Friday 4 September 2015

WATAKAOLETA VURUGU KUKIONA"



Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki, amesema kwamba serikali ina taarifa kwamba kuna kundi la vijana ambalo litafanya vurugu wakati huu wa kampeni za uchaguzi na siku ya uchaguzi.



 
Hata hivyo, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limesema halina taarifa zozote kuhusu vurugu hizo.
 
Sadiki alitoa taarifa hiyo jana katika mkutano wa kampeni wa mgombea mwenza wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan, katika viwanja vya Mbagala Charambe jimbo la Mbagala.
 
Kada huyo wa CCM ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Dar es Salaam, alipanda jukwaani na kuwahutubia wananchi waliokusanyika kumsikiliza Samia ikiwa siku ya kwanza ya kampeni za chama hicho katika Mkoa wa Dar es Salaam.
 
Hata hivyo, Sadiki hakufafanua vijana hao wameandaliwa na nani wala maeneo waliyoko. Pia hakueleza kama ni kutoka vikundi vya uhalifu wala vyama vya siasa zaidi ya kusema kuwa wameandaliwa kufanya fujo. 
 
POLISI WASEMA HAWANA TAARIFA
Alipotafutwa  Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, kuzungumzia suala hilo alisema hawezi kulizungumzia kwa kuwa bado hajapatiwa taarifa na kuahidi kuwa atakapopatiwa taarifa, atalitolea ufafanuzi.
 
“Sijaisikia hilo suala, siwezi kulizungumzia mpaka nitakapopata taarifa nitaliongelea,” alisema Kamanda Kova.
 
Kamanda Kova alisema ni vyema atafutwe Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Temeke ili alitolee ufafanuzi.
 
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Ramadhani Madabida, alisema wanawake na vijana wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ukosefu wa ajira.
 
Akizungumza kabla ya kumkaribisha mgombea mwenza,  alisema CCM inajua changamoto hizo na kwamba mgombea mwenza akiingia Ikulu atazitatua akishirikiana na mgombea urais wa CCM, Dk. John Magufuli.
 
SAMIA AMWAGA AHADI MBAGALA
Akizungumza na wananchi wa jimbo la Mbagala, Samia alisema Mbagala siyo kituo cha utalii ambacho wanasiasa wanaweza kwenda na kupiga picha.
 
Alisema atahakikisha anatatua kero ya foleni ya magari ikiwamo kujenga barabara ya Mbagala hadi Kongowe.
 
Pia, aliahidi kujenga soko katika eneo la Temeke pamoja na Kijichi ili kutoa nafasi 5,000 kwa wafanyabiashara kufanya biashara.
 
Kuhusu usumbufu kwa wafanyabiashara  ndogo ndogo jijini Dar es Salaam, alisema hakuna mtu atakayebughudhiwa ikiwamo kulipishwa kodi zinazoleta usumbufu.
 
Aliahidi kuwaunganisha wafanyabishara katika benki mbalimbali ili wapatiwe mikopo ya kuanzisha na kuendeleza biashara.
 
Akizungumzia tatizo la ukoesfu wa maji, Samia alisema katika Jiji la Dar es Salaam kero hiyo itamalizika haraka watakapoingia Ikulu.
 
Samia alisema asilimia 30 ya tenda zote za halmashauri watahakikisha zinatolewa kwa wananchi wa kawaida ambao wananishi katika eneo husika.
 
Akizungumzia msongamano, Samia alisema tatizo hilo litaisha haraka watakapoingia Ikulu kwa kuwa watajenga barabara za juu pamoja na kusimamia usafiri wa reli.
 
MGOMBEA UBUNGE
Akizungumza katika mkutano huo, mgombea wa ubunge wa Jimbo la Mbagala (CCM), Issa Mangungu, alisema jimbo hilo linakabiliwa na uhaba wa vifaa vya ujenzi ukiwamo mchanga.
 
Kuhusu tatizo la barabara, Mangungu aliomba kujengwa njia mbili kutoka Mbagala hadi Kongowe ili kumaliza kero hiyo.
 
MGOMBE UDIWANI
Mgombea udiwani katika Kata ya Kilungule, Said Fela maarufu kama mkubwa Fela, alisema anajua matatizo mbalimbali yanayowakabili wananchi.
 
Fela ni mmmiliki wa bendi maarufu ya Yamoto ambayo imepata umaarufu kwa makundi yote wakiwamo wanawake na vijana.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!