Friday 24 July 2015

MIRAMBO: MTEMI ALIYEKUWA KIBOKO YA WAARABU


JINA la Mirambo ni maarufu sana hapa Tanzania na katika eneo lote la ukanda wa Afrika Mashariki. Lakini ni watu wachache wanaoweza kueleza Mirambo ni nani na alifanya nini hadi kustahili sifa kubwa kiasi hicho.

Kutokana na sifa hizo, hivi leo, kuna mtaa moja katika Jiji la Dar es Salaam uliopewa jina lake. Huko Tabora, Shule ya Sekondari na kambi ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) vimepewa jina la Mirambo. Kumbukumbu kama hizo zinaashiria kwamba Mirambo alikuwa ni mtu maarufu.
Katika kipindi hiki tunapoadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika, ambayo kwa wengi sasa hujulikana kama Tanzania Bara, ni vizuri kujikumbusha Mirambo alikuwa ni nani na alifanya nini wakati wa enzi zake hadi kujikusanyia sifa zote hizo.
Ni vizuri pia kujikumbusha kwamba wakati wa Mirambo, Tanganyika na baadaye Tanzania hazikuwapo, yeye aliishi katika kipindi ambapo eneo la Afrika Mashariki na Afrika nzima kwa ujumla ilitawaliwa na viongozi wa makabila au wafanyabiashara maarufu.
Mirambo ni miongoni mwa viongozi wa Afrika waliotokana na makabila yao kama vile Chifu Mkwawa  wa Wahehe, Shaka Zulu wa kabila la Wazulu, Kabaka Mutesa 1 wa kabila la Buganda na wengineo katika Afrika. Mirambo alikuwa ni Mnyamwezi.
Mtemi Mirambo alizaliwa kwenye miaka ya 1840 katika tawala ndogo ya Ukune katika eneo la Unyamwezi, Mkoa wa Tabora Tanzania. Baba yake alikuwa mtemi Kasanda wa Uyowa katika wilaya ya sasa ya Urambo. Mama yake aliitwa Masele Nyakasi au Nyakashi wa uzawa wa Mtemi Kifumigulu mkimbu kutoka Ikungu aliyefika Usumbwa na kuanzisha tawala ndogo ya Ukune. Kifumigulu alikuwa ni mtoto wa Mapokela Kiumbe I mtemi wa Ikungu.
Kifumigulu na ndugu yake Magokola waliondoka  Ikunga kwenda Usumbwa kuwinda tembo na kufanya biashara. Lakini baada ya kugundua kwamba wenyeji waliowakuta hawakuwa na nguvu, waliweza kuanzisha tawala mbili za Ukune na Uyogo.
Mirambo mwenyewe alizaliwa Ukune kwani Nyakasi alipokuwa na mimba na kwa sababu alikuwa ni mimba ya kwanza alirudi kwa wazazi wake kwenda kujifungua.
Nyakasi alijifungua mtoto wa kiume aliyepewa jina la Mbula Mtelya kwa mujibu wa Profesa Norman Bennett wa Chuo Kikuu cha Boston, Marekani.
Mirambo alikulia Uyowa na baba yake mtemi Kasanda alipofariki, Mirambo alirithi utawala wa Uyowa.
Kasanda alikuwa na Jeshi lake ambalo masimulizi yanaeleza kuwa aliliongoza kwa ushupavu mkubwa lakini kwa sababu Uyowa ilikuwa  ni tawala ndogo yenye watu wapatao 4,000 wakati Mirambo anatawazwa, hakuweza kuingia kwenye mapambano makubwa kama alivyofanya Mirambo baadaye. 
Kwa kutambua kikwazo hicho cha udogo wa tawala ya Uyowa aliyoirithi kutoka kwa baba yake, Mirambo aliamua kuondokana na kikwazo hicho. Miaka miwili tu baada ya kuwa mtemi wa Uyowa, Mirambo alivamia tawala ya jirani ya Ulyankulu na kuiunganisha na Uyowa na  kuzitawala zote mbili kwa pamoja. Baadaye tawala hizo mbili zilikujajulikana kama Urambo jina ambalo linatumika hadi leo.
Mirambo aliishi na kutawala katikati ya karne 19. Katika kipindi hicho mambo mengi yalikuwa yanatokea ulimwenguni ambayo yalianza kuligusa bara la Afrika ikiwemo Afrika Mashariki.
