Friday, 18 September 2015

52 KORTINI KWA KUHARIBU MABANGO YA WAGOMBEA


Watu 52 wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma mbalimbali zikiwamo za kuharibu mabango ya wagombea.


 
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, tuhuma nyingine ni kujihusisha na matukio mengine ya kiuhalifu katika kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, mwaka huu zinazoendelea nchini.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Bulimba, alisema jumla ya matukio 107 ya vitendo vyenye muelekeo wa uvunjifu wa amani, vimeripotiwa katika jeshi hilo huku 38 kati ya hayo, yenye jumla ya watuhumiwa 52 yakifunguliwa kesi na kufikishwa mahakamani.
 
Hivi karibuni kumekuwapo na malalamiko ya wagombea mbalimbali wa vyama kuhusiana na vitendo vya kuharibiana mabango ya kampeni.
 
Malalamiko kuhusiana na matukio hayo yamekuwa yakivihusisha zaidi Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ambao unaundwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF), National League for Democracy (NLD) na NCCR-Mageuzi. 
 
Bulimba alisema matukio mengine 68 kati ya hayo, bado yako katika hatua ya upelelezi na kwamba idadi hiyo imepatikana kutokana na tathmini waliyoifanya nchi nzima baada ya kuanza rasmi kwa kampeni hizo Agosti 22, mwaka huu.
 
Alisema mbali na kuharibu mabango ya kampeni, wahusika wa matukio hayo ambao wengi ni wafuasi wa vyama, walishiriki pia kuwazomea wenzao wa vyama vingine wanapokwenda katika mikutano ya kampeni.
 
Pia kuendesha mafunzo yenye muelekeo wa kijeshi kwa wafuasi wa vyama vya siasa, kuchana bendera za vyama vya mahasimu wao pamoja na kutoa maneno ya uchochezi zikiwamo lugha za matusi.
 
Alitaja makosa mengine kuwa ni kuandika maneno katika matangazo ya kampeni yaliyobandikwa na wenzao, kuwazuia watu wengine kusoma matangazo hayo, kutishia kuua kwa maneno, kujeruhi na kufanya fujo kwenye mikutano ya kampeni.
 
Bulimba alisema tathmini yao ilibainisha kuwa tangu kuanza kwa kampeni za uchaguzi, hakuna tukio lolote kubwa na la kustua la uvunjifu wa amani na kwamba hadi sasa kampeni zinaendelea kufanyika katika hali ya amani na utulivu.
 
Katika hatua nyingine, Jeshi  hilo limetoa onyo kwa wananchi, vyama vya siasa na wafuasi wao kuzingatia sheria ya vyama vya siasa na miongozo mbalimbali ambayo imekuwa ikitolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kwa lengo la kufanikisha uchaguzi.

NIPASHE.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!