Walinzi wa Rais wa Mpito Nchini Burkina Faso wamepindua Serikali, walivamia kikao cha Baraza la Mawaziri na kuwaweka chini ya Ulinzi Rais pamoja na Waziri Mkuu
-Milio ya Risasi imeanza kusikika katikati ya Jiji la Ouagadougou
Kikosi cha walinzi wa rais kimetangaza katika runinga ya taifa kwamba kimevunjilia mbali kile ilichokitaja kuwa serikali ya mpito isiyoambilika.
Mwanachama wa kikosi hicho jenerali Gilbert Diendere ametajwa kuwa kiongozi mpya wa mpito.
Mipaka yote imefungwa huku amri ya kutotoka nje ikiwekwa.Mkuu wa bunge amelitaka jeshi kuingilia kati ili kuzuia hatua hiyo aliyoitaja kuwa ya kundi dogo la wanajeshi.
Kikosi cha walinzi wa rais kimefyatua risasi hewani katika mji mkuu wa Ouagadougou huku watu wakikongamana kufanya maandamano.
Rais wa mpito Michel Kafando amepokonywa madaraka yake huku serikali yake ikivunjiliwa mbali, kwa mujibu wa afisa mmoja wa jeshi aliyezungumza katika runinga ya taifa nchini humo RTB.
''Tumeweka baraza la kitaifa la demokrasia litakalopanga uchaguzi wa kidemokrasia,'' alisema afisa huyo aliyevaa sare za kijeshi ambaye hakutambulika.
Hatua hiyo inajiri baada ya viongozi wa serikali hiyo ya mpito nchini Burkina Faso kuzuiliwa na walinzi wanaomtii aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo Blaise Campaore aliyeng'atuliwa mamlakani.
Hakuna majeraha yalioripotiwa lakini kumedaiwa kuwepo kwa hali ya wasiwasi huku maduka yakifunga biashara mapema na raia wengi kuelekea majumbani mwao.
Maandamano ya ghasia yaliyoshirikisha kulichoma bunge yalimshinikiza rais aliyehudumu kwa mda mrefu Campaore kung'atuka mamlakani mnamo mwezi Octoba mwaka 2014.
Bwana kafando na luteni kanali Zida walipewa jukumu la kuandaa uchaguzi mpya wa urais mwezi ujao.
Wao pamoja na maafisa wengine walitekwa nyara na walinzi wa RSP, mkuu wa bunge la mpito Moumina Cherrif Sy,alisema katika taarifa.
No comments:
Post a Comment