Huko Ulaya Wazungu walikuwa wameandaa kitu kilichojulikana kama uvumbuzi wa bara la Afrika. Kwa hiyo misafara ya watu kama akina Dk. David Livingstone, John Hannining Speke, Hanry Morton Stanley na Wamissionari kwa lengo la kueneza dini ya Kikristo ilianza kufika katika eneo la Afrika Mashariki.
Wakati huohuo Waarabu kutoka Oman walifika Zanzibar na kuifanya kitovu cha utawala wa himaya yao katika Afrika Mashariki.
Waarabu hapa Afrika Mashariki walianza  shughuli za biashara katika eneo lote la pwani na kuanza kuingia pia ndani ya bara la Afrika Mashariki kuelekea maziwa makuu na nchi ya Kongo.
Waarabu kutoka Zanzibar walifanya misafara yao kwenda Kongo kupitia Unyamwezi. Kwa hiyo watawala wa Kinyamwezi walijikuta katika ushindani wa kibiashara na Waarabu na Mtemi Mirambo alijikuta katika mazingira hayo.
Unyamwenzi ni eneo kubwa lakini wananchi wake waligawanyika katika tawala nyingi ndogondogo zilizo huru na zisizo na mshikamano. Hali hiyo ilizifanya tawala hizo kuwa dhaifu kijeshi na katika ushindani kibiashara. Biashara kubwa ya wakati huo ilikuwa ni Pembe za tembo, watumwa na shaba.
Watemi wengi wa Kinyamwezi walipeleka misafara pwani kwenda kuuza pembe za tembo na kisha kununua, nguo, majembe, mahitaji ya kijeshi, shanga na vitu vingine vya wakati huo.
Katikati ya karne ya 19 wafanyabiashara wa Kiarabu waliingia Unyamwezi wakiongozwa na Musa Mzuri ambao walifanya makazi yao Unyanyambe, moja ya tawala muhimu ya Unyamwezi.
Baadaye alifika Muhammad bin Juma, baba yake Tippu Tipu.  Muhammad Bin Juma alihalalisha ukazi wake Unyanyambe kwa kumuoa Kalunde, binti ya mtemi Fundikira I wa Unyanyembe. Hapo ndipo ushindani wa kibiashara kati ya Waarabu na Wanyamwezi ulipojitokeza kwa nguvu zaidi.
Mirambo hakupenda biashara yote idhibitiwe na waarabu na maliasili zichukuliwe bila ya wenyeji kufaidika nazo. Mirambo ameelezwa na waliomwona kuwa alikuwa na urefu wa wastani, mwenye mwili imara na mwenye akili nyingi na alikuwa tayari kusikiliza ushauri lakini uamuzi alifanya yeye. Mara akisha kuamua, Mirambo alitekeleza maamuzi bila kuchelewa.
Mirambo alikuwa mkatili na hakuvumilia utovu wa nidhamu miongoni mwa wasaidizi wake na wananchi kwa ujumla wake.
Katika mazingira ya kukabiliana na ushindani, Mirambo aligundua kuwa Uyowa na Ulyankulu peke yake zisingempa uwezo wa kupambana na wageni. Na kwa vile isingekuwa rahisi kuwaelimisha na kuwaunganisha Wanyamwezi kwa hiyari, alitumia nguvu za kijeshi.
Katika kipindi kifupi aliweza kuzivamia na kuziingiza chini ya himaya yake karibu tawala zote za Kinyamwezi isipokuwa Unyanyembe.
Wakati wa kilele cha mafanikio yake, Mirambo alidhibiti eneo lote kuanzia Ziwa Victoria hadi bonde la Ziwa Rukwa.
Katika eneo lote hilo hakuna msafara uliopita bila kibali cha mtemi Mirambo.
Katika mwaka 1871 Mirambo alijitokeza kama mtawala asiye na mpinzani katika ukanda wote wa Afrika Mashariki kufuatia mapambano kati yake na Waarabu walioweka ngome yao Unyanyambe.
Jamii ya Waarabu na Unyanyembe wakisaidiwa na Mtemi Mkasiwa waliandaa jeshi kubwa kupambana na Mirambo na kumaliza nguvu zake kabisa.
Lakini Kabla hatujaangalia kisa hiki ni vizuri kusimulia yaliyokuwa yanatokea Unyanyembe hadi kusababisha Mkasiwa (Mnyamwezi) kushirikiana na Waarabu kumwangamiza Mirambo.
