Friday, 18 September 2015

KIFAA CHA KULIPIA FAINI BARABARANI CHAANZA KUFANYA KAZI

Askari wa Usalama Barabarani akimuandika faini

Kikosi cha Usalama Barabarani kwa kushirikiana na Kampuni ya Max malipo, wamezindua kifaa cha kielektoniki cha kufanyia malipo madereva wa magari wanaovunja sheria.



Kamanda wa Polisi wa kikosi hicho, Mohammed Mpinga alisema jana kuwa kifaa hicho kitaanza kutumika kwa majaribio Dar es Salaam.
“Hii imetokana na malalamiko kutoka kwa wamiliki wa magari na madereva kwamba wamekuwa wakilipishwa faini na askari wa barabarani pasipo kupewa risiti halali za Serikali,” alisema Mpinga.
Alisema kifaa hicho kitagundua gari bovu au dereva aliyevunja sheria kama vile kutovaa mkanda au kwenda mwendokasi.Kamanda Mpinga alisema taarifa zote zitachukuliwa pamoja na namba ya gari na kuhifadhiwa, haitakuwa rahisi kwa dereva aliyefanya kosa kukataa kwa sababu ataonyeshwa. “Ulipaji huu wa kielektroniki hauna tofauti sana na ule unaotumika kulipia bili za umeme, maji na ada za magari kwa njia ya mtandao na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA),” alisema.
Kamanda huyo alisema huduma hiyo itamwezesha mmiliki wa gari endapo ameazimisha mtu gari lake, kugundua kama limekamatwa na kutozwa pesa.
Kamanda Mpinga alisema dereva atakayebainika na kosa anatakiwa alipe faini ndani ya siku saba, zaidi hapo atatozwa asilimia 25 ya tozo ya awali na baada ya siku 14 na kuendelea atatozwa ziada ya asilimia 50 ya tozo ya awali.
Alisema dereva atakayeshindwa kulipa atakamatwa na kufikishwa mahakamani ambako atatakiwa kulipa faini ya Sh50,000 au kifungo cha miaka miwili jela.
“Kifaa hiki pia kitang’amua kama gari linadaiwa tozo ya ‘notification’ iliyolimbikizwa ama la na hatua zitachukuliwa ikibainika,” alisema Kamanda Mpinga.
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!