Mzee Rashid Mfaume Kawawa ‘Simba wa Vita’ ni mwanasiasa mkongwe alisimamia kikamilifu utekelezaji wa majukumu ya Serikali aliyokabidhiwa kwa nidhamu, uadilifu na bila woga hapa nchini.
Hakika alikuwa ni miongoni mwa viongozi wachache wazalendo, jasiri na mhimili mkubwa wa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, wakati wa harakati ya kupigania uhuru wa Tanganyika dhidi ya Wakoloni wa Uingereza.
Alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Serikali ya Tanganyika mwaka 1962 na Tanzania 1972 hadi 1977, Makamu wa Pili wa Rais na Waziri wa Ulinzi na JKT 1977 mpaka 1980.
Alizaliwa Mei 27, mwaka 1926 Kijiji cha Matepwende, Tanganyika na alifariki Desemba 31, 2009 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam akiwa na umri wa miaka 83.
Watanzania wanamkumbuka Mzee Kawawa kutokana na harakati zake katika utekelezaji wa majukumu ya chama na Serikali kitaifa na kimataifa hapa nchini.
Uanzishwaji wa JKT
Mzee Kawawa alisimamia kikamilifu uanzishwaji wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Julai 10 mwaka 1963, baada ya kufanyika uamuzi sahihi wa viongozi.
Kuanzishwa kwake kulitokana na mawazo ya Marehemu Mzee Kawawa ‘Simba wa Vita,’ baada ya kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Bi. Gold Meir, katika sherehe za uhuru nchini Ghana.
‘Simba wa Vita,’ alikuwa nchini humo akiwakilisha Chama cha Wafanyakazi wa Tanganyika (TFL), akifuatana na Mwalimu Nyerere kwa tiketi ya Tanganyika African National Union (TANU).
Kiongozi huyo wa Israel, ambaye aliwahi kuwa Waziri Mkuu nchini humo, alimwalika Mzee Kawawa kwa chakula cha jioni, ambapo walipata fursa ya kuzungumza umuhimu wa JKT na jinsi vijana wanavyoandaliwa kutumikia nchi yao kwa uzalendo, uadilifu, moyo na nidhamu katika suala zima la malezi.
Mzee Kawawa alirejea hotelini , alimweleza Mwalimu Nyerere, kuhusu mkutano wao na jinsi Israel wanavyowaandaa vijana kutumikia taifa lao kwa njia ya kujitolea.
Aliporudi nchini Tanganyika, mawazo yake aliyapeleka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Tanganyika African National Union (TANU Youth League), Hayati Joseph Nyerere, ambaye aliyafikisha katika Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika mkoani Tabora Agosti 25,1962.
Mkutano huo uliafiki mawazo ya viongozi hao na Aprili 19, 1963, Baraza la Mawaziri la Tanganyika chini ya Rais wa Jamhuri ya Tanganyika, Mwalimu Nyerere, lilipitisha azimio la umoja huo.
Mnamo Julai 10, 1963 JKT ilianza kutekeleza majukumu yake kwa kuwachukua vijana kutoka mikoa mbalimbali ya nchi kujiunga na jeshi hilo na kundi la awali la vijana 11 kutoka wilaya 11 walipata mafunzo Kambi ya JKT Mgulani Dar es Salaam.
Kuanzishwa kwa chombo hicho, kulilenga umoja wa kitaifa, kuwapatia mafunzo ya kijeshi na stadi za maisha vijana waweze kulitumikia taifa lao kwa ukakamavu na uzalendo katika nyanja mbalimbali za uchumi, jamii, kilimo, ulinzi na usalama wa taifa.
Malengo mengine yalikuwa ni kujenga mshikamano, udugu, kujitegemea, kuongeza ufanisi wa kazi, nidhamu, kujituma na kuwaandaa vijana kulitumikia taifa kupitia sekta binafsi na vyombo vya ulinzi na usalama kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla.
JKT ilifanikiwa kutimiza malengo yake kitaifa na kimataifa kuwakomboa wananchi kiitikadi, kielimu, kisaikolojia, kiutamaduni, kiutendaji na kwamba hakukuwa na ubaguzi ulioruhusiwa kuota mizizi miongoni mwa jamii.
