Sunday 2 August 2015

LOWASA AREJESHA FOMU YA KUGOMBEA URAIS


Mtangaza nia ya Urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, jana alipokelewa na mamia ya wanachama waliojitokeza kwenye ofisi za chama hicho, wakati akirejesha fomu kuwania nafasi hiyo.



Wanachama hao walimpokea kwa mabango yanayosomeka "Poverty is over by Lowassa", "kwa Lowassa hata wanyonge tutapata ajira", "Lowassa ni jembe", "Kingunge karibu Chadema".

Lowassa aliwasili kwenye ofisi za chama hicho saa 9.45 alasiri jana akisindikizwa na waendesha bodaboda huku akiwa ameambatana na familia yake pamoja na wapambe wanaomuunga mkono.

Fomu hizo zilipokelewa na Makamu Mwenyekiti Bara, Profesa Abdallah Safari.

Prof.  Safari alisema, kuna baadhi ya watu walipomuona Lowassa amechukua fomu juzi walitegemea ataugua au hatazirejesha lakini kwa sababu ni chaguo la Mungu ametekeleza.

Alisema kuwa Kamati Kuu ya chama itakutana leo na siku itakayofuata Baraza Kuu litakaa na hatimaye kuamua.

“Tunaamini hakutakuwa na pingamizi dhidi ya mgombea huyu kwa sababu mpaka sasa hakuna aliyechukua fomu ya kuwania Urais zaidi yake ndani ya Chadema na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),” alisema na kuongeza:

“Mbowe alisema CCM imekuwa washauri wetu hivyo asipokelewe Chadema, sasa hivi kinachoendelea wanatushauri tuelekeze nguvu kwenye  ubunge na udiwani. Wanataka Urais tujipange baadaye, ila tunawaambia chenga tutapiga na goli tutafunga,” alisema.

Kuhusu uchukuaji fomu ya Urais Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec), alisema watamsindikiza mgombea wao, baada ya Jumanne ijayo.

Profesa Safari alisema katika mikoa 32 ya kichama iliyopo kanda kumi iliyomdhamini Lowassa hadi jana imemwezesha kupata wadhamini 1,662,397.

Naibu Katibu Mkuu wa Taifa wa chama hicho upande wa Zanzibar, Salumu Mwalimu, alisema kuwa CCM haiwezi kuwachonganisha wala kuwavuruga na kwamba wanafahamu njama na mikakati yao.

“Lowassa hatujamwokota njiani bali ameongozwa na Mungu kuja Chadema, njama zote za CCM zitashindwa, sisi tutaongozwa na kiongozi anayechukia umaskini sio wao wanaojidai kupinga falsafa hii huku wakiiba pembeni,” alisema.

Kuhusu udhamini wa Lowassa, alisema kwa sababu  muda wa uchukuaji fomu ulikuwa mchache, waliongeza kipengele cha kuwataka wadhamini wake waandike namba za shahada za kupigia kura na za simu ili waliopo mikoani wapate fursa hiyo.

“Siku ya kwanza baada ya kuchukua fomu hapa makao makuu watu 700 walijitokeza kumdhamini ingawa tuliwaona 300 kutokana na muda,” alisema.

Wakitoa maoni yao mara baada ya Lowassa kuondoka kwenye ofisi hizo, Mbunge Ester Bulaya, alisema kuwa, uchaguzi mkuu watawashinda kwenye boksi la kura  bila upinzani.

Viongozi wengine waliohudhuria shughuli hiyo ni wabunge, waratibu wa kanda, viongozi wa mikoa , majimbo na wilaya.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!