Wednesday, 1 July 2015

WALIOMUUA ALBINO MWAKAJILA WA MBEYA LEO WAMEHUKUMIWA KUNYONGWA HADI KUFA


Hakimu Mwakalinga siku alipohukumiwa 
kunyongwa hadi kufa kwa mauaji 
ya Mwenyekiti
 wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe. 
Leo amehukumiwa tena kunyongwa
 mpaka kufa
 katika mauaji ya mlemavu wa ngozi 
Henry Mwakajila.



Na Daniel Mbega
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Mbeya leo hii imewahukumu kunyongwa mpaka kufa 
watu wanne kati ya watano waliomuua Henry Mwakajila (17) ambaye ni mlemavu wa ngozi
 (albino).


Waliohukumiwa kunyongwa mpaka kufa ni Asangalwisye Kayuni maarufu kama
 Katiti au Mwakatoga na Gerard Korosso Kalonge (wakazi wa Kijiji cha Mbembati wilayani
 Ileje), na Leonard Msalage Mwakisole na Hakimu Mselem Mwakalinga (wakazi wa Kiwira 
wilayani Rungwe).
Mshtakiwa wa nne, Mawazo Philemon Figomole, ameachiliwa huru na mahakama hiyo 
baada ya ushahidi wa upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha pasi na shaka kwamba
 alihusika katika mauaji hayo.
Akisoma hukumu ya kesi hiyo ya mauaji yenye kumbukumbu Namb. KIW/IR/49/2008
 na PI 5/2013, Jaji wa Mahakama Kuu Dk. Revila, amesema mahakama imejiridhisha
 pasi na shaka na ushahidi wa upande wa mashtaka kwamba washtakiwa hao wanne 
walitenda kosa hilo na hivyo wanastahili adhabu hiyo.
Hii ni kesi ya saba ya mauaji ya albino kutolewa hukumu ambapo mpaka sasa
 jumla ya watuhumiwa 15 wamehukumiwa kunyongwa mpaka kufa.
Ililezwa mahakamani hapo kwamba, mnamo Februari 5, 2008 majira ya saa 12:00
 na saa 1:00 jioni huko katika Kijiji cha Ilolo, Kata ya Kiwira, tarafa ya Ukukwe, 
wilayani Rungwe katika Mkoa wa Mbeya, washtakiwa hao walimteka nyara
 kijana Henry Mwakajila, ambaye ni mlemavu wa ngozi aliyekuwa akisoma kidato cha pili
 katika Shule ya Sekondari Ukukwe na kisha kumuua.
Wakati wa mwenendo wa kesi, ilielezwa na mashahidi wa upande wa mashtaka 
kwamba mshtakiwa wa kwanza Asangalwisye Kayuni maarufu kama Katiti au Mwakatoga
 ambaye ni mganga wa jadi, mkazi wa Kijiji cha Mbembati, Wilaya ya Ileje, alikutwa 
na utumbo unaodhaniwa kuwa wa binadamu na ulipopelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali
 ukathibitika kwamba ni utumbo wa marehemu Henry.
Mshtakiwa wa pili, Gerard Korosso Kalonge wa Kijiji cha Mbembati wilayani Ileje 
alikutwa na vidole vinne na mifupa kumi (10) vyote vinavyodhaniwa kuwa vya binadamu 
na baada ya uchunguzi wa Mkemia Mkuu wa Serikali ilibainika kwamba ni viungo
 vya marehemu Henry Mwakajila.
Ilielezwa pia kwamba, washtakiwa Leonard Msalage Mwakisole, Mawazo Philemon Figomole
 na Hakimu Mselem Mwakalinga ndio waliodaiwa kumteka nyara mtoto huyo na kumuua,
 kisha kupeleka viungo kwa mganga wa kienyeji Asangalwisye Kayuni.
Mshtakiwa wa tano, Hakimu Mselem Mwakalinga, tayari alikwishahukumiwa kunyongwa
 katika kesi nyingine ya mauaji ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe,
 John Mwankenja, ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi nyumbani kwake.
Hukumu ya kesi hiyo namba 131/2012 ilitolewa Novemba 13, 2013 ambapo inaelezwa 
kwamba watuhumiwa walitenda kosa hilo Mei 19, 2011 katika kijiji cha Mpandapanda,
 Kata ya Kiwira Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya.
Ingawa watuhumiwa walikuwa wanne, lakini Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya chini ya Jaji
 Samwel Karua iliwahukumu kunyongwa mpaka kufa mshtakiwa wa kwanza Hakimu 
Mwakalinga na mshtakiwa wa pili Daudi Mwasipasa kwa maelezo kwamba walihusika
 moja kwa moja na mauaji hayo ya kukusudia.
Mshtakiwa namba tatu Obote Mwanyingili yeye alitiwa hatiani kutokana na kosa
 la kumhifadhi mtuhumiwa namba moja baada ya kutoka kufanya mauaji wakati mshtakiwa
 namba nne Kelvin Myovela alitiwa hatiani kutokana na kuhifadhi silaha iliyotumika katika
 mauaji hayo ingawa hakusika na kitendo hicho moja kwa moja, hivyo wote wawili 
walihukumiwa kifungo cha miaka saba jela.
Hata hivyo, Myovela tayari alikwishahukumiwa kifungo cha miaka 20 jela kwa kukutwa
 na silaha kinyume cha sheria.
Inadaiwa kwamba, chanzo cha mauaji hayo ya John Mwankenja, ambaye pia alikuwa
 Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Wilaya ya Rungwe, kilitokana na kiongozi 
huyo kufahamu kwamba hao ndio waliomuua mlemavu wa ngozi Henry Mwakajila, 
hivyo aliuawa ili kupoteza ushahidi.


Imeandaliwa na mtandao wa www.brotherdanny.com

1 comment:

Anonymous said...

aziz bilal05:39


1


Binafsi bado kutosheka na hiyo hukumu, ingelitakiwa wanyongwe na pia ionyeshwe nchini kote ili watu wote wajionee ili iwe ndio fundisho kwa wote wauawe kwa kunadiwa mbele ya ulimwengu mzima lazima waaibishwe mbele ya ulimwengu,maana hawa washenzi wanachangia matusi tunayotukanwa sisi watz,mpaka sasa wengine tu nashindwa kujinasibu utanzania kwa kuhofia backlash za watu.Wangefanyiwa kitendo kibaya ili iwe fundisho kubwa kwa wengine,kama ni haki za binadamu je wao walikuwa wana haki gani ya kumuua mtu mwenye ulemavu wa ngozi?

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!