Wananchi walijenga imani kubwa kwa JKT kulingana na utendaji kazi wake kwa kujali jamii katika masuala ya maafa, kujitolea katika mambo mbalimbali, ikiwamo ufundishaji wa elimu ya watu wazima, ujenzi wa makazi na uelimishaji umma dhidi ya magonjwa, kilimo na utunzaji mazingira.
Msaada wa mafunzo kutoka Israeli
Itakumbukwa kwamba Serikali iliomba nchini Israeli kuwafunza viongozi kuhusu uendeshaji wa JKT, ambapo mwaka 1960, baadhi ya vijana walipelekwa nchini humo.
Miongoni mwao walikuwa ni aliyewahi kuwa Mkuu wa JKT, Marehemu Meja Jenerali Makame Rashid Nalihinga, Brigedia Jenerali (mstaafu) Dismas Msilu na Marehemu Brigedia Jenerali Irungi Athumani Msonge.
Pamoja na Israeli kuleta wataalamu wake hapa nchini kwa ajili ya utoaji mafunzo zaidi, Serikali ilipanua wigo kwa kupeleka vijana katika nchi za Bulgaria na Yugoslavia kujifunza mbinu mbadala kuhusu suala zima la malezi.
JKT ilipoanza kutekeleza majukumu yake, iliwachukua vijana wa kujitolea kutoka mikoa mbalimbali ya nchi na baadaye wasomi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa mujibu wa sheria.
Mwandishi wa makala hii, alipata fursa ya kuzungumza na Mzee Kawawa nyumbani kwake kijijini Madale mwaka 2006, enzi ya uhai wake, ambapo anasema, vijana wasomi waligoma kwenda JKT kwa kutofahamu umuhimu wake na waliandamana.
Pamoja na Bunge la Tanzania kuridhia wasomi kwenda JKT mwaka 1967, Mwalimu Nyerere alitetea uamuzi wa Serikali wa kuridhia mafunzo hayo, hivyo vijana waliokaidi amri hiyo walirejeshwa kwa wazazi wao kutafakari kitendo chao cha kugoma.
‘Simba wa Vita’ anakumbuka jinsi Bw.Ali Said Mchumo, baada ya kuhitimu elimu yake Chuo Kikuu alimfuata akiomba apelekwe JKT akajitolee.
Kijana huyo ambaye aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali s e r i k a l i n i , a l i t a k i w a kuthibitisha kauli yake kwa kuja na wazazi wake, ambao waliridhia mtoto wao aende JKT.
Anasema , baada ya kuthibitika alikwenda kumpa taarifa Mwalimu Nyerere kuhusu ujasiri aliouonyesha kijana huyo, ambao uliridhiwa na viongozi hao na alikubaliwa kujiunga na jeshi hilo akamilishe dhamira yake.
Mzee Kawawa alijiunga JKT
Ilikuwa ni mwaka 1967, Mzee Kawawa na viongozi wenzake walifanya uamuzi sahihi kujiunga na JKT Kambi ya Ruvu mkoani Pwani, wakionyesha mfano, jambo ambalo haikuwa rahisi kutokana na uzito wa majukumu yao kitaifa.
Licha ya kukutana na mikasa mbalimbali jeshini, alifikia uamuzi huo kutokana na umuhimu wa taasisi hiyo kwa manufaa ya taifa, kwani kila mtu alipaswa kupitia mafunzo ya JKT kabla ya kuajiriwa katika sekta ya umma ama binafsi.
Aliwataja viongozi hao kuwa ni pamoja na Waziri Mkuu, Marehemu Edward Moringe Sokoine, Mzee Aboud Jumbe Mwinyi na Chifu Adamu Sapi Mkwawa.
“Tulipofika mlangoni, ilibidi tusahau vyeo na madaraka yetu wakati ule, tulibeba mizigo yetu, tulipiga kwata na mazoezi mbalimbali ya kijeshi kama tulivyotakiwa na makamanda wetu,” anafafanua.
