Wednesday, 25 November 2015

JARIDA LA WANAWAKE-NI WAKATI GANI UNAWEZA KUPATA UJAUZITO?



hedhi na kupata mimba



Katika mfulululizo wa mada yetu ya leo, tulianza kwa kuona mzunguko wa hedhi ni nini na matatizo yanayojitokeza wakati wa mzunguko wa hedhi. Tukazungumzia awamu ya kwanza ya mzunguko wa hedhi – Kutoa Damu – inayoanza siku ya kwanza mwanamke anapoanza kutokwa na damu. Tutaendelea kwa kuzungumzia awamu nyingine tatu za mzunguko huo na mwisho kubainisha siku ambazo mwanamke anaweza kubeba mimba katika mzunguko huo. Karibu tuanze na awamu ya pili:


The Follicular Phase


Hii ndiyo awamu inayofuatia mara baada ya awamu ya kwanza ya Kutoa Damu (The bleeding Phase). Awamu hii imepewa jina hilo kwa sababu tezi ya pituitary (Pituitary Gland) inatoa homoni iitwayo Follicle Stimulating Hormone (FSH) ambayo inatoa ishara ambayo itavifanya vifuko vinavyotunza mayai (follicles) kukomaa. Shughuli katika awamu hii ya mzunguko wa hedhi huanzia kwenye tezi ya hypothalamus inayopatikana katika ubongo. Tezi hii inashughulika na usimamiaji wa kiu, njaa, usingizi, hamu ya mapenzi n.k. Hypothalamus hutoa kemikali iitwayo Follicle Stimulating
Hormone Releasing Factor (FSH-RF) ambayo itaiamuru tezi ya pituitary kutoa homoni iitwayo Follicle Stimulating Hormone (FSH) na kiasi kidogo cha homoni ya Leutenizing Hormone (LH). Utolewaji wa homoni hizi katika damu husababisha vifuko vya mayai (follicles) kukomaa.
Vifuko vya mayai vikianza kukomaa vitatoa homoni nyingine iitwayo estrogen. Kadiri vifuko hivi vinavyozidi kukomaa katika siku saba, homoni ya estrogen hutolewa zaidi na zaidi. Pamomja na estrogen, testosterone homoni ya aina nyingine huongezeka katika damu. Kuongezeka kwa homoni hizi mbili huufanya mwili kupata nguvu na ufanyaji kazi wa ubongo huboreshwa. Mwanamke atasikia hali ya kujiamini na mwenye kupenda kuthubutu. Kuongezeka kwa testosterone kutamfanya ajisikie kupenda kufanya mapenzi wakati oestrogen itamfanya apende kuwa mtu wa kutoka na kuonekana
wakati huo hamu ya kula ikipungua. Ni kipindi cha kusikia ukamilifu na bora kwa kufanya maamuzi na kuthubutu mipango mikubwa na migumu.
Homoni ya estrogen huifanya ngozi nyororo inayotanda juu ya nyumba ya uzazi (uterus) kuwa nene na kuleta mabadiliko kwenye ute wa mwanamke (cervical mucous). Kiwango cha estrogen kikifikia kiasi fulani, hypothalamus hutoa Leutenizing Hormone Releasing Factor (LH-RF) ambayo itaifanya tezi ya pitutary kutoa kiasi kikubwa cha Leutenizing Hormone (LH). Tendo hili hukifanya kifuko cha yai kilichokomaa kupita vyote kupasuka na kuachia yai.

The Ovulatory Phase


Kutolewa kwa yai (ovulation) ni kilele cha shughuli zote zilizokuwa zikiendelea katika mwili wa mwanamke katika wiki chache sasa toka alipoanza kutoka damu. Yai lililotolewa na kifuko katika ovari lina uhai wa wastani wa saa 12 hadi 24 kabla ya kunywea.
Yai linapokaribia kuachiwa, kiwango cha damu kinachopelekwa kwenye ovari huongezeka na misuli inayoshikilia ovari hujikunja ili kusogeza ovari karibu na mrija wa uzazi (fallopian tube), kulifanya yai litakaloachiwa kuingia kirahisi ndani ya mrija wa uzazi. Muda mfupi kabla ya yai hili kuachiwa, mlango wa uke (cervix) hutoa ute kwa wingi. Ute huu unaonata huasidia mbegu za kiume kusafiri kuelekea kwenye yai. Baadhi ya wanawake hutumia ute huu
kama ishara ya siku ambazo wanaweza kupata ujauzito.
Yai likiwa ndani ya mirija ya uzazi husafirishwa kwa kutumia namna ya vijinywele viitwavyo “cilia” kuelekea kwenye nyumba ya uzazi (uterus). Yai hili litarutubishwa endapo kutakuwa na mbegu za kiume.
Tofauti na mwanamme ambaye hutengeneza mbegu za kiume kila siku na kwa karibu muda wote wa maisha yake, mwanamke
anazaliwa na mayai yake ndani ya vikapu vyake miwili – ovari. mwanamke huzaliwa na mayai yake haya machanga yapatayo milioni moja hadi mbili ndani ya ovari. Katika maisha yake mayai mengi hufa, kuanzia anapokuwa mchanga, na hubakia na mayai yapatayo 400,000 anapofikia kuvunja ungo. Kila anapoingia mwezini, mayai yapatayo 1,000 hupotea na ni moja tu linalofikia kukomaa (ovum) na kuachiwa liingie ndani ya mrija wa uzazi. Katika mayai yake yote milioni moja au ambili aliyozaliwa nayo, ni mayai kama 450 tu yatakayofikia kukomaa.
Ni kiasi kidogo sana cha follicles kitakuwa kimebakia mwanamke huyu anapofikia kukoma hedhi hali ambayo kwa wanawake wengi hutokea kwenye miaka kati ya 48 na 55.  Hata hivyo follicles hizi si rahisi kukomaa tena na kutoa mayai kutokana na mabadiliko ya homoni yanayoendana na kukoma kwa hedhi.

