Saturday, 12 September 2015

JE NI KWELI MAVAZI HUBADILI AHALISIA WA MTU?



Hapo awali mavazi yalitumika kama stara tu, inasemekana kuwa Adam na Hawa walipoanza kupata hisia za haya,soni au aibu walitumia majani ya miti kujistiri.


Zingatia: Mavazi ni neno linalokusanya kila kitu kinachovaliwa au kuambatana na mvaaji; kwanzia nguo, vito, viatu, bali hata mwamvuli, mkoba na nk.
Mavazi ni moja kati ya mahitaji muhimu na ya dharura kwa wanadamu, kwa kawaida binadamu huwa hatenganishwi na mavazi kwanzia siku ya kuingia duniani na hata siku ya kuondoka duniani.
Kutokana na kutanuka jamii za wanadamu, mavazi yalipatikana kwa namna, rangi na miundo tofauti kulingana mila na desturi za jamii hizo.
Lakini kwa sasa kutokana na utandawazi na kuharibika mipaka ya kitamaduni kumekuwa na muingiliano wa mavazi na uigaji wa tamaduni za mavazi katika jamii nyingi, uigaji huu umeathiri jamii nyingi na kuleta tamaduni mpya za kuiga: kuna ambazo ni nzuri na zimekuwa zikisifiwa na wenye hekima na akili timamu na pia kuna ambazo si sahihi na zimekuwa zikionywa na wenye hekima.
tamaduni hizi mbovu zimekuwa zikifuatwa na watu wasiojifahamu nakudhani kwamba: kuiga tamaduni hizo kutawafanya waonekane kuwa wanakwenda na wakati, fasheni na kuonekana kuwa si washamba, bila ya kuzingatia kuwa tamaduni hizo zinakinzana na tamaduni zao asilia.
Tumeshuhudia wanaume wengi wakivaa mapambo,kushusha suruali nusu mlingoti (mtepe, mlegezo,kata K) pia tumeshuhudia wanawake wakivaa mazavi ya aibu, namengine mengi ambayo katika tamaduni zao yanaonekana kuwa ni mambo ya aibu lakini wanafanya hivyo ili tu waonekane kuwa wanakwenda na wakati.
Swali lakujiuliza ni kwamba Je mavazi yanaathari gani kwa mvaaji na yanatoa ujumbe gani kwa mtazamaji?
Ni kweli kwamba mavazi hubadilisha mtazamo na muonekano wa mvaaji, lakini huwa hayabadilishi uhalisia wa mvaaji, hata kama atajaribu kuigiza kuendana na mavazi hayo, kama vile ambavyo baadhi ya watu hubadilisha mwendo au hata namna ya kuzungumza kwa kuwa tu wamevaa mavazi ya namna flani.
Kwa upande wa mtazamaji, mara nyingi mtazamaji humfasili mtu kutokana na muonekano wa mavazi yake, kuna wakati mtu anaweza kuonekana muhuni au mtu mwenye adabu kutokana na mavazi yake ingawa inawezekana ikawa ni tofauti na uhalisia wa mtu huyo.
Kwani inawezekana mwizi akava kanzu au suti na akaonekana mtu wa heshima ilihali ni muhalifu, vivyohivyo yamikini kahaba akavaa hijabu au vitenge na khanga na kuonekana msichana mwenye haiba.
Hivyo ni muhimu ifahamike kuwa kuvaa mavazi flani hakubadilishi uhalisia wa mtu, pamoja na kuwa mara nyingi watu huvaa mavazi yanayoendana na hadhi zao, hivyo si busara kumhukumu mtu kwa mavazi yake kwani mavazi si ushahidi wa kutosha.
Hakuna shaka kwamba tuna haki na uhuru wa kuvaa mavazi tuyatakayo, lakini tunatakiwa kulinda mpangilio wa jamii, na si kujiangalia sisi kama sisi binafsi, kuvaa nguo za kuonyesha ndani au Kimini kunaweza kukufanya upate upepo wa kutosha na kujihisi vizuri, lakini kunahatarisha nidhamu na mpangilio wa jamii, kwani kunashawishi anasa na kuamsha hisia za vijana wasio na hatia na hivyo kuchochea vitendo vichafu katika jamii.
Kuvaa mlegezo kuna weza kukufanya uonekane kama Tupac au msanii flani kutoka Marekani au nchi nyingine zenye maendeleo, lakini pia kunashusha heshima ya familia yako na kukufanya kuonekana kibwagizo katika jamii yetu, ambayo mambo hayo yanaoneka kuwa ni mageni.
Ni muhimu kujua kuwa mavazi humpandisha au kumshusha mtu, humfanya mtu apendeze au kuchukiza, humfanya mtu aheshimike au kudharaulika.
Lakini tusisahu kwamba mavazi hayabadilishi uhalisia wa mtu, hivyo ni juu yako wewe ujitazame wewe binafsi au ujitazame wewe na jamii yako.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!