Friday 4 September 2015

MICHEZO: HAWA NDIO NYOTA WATATU WA KUIUA NIGERIA

Wachezaji hao ni Mbwana Samatta, John Bocco na

Dar es Salaam. Wakati timu ya Taifa ya Tanzania, ‘Taifa Stars’ ikijiandaa kuikabili Nigeria, wachezaji watatu au wanne wameonekana ndiyo watakaoamua mechi hiyo mapema endapo watacheza katika ubora wao. Wachezaji hao, Mbwana Samatta, John Bocco na Thomas Ulimwengu ndiyo pekee wameshikilia mkononi roho za Watanzania ili kuhakikisha wanaipa ushindi wa mapema Stars.


Stars inaikabili Super Eagles ya Nigeria Jumamosi katika mchezo wa kuwania tiketi ya kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka 2017. Timu hiyo ilirejea jana saa 9 alfajiri ikitokea Istanbul, Uturuki ilikoweka kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo huo dhidi ya Nigeria utakaochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchambuzi masuala ya soka, Joseph Kanakamfumu aliliambia gazeti hili jana kuwa mchezaji pekee anayeweza kuamua mchezo huo kwa kuleta matokeo mazuri ni Samatta. Kanakamfumu alisema Samatta ndiye atabeba matumaini ya Watanzania, lakini kama ataamua kucheza mpira kwa kiwango ambacho amekuwa akikionyesha akiwa TP Mazembe.
Kwa upande wake, Ally Mayay anawataja Samatta, Ulimwengu na Mrisho Ngassa kama wachezaji wanaoweza kuibeba Stars.
Alisema tatizo la Stars siyo ulinzi wala kiungo, isipokuwa washambuliaji ambao wanakosa umakini wa kutumia nafasi zinazopatikana. Kulingana na Nigeria ilivyo na kikosi imara cha wachezaji wengi wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi hiyo, Stars haiko nyuma kwani inao wachezaji inaowategemea kuleta furaha kwa mashabiki.
Samatta, Ulimwengu wanaocheza soka la kulipwa kwenye klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), tayari wamewasili nchini na Ngassa anayecheza soka ya kulipwa Afrika Kusini akisubiriwa.
Enyeama ‘aiogopa’ Stars
Wakati huohuo, nahodha na kipa wa Nigeria, Vincent Enyeama amejitoa kwenye kikosi kitakachoivaa Taifa Stars, Jumamosi.
Mtandao wa Supersport.com umekariri vyanzo kutoka kambi ya Super Eagles mjini Abuja ukieleza kuwa kipa huyo mwenye miaka 33 amejiondoa kwa sababu za kifamilia.
Kujitoa kwa Enyeama kunaifanya Super Eagles kumuita kipa Carl Ikeme wa Wolves au Ikechukwu Ezenwa wa Sunshine Stars.

MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!