The Luteal Phase


Siku 2 hadi 3 baada ya yai kutolewa, viwango vya estrogen na testosterone vitaanza kushuka katika damu na homoni ya progesterone kuanza kutengenezwa. Progesterone ni homoni inayopunguza wasiwasi katika mwili hivyo kuufanya mwili kuwa tulivu. Katika siku zinazofuata, wanawake wengi hujisikia vibaya kutokana na Premenstrual Syndrome (PMS), tatizo ambalo limejulikana kwa miaka mingi.
Premenstrual Syndrome ni jumla ya matatizo yanayowapata wanawake na kuwafanya wajisikie vibaya kutokana na viwango
vya homoni kuwa juu kabla, na wakati mwingine, wakati wakiwa katika hedhi.
Aina moja ya PMS hujionyesha kwa mwanamke kuwa na wasiwasi, kuna na hasira na asiyetabika. mara nyingi hali hupotea mara baada ya kuingia kwenye siku zake. Hii inaweza kutokana na uwiano wa estrogen na progesterone. Estrogen ikizidi, wasiwasi hutanda na progesterone ikizidi, hali ya kuwa na mfadhaiko hujionyesha.
Aina nyingine ya PMS ni kupenda sana sukari (chocolate, mikate , wali mweupe n.k.), uchovu wa mwili na maumivu ya kichwa. Hii inaweza kuwa inatokana na mwili kuongeza usikivu wa insulin unaotokana na kuongezeka kwa viwango vya homoni kabla ya hedhi.
Wakati huu kuna mabadiliko yayotokea kwneye uterus na ovari. Kile kifuko kilichotoa yai hubadilika rangi na kuwa cha njano “corpus luteum.” Kifuko hiki kinavyoendelea kupona kinatoa homoni ya estrogen na kiwango kikubwa cha progesterone, homoni muhimi katika utunzaji wa mimba. Hapo baadaye endapo mimba haikutungwa, kifuko hiki hubadilika rangi na kuwa cheupe ” corpus albicans”.
Homoni ya progesterone huifanya ngozi laini inayotanda juu ya uterus (endometrium) kufunikwa na ute, unaozalishwa na tezi zilizopo katika ngozi hiyo. Kama yai halikurutubishwa na mimba kutungwa, arteri za kwenye ngozi nyororo ya juu ya uterus hujifunga na damu kusitishwa kuelekea kwenye ngozi hiyo. Vijibwawa ya damu katika veni hupasuka, pamoja na utando wa endometrium, hutoka nje ya mwili na kuwa ndiyo mwanzo wa hedhi. Urefu wa hedhi hutofautiana baina ya wanawake na hubadilika katika maisha yao.

Siku Za Kupata Mimba Katika Mzunguko Wa Hedhi


Baadaa ya kuuelewa vizuri mzunguko wa hedhi wa mwanamke, sasa tunaweza kuzungumzia siku za kupata mimba mwanamke. Kimsingi kuna siku 6 ambazo mwanamke anaweza kubeba mimba – siku 5 kabla ya kutoa yai na saa 24 baadaya yai kutolewa. Hii ni kwa sababu mbegu za mwanamme zina uwezo wa kukaa kwa siku 5 ndani ya mwili wa mwanamke kabla hazijafa na yai (ovum) la mwanamke lina uwezo wa kuishi kwa saa 12 hadi 24.

mzunguko wa hedhi


Kitu cha msingi ni kujua siku ambayo mwanamke anatoa yai, kazi ambayo kidogo inataka ujanja kwa sababu mwanamke hatoi yai siku ile ile katika mzunguko wake. Vitu vinavyoweza kutumika ni kufuatilia utokwaji wa ute unaonata na joto la mwili wa mwanamke mapema asubuhi kabla hajaamka na kula kitu cho chote.
Kwa mwanamke wa kawaida mwenye mzunguko unaojirudia wa siku 26-32, unaweza kuchukulia kuwa siku za kupata mimba ni
siku zote kuanzia siku ya 8 toka alipoanza hedhi hadi siku ya 19. Katika kipindi hiki, mwanamke akifanya mapenzi mara kwa mara, yamkini ni kubwa kuwa atapata ujauzito.


No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!