Wednesday 15 July 2015

WALIOVAMIA MAJANGWANI WATAKIWA KUHAMA


Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Dar es Salaam, Isaya Mungurumi, amewataka wafanyabiashara waliovamia viwanja vya Jangwani kuondoka mara moja kutokana na kujimilikisha maeneo hayo kinyume cha sheria.


 
Alitoa agizo hilo jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari na kufafanua kuwa Manispaa ilikubaliana na Serikali kutenga sehemu ndogo katika viwanja hivyo kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo ili kupunguza msongamano katika soko la Kariakoo.
 
Aidha, alisema kitu cha kushangaza ni kuwa kabla ya manispasa kuanza ugawaji wa maeneo hayo kwa wafanyabiashara wadogo, kuna watu walijitokeza na kuwauzia wafanyabiashara wengine kinyume cha sheria na kusababisha kero kubwa.
 
“Nimeandaa timu ya kuwashughulikia watu hao, hivyo naomba waondoke eneo hilo mara moja kabla sheria haijachukuliwa dhidi yao, hatuwezi kuruhusu watu kuanza shughuli zao za kibiashara katika maeneo ambayo hayajaandaliwa na kuwekwa huduma muhimu za kibinadamu,” alisema Mngurumi.
 
Aliongeza kuwa baada ya maeneo hayo kutengwa na kuwa katika hali ya usafi, vitawekwa vyoo vya kuhamisha ili vitumike kwa wafanyabiashara na watu wote watakaotembelea maeneo hayo.
 
Mungurumi alisisitiza zaidi kuwa eneo litakalotumika ni moja na kubainisha kuwa maeneo yaliyopo karibu na ofisi za Dart hayaruhusiwi kuguswa na kuongeza kuwa utaratibu maalum utatumika kuyagawa maeneo yaliyopangwa kwa wafanyabiashara na siyo kuwamilikisha ili kutumika katika kipindi hiki cha kiangazi. 
 
Kadhalika, alisema Manispaa imeamua kutumia eneo hilo kutokana na wafanyabiashara wengi wadogo kupanga bidhaa zao barabarani hasa katika soko la Kariakoo hivyo kusababisha kero kwa watembea kwa miguu na wakati mwingine kufunga barabara kabisa na kusababisha msongamano wa magari.
 
Alisema wakati wakiwatafutia hifadhi ya muda wafanyabiashara hao, manispaa inajiandaa kujenga masoko matatu ili wawe na maeneo sahihi ya kufanyia shughuli zao.
 
Masoko yatayojengwa ni Kisutu, Mchikichini na Buguruni na kwamba mazungumzo yameanza na benki kwaajili ya kutoa mkopo kufanikisha mkakati huo unaotarajia kuanza mapema iwezekanavyo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!