Tumeona hapo awali kwamba Waarabu wa kwanza wakiongozwa na Mussa Mzuri walifika Unyanyembe wakati mtemi Fundikira I akitawala.
Baadaye jamii ya kiarabu na wa fanyabiashara wa Kiswahili ilipanuka hadi kumfanya Sultan wa Zanzibar kumteua Said bin Salim kuwa liwali wa Unyanyembe.
Katika kipindi hicho waarabu waliweka fungamano na mtawala wa Unyanyembe kwa Muhammad bin Juma (Baba wa Tippu Tip) kumuoa binti wa Mtemi Fundikira I Kalunde.
Bila ya watawala wa Unyanyembe kujijua, kuteuliwa kwa liwali kumwakilisha Sultan wa Zanzibar na mwarabu kumuoa mtoto wa mtemi, kulianza kupunguza nguvu za watawala wa Unyanyembe na hili lilijidhihirisha waziwazi baada ya kufa Mtemi Fundikira I mwaka 1858.
Baada ya Mtemi Fundikira I kufariki 1858 kulitokea msuguano nani arithi utemi wa Unyanyembe. Katika msuguano huo mshindani aliyeungwa mkono na jamii ya Waarabu alifanikiwa. Tayari Waarabu walisha anza kuwa na nguvu dhidi ya watawala wa Unyanyembe. Mtemi Msabila au Mnywa Sele kama alivyopenda kujiita yeye mwenyewe, alimrithi Fundikira 1 kwa msaada wa Waarabu.
Mtemi Mnywa Sele alikuwa mkakamavu, mpenda biashara na mzalendo kweli kweli wa Unyanyembe. Haukupita muda Mnywa Sele akagombana na washirika wake Waarabu baada ya kuanza kuwatoza kodi, kudhibiti biashara ya kwenda pwani na baadae kuzuia wasiuziwe nafaka. Mnywa Sele alisahau kuwa alifika hapo kwa nguvu ya Waarabu hao hao. Waarabu walipoona biashara na ustawi wao unatishiwa, mwaka 1860 walimpindua Mnywa Sele na badala yake wakamweka Mkasiwa kuwa mtemi wa Unyanyembe.
Mnywa Sele, kwanza alikimbilia Rubunga tawala ndogo kusini mwa Unyanyembe. Lakini Waarabu waliandaa jeshi na kwenda kumfukuza hapo nae akakimbilia Ukimbu ambako aliendesha vita vya msituni kwa miaka mitano akijaribu kurudi Unyanyembe bila mafanikio.
Katika jitihada za kujipatia mahitaji ya jeshi lake la ruga ruga, Mnywasele alianza kuvamia misafara ya kutoka pwani kwenda Unyanyembe.
Mwaka 1861 Speke alikutana na Mnywa Sele porini na la jeshi lake la ruga ruga. Speke alijaribu kutafuta suluhu kati ya Mnywa Sele na Waaraabu wa Unyanyembe bila mafanikio. Mnywa Sele aliuawa baada ya kushindwa na kukamatwa na msafara uliongozwa na Mwarabu Khamisi Bin Abdulla katika eneo kati ya Ugogo na Unyanyembe mwaka 1865.
Tukirudi Unyanyembe kwenyewe, watawala wa Unyanyembe hawakuridhishwa na kitendo cha Waarabu kumsaidia Mkasiwa kuwa mtemi wa Unyanyembe.
Wengi walimuona Mkasiwa kama pandikizi la Waarabu.
Mtemi Mirambo ambaye alivutiwa na sera za Mnywa Sele za kuwatoza kodi Waarabu na kudhibiti biashara katika Unyamwezi, alimuona Mkasiwa kama kibaraka wa Waarabu.
Katika kipindi chote ambacho Mnywa Sele alipigana msituni, Mirambo alimuunga mkono. Kwa hiyo uhasama kati ya Mirambo na Waarabu na Unyanyembe ulichukua sura mpya.
Baada ya kumpindua Mnywa Sele na baadae kuuawa, Waarabu waliona kikwazo pekee katika kudhibiti biashara na siasa za Unyamwezi ni Mirambo tu.
Mirambo aliendelea kuwatoza kadi Waarabu na misafara yote iliyokuwa ikipitia Urambo kwenda Ujiji. Wagogo nao walikuwa na bugudha kubwa kwa misafara ya kutoka pwani kwenda Ujiji kupitia Unyanyembe kwa kudai hongo.