“Makamanda wale walikuwa wachungu, hawasikii wala kujali umbile wala cheo cha mtu, wao walijali nidhamu na kufuatwa kwa maelekezo,” anaeleza Mzee Kawawa.
Anasema kuwa, awali alipoingia Kambi ya JKT Ruvu, akiwa na nywele nyingi, aliambiwa azikate mwanajeshi hatakiwi kuwa nazo, hali iliyosababisha kamanda mmoja wa kike kuzikata kwa mkasi bila ya huruma, hivyo alitii amri hiyo.
“Mimi enzi ya ujana wangu nilipendelea sana kufuga nywele ndefu na sikuwahi kuzikata kwa kipindi cha mwaka mzima, sasa ghafla afande anazikata bila ya huruma,” anasema.
Wakati anajiunga na JKT, Mzee Kawawa alihudhuria vipindi mbalimbali bila ya kutoroka, hata alipokuwa anachelewa kwa udhuru makamanda walimtafuta, hali iliyotokana na umaarufu wa nyadhifa zake za Makamu wa Pili wa Rais na Waziri Mkuu wa Tanzania.
Hali hiyo ilimjengea heshima na uaminifu miongoni mwa viongozi wenzake na makamanda wakati wa mafunzo na alikuwa mfano wa kuigwa na wenzake.
Anaeleza kwamba, wakati fulani alichukua chupa ya chai na kwenda nayo nyuma ya bweni lake kujipatia stafutahi, kabla hajamaliza alitokea afande aliyejulikana ‘Afande Ubwabwa,’ ambaye aliamuru ampatie chupa hiyo.
Pamoja na kutii amri halali ya kiongozi wake, chupa hiyo ilivunjwa mbele yake na kumwamuru haraka akajiunge na wenzake katika foleni tayari kwenda porini kusenya kuni za kupikia.
Baada ya kuhitimu mafunzo ya awali ya kijeshi, Mzee Kawawa alipelekwa Kijiji cha Kitaya Mkoani Ruvuma kuimarisha ulinzi mpaka kati ya Msumbiji na Tanzania.
Kudumishwa kwa ulinzi katika mpaka huo, kulitokana na majeshi ya Ureno kuvuka mpaka mara kwa mara, hivyo kusababisha uharibifu wa mali na usumbufu kwa wananchi.
Anaeleza Mzee Kawawa kuwa, akiwa huko, alikutana n a Mk u u wa Ma j e s h i (mstaafu), Jenerali Sam Hagai Sarakikya, ambaye aliwaeleza hali tete ya usalama mpakani, hivyo walitakiwa kuchukua tahadhari.
Akiwa askari alijiamini hasa baada ya kukabidhiwa bunduki na risasi za moto tayari kukabiliana na adui, ingawa jeuri yao ilivurugwa na mnyama kiboko aliyekivuruga kikundi chao.
Alikuwa ameweka risasi chemba tayari kwa kupiga bila ya kuangalia usalama mbele yake, Jenerali Sarakikya alitoa amri kuwataka askari waliokuwa nyuma kutofyatua risasi, licha ya mnyama huyo kuuawa na askari aliyekuwa mbele yake.
JKT muhimu kwa malezi
“JKT imefanya mambo mengi mazuri katika kujenga taifa letu, ambapo limepata sifa kubwa ndani na nje ya Bara la Afrika kutokana na mshikamano na umoja wetu,” anasisitiza.
Anasema hatua mbalimbali zilizochukuliwa na viongozi waasisi wa taifa letu chini ya Mwalimu Nyerere kupiga vita tabia zenye kujenga chuki, kuleta mgawanyiko, tofauti ya kipato, elimu, jinsia, kabila na dini ni lazima zidumishwe.
Pamoja na mafunzo ya JKT kusimamishwa mwaka 1994 na kurudishwa tena mwaka 2001, ilikuwa ni hatua muhimu kuendeleza mazuri yaliyoachwa na waasisi wetu kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo waweze kufahamu tulikotoka, tulipo na tuendako bila ya kurubuniwa na mataifa mengine kifikra, kiuchumi, kielimu na kisiasa kuleta uvunjifu wa amani nchini.
No comments:
Post a Comment