Sunday, 19 July 2015

SAIKOLOJIA : je, Unajua kurekebisha mtindo wako wa kusoma kufuatana na malengo yako ya kusoma?

Je wakati mwingine unaposoma habari fulani huwa unashindwa kuelewa kilichokusudiwa? Je, hali hii huwa inatokea mara kwa mara au mara chache tu? Je, inapotokea hali hii huwa unafanya nini? Je unafikiri ni wewe tu unayekabiliwa na tatizo hili? Hata hivyo, usiwe na wasiwasi kwa kuwa wako watu wengi wanaokabiliwa na tatizo kama hili.

Siku chache zilizopita nilikuwa nazungumza na jamaa zangu ambao huwa wakipenda kusoma makala zangu na gazeti la Mwananchi kwa ujumla. Niliwauliza kama huwa wanaelewa wanachosoma bila matatizo yoyote. Wengi walisema kuwa wanaelewa kwa urahisi zaidi taarifa za habari kuliko makala maalumu. Kuna wachache walisema wao kwa ujumla huwa wanapata shida kuelewa kikamilifu kile wanachosoma.
Kwanza niliwakumbusha kuwa kusoma ni fani inayotaka ujuzi na ustadi kama zilivyo fani nyingine. Stadi hii hujengeka kutokana na dhamiri ya dhati na huweza kuimarishwa kwa mazoezi ya kutenda. Hivyo jambo muhimu kuliko yote ni kujizoeza kusoma sana hadi stadi ya kusoma na kuelewa ikajengeka katika akili kama vile kuwaza na kusema. Mwezi Julai mwaka jana niliandika makala mbili kuhusu jinsi ya kuboresha uwezo wa kusoma. Hata hivyo, nimegundua kuwa sikueleza kiasi cha kutosha kuhusu stadi ya kubadili au kurekebisha usomaji kufuatana na malengo ya kusoma.
Ni vyema tukumbuke kuwa kuna tofauti kubwa ya kuelewa kwa kumsikiliza mtu unayeongea naye ana kwa ana na kusoma habari iliyoandikwa. Unapoongea na mtu usipoelewa vyema alichokisema unaweza kumuuliza afafanue kile usichokielewa. Lakini unaposoma habari iliyoandikwa mwandishi hayuko mbele yako. Hivyo, huwezi kumuuliza amesema nini au kumuomba afafanue alichokisema katika maandishi. Unachoweza kufanya tu ni kurekebisha usomaji wako ili uweze kuelewa unachosoma.
Kutambua lengo la kusoma
Watu huwa wanasoma habari mbalimbali kwa malengo tofauti. Wewe unaposoma huwa na malengo gani? Lengo lako linaweza kuwa kupata haraka maana ya kile kifungu alichokisoma ili aweze kupata majibu ya maswali fulani. Hayo yanaweza kuwa maswali gani. Mathalan, kama unasoma habari katika gazeti maswali yanaweza kuwa kama vile tukio hilo lilitokea lini, wapi na nani aliyehusika. Mathalan, utataka kujua kinachoelezwa na kundi la maneno, ama sentensi zilizo katika habari hiyo. Hebu fikiria kama ungetakiwa kusoma habari ambayo hatimaye ungeulizwa maswali ili kupimwa kiasi ulichoelewa. Katika hali kama hiyo lengo mahsusi halitaishia tu katika kuelewa kile ulichosoma bali pia kukumbuka maudhui yake. Wakati mwingine lengo lako linaweza kuwa jepesi yaani unasoma aya au habari fulani ili kujua tu inahusu nini.
Unawezaje kubadili mtindo wako wa kusoma
Kabla hujaendelea kusoma makala hii hebu jiulize swali jingine. Je, wewe unaposoma makala za aina mbalimbali huwa unazisoma vilevile bila kujali tofauti zake. Kama hivyo ndivyo unavyofanya, kwa hakika huwa hausomi kwa kuzinngatia kanuni za usomaji mzuri. Wasomaji hodari huwa wakisoma kwa kubadilisha kasi ya usomaji kufuatana na malengo waliyonayo. Kuna wakati wanasoma polepole na wakati mwingine wanasoma kwa kasi ya wastani. Je unajua viwango hivi tofauti vya kasi ya usomaji huwa vinafaa kwa aina zipi habari.