Kwa hiyo Waarabu walijikuta katika mazingira magumu kibiashara na kiusalama.
Mwaka 1871 Waarabu waliandaa jeshi kumkabili Mirambo ili kufungua njia ya kwenda Ujiji.
Katika Kampeni hiyo Waarabu walisaidiwa na Mtemi Mkasiwa na mvumbuzi Henry M. Stanley ambaye msafara wake ulikuwa umezuiwa na Mirambo kwenda Ujiji kupitia Urambo.
Jeshi la wapiganaji 2255 kati yao1500 wakiwa na bunduki na waliobaki wakiwa na silaha za asili.
Kwa mujibu wa kumbukumbu za Stanley, Mirambo aliandaa rugaruga 1,000 akaunganisha na washirika wake Wangoni 1,500 kuwakabili Waarabu na washirika wao.
Baada ya kuombewa dua za kiislamu na tambiko za Kinyamwezi, Waarabu walianza mashambulizi kwa nyimbo za vita na tumbuizo za ngoma.
Mirambo kwa ushujaa wake na utaalamu wa mbinu za kivita aliamuru majeshi yake yasipigane kwa nguvu badala yake wawe wanarudi nyuma kama vile wamezidiwa.
Kwa mbinu hiyo aliweza kuwavuta wavamizi hadi wakafika karibu na  Ulyankulu  kwa upande wa kaskazini.
Baada ya kuona majeshi yote ya wavamizi yameingia katika himaya  yake, Mirambo aliamuru majeshi  yake yaanze kuishambulia.
Baada ya mapambano makali ya ana kwa ana jeshi la uvamizi lilivunjika na kusambaratika na kuanza kukimbia ovyo kurudi Unyanyembe bila ya mpangilio. Mirambo aliwafuata na askari wengi wa wavamizi waliuawa. Alipofika Unyanyembe, Mirambo aliharibu sehemu kubwa ya boma la Itetemia lakini hakuzingira sehemu alikojichimbia Mkasiwa wala sehemu alikokuweko Stanley.
Aidha Mirambo hakuharibu ngome za Waarabu. Lakini ghafla Mirambo aliisitisha mashambulizi ya Itetemia na kuamuru wanajeshi wake kurudi nyuma ingawa hakukuwa na upinzani mkali.
Hakuna maelezo yoyote kutoka kwa Mirambo kwa nini alisitisha mashambulizi ya Itetemia.
Kuna mawazo kwamba huenda Mirambo hakutaka kusababisha madhara yoyote kwa Stanley aliyekuwepo kwenye boma hilo na pia hakutaka kuingia kwenye mgogoro wa moja kwa moja na Sultani wa Unguja Zanzibar kwa kuwaangamiza Waarabu wa Unyanyembe.
Hata hivyo, wakati majeshi ya Mirambo yanarudi nyuma mwarabu moja, Khamisi bin Abdulla aliamurisha wafuasi wake kushambulia kwa kudhani majeshi ya Mirambo yalikuwa yameshindwa.
Alijidanganya. Mara moja majeshi ya Mirambo ya yalizingira ngome ya Mwarabu huyo na kuuwa wafuasi wake wote pamoja na yeye mwenyewe na kuharibu kabisa ngome yake.
Kitendo cha kutomgusa Stanley ambaye alikuwa amekimbiwa na watu wake na kuwaacha Waarabu salama kinaonyesha jinsi Mirambo alivyokuwa mwerevu. Hakutaka kuharibu uhusiano wake na jamii ya kimataifa.
Stanley alichukizwa sana na udhaifu walioonyesha Waarabu katika kampeni dhidi ya Mirambo ambaye alimwita ‘’ Jambazi” na pia ‘’Bonaparte wa Afrika,” akimlinganisha na mfalme Napoleon Bonaparte wa Ufaransa.
Stanley alichukizwa na kitendo cha Waarabu kumwingiza kwenye mapambano na Mirambo wakati wanajua hawana uwezo.
Stanley aliondoka Unyanyembe kwenda kusini ili kumkwepa Mirambo. Alipita Ukonongo kisha akaelekea magharibi na baadaye kaskazini hadi Ujiji alikomkuta Dk. David Livingstone mwaka 1871.
Ushindi wa Mirambo dhidi ya Waarabu wa Unyanyembe na washirika wao ulimfanya aonekane kama kiongozi asiye na mpinzani katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.
