Friday, 3 July 2015

SHILINGI YAANZA KUIMARIKA SOKONI.

 
Siku mbili baada ya shilingi ya Tanzania kuanza kuimarika dhidi ya Dola, Waziri wa Fedha na Uchumi, Saada Mkuya amezitaja mbinu zilizochukuliwa ili kuiimarisha ikiwa ni pamoja na kuzuia uhamishwaji wa fedha kutoka benki moja kwenda nyingine kitaalamu ‘swapping.’

Waziri Mkuya alisema uhamishaji huo utafanyika pale tu kutakapokuwa na shughuli za kiuchumi.
“Benki zilikuwa zinahamisha fedha kutoka benki moja kwenda nyingine bila sababu za msingi za shughuli za kiuchumi, hii ilisababisha kushuka kwa shilingi lakini kwa sasa tumezuia na itafanyika pale  tu gavana atakapoidhinisha,” alisema.
Waziri Mkuya alisema kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuhakikisha shilingi inaimarika hivyo hayo ndiyo matokeo yake. “Hii ndiyo hatua tuliyochukua, mlitusema vibaya kwamba hatufanyi kazi lakini sisi tulikuwa tunachukua hatua kwa nafasi yetu,” alisema.
Shilingi ya Tanzania ilianza kuimarika juzi, kwani ilinunuliwa kati ya Sh1,700 na Sh1,900 badala ya Sh 2,400 ya awali dhidi ya dola moja ya Marekani.
Wiki iliyopita, mporomoko huo ulizua mtikisiko wa uchumi kiasi cha kuelezwa kuwa fedha hizo zingeweza kufikia kati ya Sh2,500 na Sh2,800 wakati huo nchi ikielekea kwenye Uchaguzi Mkuu.
Akizungumzia jitihada zilizochukuliwa, Waziri Mkuya alisema Serikali pia imepunguza uzuiaji wa dola kutoka asilimia 10 hadi nane ili kuipa nguvu shilingi.
“Serikali ilishika kiasi kikubwa cha fedha na sasa imepunguza asilimia 2, hiyo nayo imeleta unafuu,” alisema Waziri Mkuya.
Sababu  nyingine ya kuimarika kwa shilingi aliyoitaja Waziri Mkuya ni pamoja na kuongezeka kwa mzunguko wa fedha ambao ulikwamishwa kutokana na Bajeti ya Serikali na kusema kuwa kwa sasa fedha nyingi zimeshaingia katika mifuko ya bajeti.
Kuanguka kwa shilingi kulitokana na uchumi wa Marekani kukua jambo lililosababisha fedha za nchi nyingi kushuka ingawa alisema shilingi  ya Tanzania ilianguka zaidi.
Mkurugenzi wa Uchumi, Utafiti na Sera wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Dk Joseph Massawe, alikaririwa na gazeti la The Citizen juzi akisema kuwa shilingi imeimarika baada ya BoT kuingilia kati tatizo lililojitokeza.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!