue, alikwenda Muhimbili kukagua vitanda 300 na magodoro ambavyo Rais Magufuli aliagiza Sh. milioni 225 zilizokuwa zimechangwa na wadhamini kwa ajili ya sherehe ya kuzinduliwa kwa Bunge la 11 Novemba 20, mwaka huu, zinunulillie vifaa hivyo kwa ajili ya kuondokana na changamoto ya wagonjwa kulala chini katika hospitali hiyo.
 
“Rais Magufuli ameonyesha kusikitishwa na kukerwa na tatizo la kipindupindu ambacho kinasababishwa na uchafu, kilichoenea nchini nzima ikizingatiwa kuwa ni miaka 50 ya uhuru sasa, lakini bado nchi hasa Jiji hili limekuwa na uchafu,” alisema Balozi Sefue na kuongeza: 
 
“Kwa maana hiyo, ameagiza siku hiyo hakutakuwa na gwaride wala shamrashamra za aina yoyote, badala yake viongozi wote wa mkoa na viongozi wa halmashauri wajiandae kwa ajili ya kufanya usafi wa maeneo nchi nzima, wahakikishe wananunua vifaa vya kufanyia usafi kwa ajili ya siku hiyo na kila Mtanzania atashiriki kazi hiyo.”
 
Kwa mujibu wa Balozi Sefue, Rais Magufuli pia alisema fedha ambazo zingetumika kufanya shughuli hiyo, Rais Magufuli atazitafutia shughuli nyingine za jamii na atatoa tarifa kwa vyombo vya habari.
 
Balozi Sefue alisema lengo la Rais Magufuli ni kuhakikisha nchi inarejea katika hali ya usafi na kwamba viongozi wataoshindwa kudhibiti uchafu katika mikoa yao hatua kali zitachukuliwa dhini yao.
 
“Rais Magufuli, ameshaagiza na kinachofuata ni utekelezaji na tatizo la uchafu linatokana na watendaji kutotimiza wajibu wao kusimamia mazingira na baada ya Disemba, mkoa ambao utabainika kuwa mchafu, watendaji wake watachukuliwa hatua ikiwamo kijieleza,” alisema.
 
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Donan Mmbando, alisema kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2009 ya Afya ya Jamii, adhabu ya mtu atakayebainika kutupa takataka ovyo atatozwa kiasi cha Sh. milioni moja, kwenda jela miezi mitatu au vyote kwa pamoja.
 
“Kama ambavyo madiwani, walipitisha sheria hii, tutahakikisha inatekelezwa na baada ya jiji kuwa safi yeyote atakayebainika kufanya hivyo atatumikia adhabu hiyo,” alisema Dk. Mmbando.
 
Ugonjwa wa kipindupindu umesababisha vifo vya watu takribani 106 nchini, baada ya kulipuka hivi karibuni.  
 
Katika hatua nyingine, Balozi Sefue, alisema Rais Magufuli ameagiza watumishi wote wa umma kuvaa begi zenye majina yao ili watambulike kwa wananchi wanaowahudumia.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!