Yeye mwenyewe alijiita ‘Sultan Mkuu wa Afrika’. Uhasama kati ya Mirambo na Waarabu wa Unyanyembe uliendelea kwa kipindi chote cha uhai wa Mirambo.
Jaribio jingine la Mirambo la kuangamiza Unyanyembe na kuvunja kabisa nguvu za Waarabu lilishindwa. Septemba 1871 Mirambo alishambulia Unyanyembe kwa lengo la kuwasambaratisha Waarabu.
Katika mapigano yaliyofanyika katika kijiji cha Mfuto karibu kabisa na Unyanyembe, Mirambo alishindwa vibaya. Baadaye iligundulika kuwa, siku ile Mirambo aliongoza mapigano akiwa amelewa.
Inawezekana tukio hili ndilo lililomfanya Mirambo kuacha pombe kwani alimweleza mmisionari mmoja kuwa asingeweza kuendesha shughuli zote na kutawala watu wake vizuri kama angekuwa anakunywa pombe.
Kutokana na ushindi huo, Waarabu wa Unyanyembe waliamua sasa kumwangamiza Mirambo. Waliandaa jeshi kubwa lililojumuisha Waarabu wa Unyanyembe, kikosi kilicholetwa na Waarabu wa Usangu, Mtemi Mulimanombe wa Ugunda, Mtemi Simba Kaung’ando wa Usawila na askari 300 walioletwa na Mwarabu wa Ujiji, Said Bin Majid.
Said bin Majid alitaka kutumia mwanya huo kulipiza kisasi kutokana na Mirambo kumuua mtoto wake, Soud bin Majid na Mwarabu mashuhuri wa Unyanyembe Khamis bin Abdulla.
Khamis bid Abdulla ndiye aliyemuua Mnywa Sele (Msabila) ambaye Mirambo alimuona ndiye mtemi halali wa Unyanyembe na siyo Mkasiwa.
Kuongozea nguvu mtemi Mkasiwa alipeleka wa rugaruga kwenye jeshi la Waarabu na yeye mwenyewe alikuwepo kwenye mapambano yaliyoongozwa na Said bin Salim, liwali wa Unyanyembe kama mwakilishi wa Sultan wa Zanzabir.
Dk. David Livingstone akiwa Ujiji alipata habari kuwa jeshi la Waarabu lilikuwa na watu 2,000. Katikati ya Mwaka 1872 Waarabu walishambulia Urambo.
Mirambo alijua ukubwa wa jeshi la maadui lakini hakutishika sana.
Walipokuwa wanasogelea Urambo, Mirambo alifanya shambulio kubwa na kuwashinda Waarabu na mara kikosi chote cha wavamizi kilisambaratika na kiongozi wao, Said bin Salim akakimbia kurudi Unyanyembe.
Wapiganaji baada ya kuachwa na kiongozi wao, kila mmoja alirudi kwao kwa njia aliyojua mwenyewe.
Kushindwa kwa Waarabu katika kampeni hii ambayo ilionekana kuandaliwa vizuri, Mirambo alibaki bila tishio lolote katika udhibiti wake wa sehemu kubwa ya Unyamwezi.
Baadaye Mirambo alipata washirika wakusaidiana naye. Wa kwanza ni Nyungu ya Mawe ambaye awali alikuwa anazunguka na jeshi lake katika misitu ya Ukimbu bila ya kuwa na makao maalumu.
Kisha alishambulia tawala ya Ukimbu ya Kiwele na kuishinda na kujifanya mtemi wa Kiwele na kuburi lake liko huko hadi leo.
Mwingine ni mtemi Mtinginya wa Usongo. Mtinginya na Nyungu ya Mawe waliwahi kupigana lakini baadaye walipatana na kwa pamoja wakawa washirika wa Mirambo bila ya kuwa chini ya uongozi wa Mirambo dhidi ya Unyanyembe na Waarabu wake.
Mshirika wa tatu ni Simba Kaung’ando wa Usawila. Huyu pamoja na Mtemi wa Ugunda walimsaidia Mkasiwa na Waarabu wake kumshambulia Mirambo, lakini alibadilika na kufanya urafiki na Mirambo.
Kwa kushirikiana na Watemi, Mtinginya, Nyungu ya Mawe na Simba Kaung’ando, Mirambo alidhibiti njia zote za kwenda ziwa Tanganyika na Kongo na njia ya kaskazini kwenda Uganda.
