Thursday 8 October 2015

KIWANDA CHA WACHINA WAKAUSHA NYETI ZA NG'OMBE CHAFUNGWA


SERIKALI imekifungia na kukitoza faini ya Sh milioni kumi kiwanda bubu cha Wachina, kilichopo Tabata Bima, Dar es Salaam kwa kukiuka taratibu za nchi. Kiwanda hicho kilikuwa kikijihusisha kukausha nyeti za ng’ombe na kusafirisha bila kuwa na vibali.


Kibali chao cha kufanya kazi nchini, kilikuwa cha kuuza vyombo katika eneo la Kariakoo, katikati ya jiji la Dar es Salaam. Kiwanda hicho kilifungwa jana na timu ya maofisa kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.
Maofisa hao wa Manispaa walifika kiwandani hapo, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wakazi wa eneo hilo, kufuatia harufu kali ya nyeti hizo, ambazo zilikutwa zimeanikwa ili kuzikausha.
Pia maofisa hao walikuta pembe za ng’ombe zimefungwa kwenye viroba. Maofisa hao walipofika kiwandani hapo, waligonga kwa muda mrefu, kisha walifungua vijana ambao walikuwa wakikusanya taka hizo na kwenda kuzitupa. Baada ya ukaguzi wa kiwanda hicho, maofisa hao wa manispaa walikuta raia wawili wa China, ambao awali walijifanya hawajui Kiswahili.
Mmoja wao alianza kuongea, ingawa baadaye alimwita mkalimani. Msimamizi wa kiwanda hicho, aliyejitambulisha kwa jina la Faing Zhou, alisema nyeti hizo wanazipata machinjioni na zinakusanywa kwa ajili ya kupelekwa China kwa ajili ya chakula cha mbwa.
Pia, alisema pembe za ng’ombe zinapelekwa China kwa ajili ya kutengenezea vifungo vya nguo, vitana na vitu vingine ambavyo hakuvitaja. Hata hivyo, vijana waliokuwa katika eneo hilo, walidai kuwa nyeti hizo zinapelekwa China kwa ajili ya kutengeneza dawa za kuongeza nguvu za kiume, jambo ambalo mchina huyo alisema sio kweli.
Wachina hao walipotakiwa kutoa vibali vya kufanya shughuli hizo, walidai hawana kibali chochote na kwamba walikuwa katika mchakato wa kupata vibali hivyo. Hata hivyo, Wachina hao walikuwa na vibali vya kufanya biashara za vyombo vya ndani katika Mtaa wa Aggrey uliopo Kariakoo.
Ofisa Mazingira wa Manispaa ya Ilala, Feada Magesa akimfafanulia raia huyo wa China ambaye ni msimamizi wa kiwanda hicho, alisema kulingana na mazingira hayo kuwa machafu mno, yanayohatarisha maisha ya wakazi wa eneo hilo, ikizingatiwa nje ya kiwanda hicho kuna shule ya msingi, kiwanda kinafungwa sambamba na kupigwa faini hiyo.
Ofisa wa Afya wa Kata ya Tabata, Jacob Mjata alisema wamefanya ukaguzi na kukuta hali mbaya katika kiwanda hicho, ambacho kinakausha nyeti na pembe za ng’ombe kiholela.
“Tulifanya ukaguzi katika eneo la kiwanda hiki na kukuta uchafu wa mazingira kupelekea majirani kuishi maisha magumu kufuatia harufu kali na inzi wengi wanaotoka kiwandani hapo,” alisema Mjata.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!