
MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
LIGI Kuu ya Tanzania Bara msimu wa 2015/2016 unaanza kesho Jumamosi kwa viwanja saba tofauti.
Katika mechi zitakazochezwa kesho timu ya Ndanda FC itaikaribisha Mgambo Shooting, katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, African Sports ‘Wana Kimanumanu’, watakuwa nyumbani katika Uwanja wa Mkwakwani,Tanga kuwakabili Simba huku Majimaji ikiwa katika Uwanja wa Majimaji mkoani Ruvuma itaikaribisha JKT Ruvu.
Azam FC watakuwa katika uwanja wake wa Azam Complex, Dar es Salaam kuwakabili maafande wa Tanzania Prisons, huku Stand United wakiwa nyumbani katika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga kuikaribisha Mtibwa Sugar.
Toto African ‘Wana Kishamapanda’ watakuwa katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kuwakaribisha Mwadui ya Shinyanga, huku katika Uwanja wa Sokoine, wenyeji Mbeya City watakuwa kibaruani kuwakabili Kagera Sugar.
Mabingwa watetezi wa taji hilo, timu ya Yanga wenyewe wataanza harakati za kulibakisha taji hilo mitaa ya Jangwani na Twiga, watakapocheza na Coastal Union ya Tanga katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.













No comments:
Post a Comment