Misafara yote iliyopita katika kipindi cha 1871 na 1879 ilifanywa hivyo kwa idhini yake na aliwatoza kodi. Kulikuwa na njia tatu, moja ilitoka pwani kupitia Ugogo na Unyamwezi  kaskazini kwenda Uganda.
Njia ya pili na maarufu ilipita Ugogo na Unyanyembe kwenda Ujiji na Kongo, na njia ya tatu ilipita Usagara, Usangu, Ukimbu hadi Karema katika Ziwa Tanganyika.
Mirambo na washirika wake, Mtinginya na Nyungu ya Mawe walidhibiti njia ya kati ya Ugogo na Unyanyembe na kaskazini kwenda Uganda.
Kwa upande wa Kusini kwa kushirikiana na Nyungu ya Mawe na Simba Kaung’ando walidhibiti njia ya kupitia Ukimbu kwenda ziwa Tanganyika.
Wamisionari wawili, Tom Cadenhead na Frederick Carter walipojaribu kumkwepa Mirambo kwa kupita njia ya kusini alipeleka jeshi lake kusini.
Kwanza alishambulia Ugunda iliyokuwa imesaidia Waarabu wa Unyanyembe na kisha akaingia Usawila bila ya mapigano kwa kuwa Simba Kaung’ando alifanya mapatano na Mirambo.
Baadaye majeshi ya Mirambo yakisaidiwa na majeshi ya Simba Kaung’ando yalimshambulia Mtemi Kasogela wa Upimbwe aliyekuwa amewapokea wamisionari hao wawili, Cadenhead na Carter.
Upimbwe iliangamizwa na wamisionari hao wawili wakauawa. Katika kampeni hiyo, Mirambo alikuwa pamoja na majeshi yake. Kwa tukio hilo njia ya kupitia Usangu na Ukimbu ikafungwa.
Kwa udhibiti huo, Waarabu wa Unyanyembe hawakuwa na hiyari isipokuwa kupata kibali cha Mirambo na kulipa kodi au ushuru wapate kufanya biashara katika eneo la Unyamwezi na hata kupitisha misafara kwenda Kongo.
Waarabu wa Unyanyembe hawakutaka tamaa katika harakati zao za kumwondoa Mirambo wapate uhuru wa kufanya biashara ya watumwa na pembe za tembo.
Walimgeukia Sultan Barghash bin Said wa Zanzibar kumtaka apeleke jeshi kummaliza Mirambo. Barghash alikubali kujiingiza kwenye mgogoro wa Waarabu wa Unyanyembe na Mirambo siyo tu kwa sababu ya kuwasaidia lakini kwa sababu biashara ya pembe za tembo, ilianza kuyumba.
Soko la Zanzibar lilikuwa halipati pembe nyingi kama siku za nyuma. 
Agosti 1873, jeshi la Bargash likiongozwa na Amir bin Sultan liliwasili Unyanyembe tayari kuungana na wenyeji wao kumkabili Mirambo.
Kwa mshangao Waarabu wa Unyanyembe hawakupenda uteuzi wa Amir bin Sultan ambaye alishawahi kukaa Unyanyembe kabla ya kurejea Zanzibar na kusita kushirikiana naye.
Jeshi hilo ambalo liliundwa na Mabulushi kutoka Zanzibar na Waswahili kutoka Pwani  baadaye  liligawanyika.
Waswahili kutoka Pwani wakaendelea kumtii Amir bin Sultan na Mabulushi wakahamishia utii wao kwa Waarabu wawili wa Unyanyembe wenye ushawishi mkubwa Shaykh bin Nasibu na Abdulla bin Nasibu.
Ndugu hao wawili walihofu kunyang’anywa madaraka na ushawishi waliokuwa nao katika Unyanyembe na Amir bin Sultan.
Katika Mazingira ya mgawanyiko huo miongoni mwa Waarabu, uwezekano wa kumshambulia Mirambo ukawa haupo.
Mirambo alijua uwepo wa jeshi la Sultan Barghash hapo Unyanyembe lakini hakushambulia aliwasubiri wathubutu.
Sultan Barghash alimtuma Abdulla Mohammed kwenda Unyanyembe kuchunguza kwa nini Mirambo hajashambuliwa. Mjumbe alitoa taarifa kwa Barghash kwamba hakukuwa na umoja miongoni mwa Waarabu kiasi kwamba kumshambulia Mirambo isingewezekana.