Unaposoma habari kwa lengo la kupata taarifa mathalan kupata jibu kwa maswali maalum itakubidi usome kwa kasi hadi utakapoifikia sentensi, neno au kirai au tarakimu inayojibu swali ulilonalo katika fikara zako. Unapofika hapo soma aya au sehemu hiyo polepole na kwa makini ili uweze kuelewa maana iliyokusudiwa. Kila inapobidi rudia kuisoma tena sehemu hiyo kwa umakini zaidi ili uweze kutambua ulichokisoma na kukumbuka maudhui ya habari hiyo ambalo ndilo la lengo la kusoma habari hiyo.
Hebu tusome mfano kuu. Kwa mfano kama umekuwa ukisikia kijiji fulani kikisifiwa sana na ukahisi kuwa ukifika katika kijiji hicho utapata maarifa na ujuzi utakaokusaidia sana katika maisha yako. Lakini kila mara unapomtafuta mtu atakayeweza kukueleza kwa makini habari za kijiji hicho unashindwa kumpata. Hivyo unabaki na maswali mengi kichwani kuhusu kijiji hicho ambayo ungependelea kujua majibu yake.
Baada ya kutafakari kwa makini kuhusu kijiji hicho unagundua huna unaloweza kufanya ila kwenda hadi kwenye kijiji hicho. Kwa kuwa una gari unaamua kwenda kwa gari yako. Hata hivyo, unapoanza safari kuna jamaa yako anakudokezea kuwa kijiji hicho kiko mbali na kwamba barabara inayokwenda kwenye kijiji hicho inapita kwenye vijiji vingi lakini anakutajia baadhi ya dalili zitakazokufahamisha kijiji hicho. Kwa kuwa unakwenda kwa gari na njiani kuna vijiji vingi unalazimika kwenda kasi kwa sababu mbili kwanza ili usichelewe kukifikia kijiji unachokitaka. Sababu ya pili kwa kuwa hutaki kupoteza wakati wako kwa kuchunguza vijiji ambavyo hukuvikusudia. Baada ya muda unafika kwenye kijiji ambacho ulikuwa unatakiwa kukifikia. Unafanya haraka kukichunguza ili uone alama zitazokuthibitisha kuwa hicho ndicho kijiji ulichokuwa umetamani sana kukifikia.
Itakubidi sasa uende polepole huku ukichunguza kila kitu katika kijiji hicho. Wala hutoishia kukizungukia mara moja tu. Utarudia mara mbili au zaidi ili uweze kukielewa vyema jinsi kilivyo. Kwa kufanya hivyo utaweza kunufaika kwa mambo matatu kwanza ni kujua habari zinazokifanya kivutie watu wengi na kukisifu. Jambo la pili ni kukielewa vyema jinsi kilivyo na kupata majibu ya maswali uliyokuwa nayo. Jambo la tatu ni kupata elimu na maarifa kutoka kwenye kijiji hicho yatakayoweza kuwa na manufaa katika maisha yako. Kisa hiki kimetumika kama kielelezo cha kutuonyesha jinsi mbinu ya usomaji inavyoweza kubadiliswa kufuatana na lengo la kusoma. Kijiji kimetumika kama habari inayokusudiwa kusomwa, vijiji vingine vimetumika kuonyesha aya nyingine katika habari. Gari limetumika kama kitendo cha kusoma. Aidha, kutokana na mfano huu tunaweza kuwa tumeelewa ni wakati gani tunapaswa kusoma taratibu. Wakati lengo lako la kusoma sehemu ya habari fulani ni kuelewa tu inatoa ujumbe gani huna budi kusoma kwa kasi kuliko wakati unaposoma kwa kutafuta taarifa maalumu.
Pamoja na stadi hizi tulizojifunza kuna jambo moja muhimu la kuzingatia ambalo ni kuepuka kuufanya usomaji wako kuwa mgumu kwa kuzingatia sheria hadi ukaogopa hata kusoma. Kumbuka kusoma ni burudani, hususan unaposoma vitu kama hadithi, tamthilia na magazeti kwa lengo la kujifurahisha. Unaposoma kwa lengo la kujistarehesha soma haraka tu bila kujikalifu. Hata hivyo usisahau mambo mawili ambayo unatakiwa kuyazingatia ili uwe msomaji hodari. Kwanza soma sana kwa kuhakikisha unasoma karibuni kila siku bila kukosa ili ujijengee uwezo wa kusoma na kuelewa iwe tabia yako. Jambo la pili, kumbuka ikiwa unataka kuwa msomaji mahiri jifunze kutofautisha usomaji wako kulingana na malengo yako.
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!