Barghash kwa hasira akayaondoa majeshi yake kuyarudisha Zanzibar. Waarabu wa Unyanyembe walilalamika lakini Barghash akawajibu kuwa kama wanataka kuendeleza mgogoro na Mirambo wanaweza kufanya hivyo kwa wakati wao.
Baadaye Barghasha alimwambia James Elton, mwakilishi wa Uingereza Zanzibar kuwa hana uwezo wa kufanya zaidi ya alivyofanya na mtazamo wake ni kuwaacha wakoloni wa Kiarabu waendeshe mapigano wao wenyewe.
Kisha akaongeza kuwa “hana mamlaka katika nchi hiyo (Unyamwezi)". Said bin Salim ambaye Wanyamwezi walimpa jina la Kissesa na ambaye Mirambo alikuwa hampendi kabisa alipeleka ombi kwa Kabaka Mutesa I  wa Buganda kumtaka alete jeshi kumwondoa Mirambo.
Mutesa I alikubali na kuandaa jeshi la watu 9,000 kwenda Urambo.
Mirambo mwenyewe alimueleza mmisionari, Dk. Ebenezar Southon aliyekuwa Urambo kuwa jeshi la Kabaka Mutesa I lilisitisha msafara na Kurudi Buganda baada ya kukosa maji ya kunywa kwa watu 9,000.
Kushidwa kwa kampeni ya Mutesa I dhidi ya Mirambo kuliwaacha Waarabu wa Unyanyembe na  njia moja  tu ya kutafuta suluhu na Mirambo.
Mwaka 1875 Said bin Salim alipeleka ujumbe kwa Mirambo akitaka suluhu. Kilichozungumzwa na kukubalika hakikujulikana lakini matokeo yake ni kwa Mirambo kuruhusu misafara ya Waarabu kupita katika himaya yake kwa kulipa ushuru.
Kampeni za kivita za Mirambo katika sehemu kubwa ya Unyamwezi na kampeni za Nyungu ya Mawe katika eneo la Kusini na Kusini Mashariki ya Unyanyembe na harakati za Mtinginya Kasikazini Mashariki ya Unyanyembe zilifanya biashara ya pembe za ndovu katika soko la Zanzibar kudorora na Mkasiwa wa Waarabu wake hapo Unyanyembe kubaki kama wafungwa.
Mkasiwa hukuweza kutoka Unyanyembe kwa hofu ya wababe hao watatu. Kwa kulinda soko la Zanzibar na kwa kutotaka mapambano ya kijeshi, Sultan Barghash aliamua kumwekea vikwazo vya biashara Mirambo hasa vifaa vya kijeshi kama bunduki, baruti, risasi na fataki.
Vikwazo hivyo vilimwathiri sana Mirambo ingawa alivipata kwa njia ya uvamizi na kwa kununua kupitia watu wengine.
Mirambo alianza kushindwa katika baadhi ya mapambano aliyoyafanya mwishoni mwa miaka ya 1870 na mwanzoni mwa miaka ya 1880.
Kwa mfano uvamizi aliofanya Mirambo katika utawala wa Turu na Iramba ulishindwa na akalazimika kurudi nyuma.
Mwaka 1877 Barghash alieneza vikwazo vya silaha kwa machifu wengine zaidi ya Mirambo katika eneo hili la Afrika Mashariki.
Mirambo ameelezwa kuwa alikuwa mjanja, mwerevu na mwepesi wa kuchukua hatua wakati mwingine alikuwa mgumu kumuelewa.
Wangoni walipofika katika nchi ya Unyamwezi kuna wakati aliwatumia katika nchi ya rugaruga na wakati mwingine alitofautiana nao na kupigana.
Inasemekana kuwepo kwao katika jeshi lake kulimsaidia sana Mirambo. Nyungu ya Mawe ambaye alikuwa mtawala aliyemtegemea kwanza Mirambo, aliafiki harakati zake lakini baadaye alitamani Nyungu ya Mawe apunguzwe nguvu zake.
Ingawa baada ya mapatano na Waarabu mwaka 1875 Mirambo alianza kuzungumza amani na kwamba vita sasa basi, lakini aliendelea kushambulia maeneo ya Ukongo hadi Ubende.
Mirambo hakuvumilia uasi na utovu wa nidhamu. Hali hiyo ilipojitokeza ilizimwa kwa ukatili mkubwa. Viongozi wa tawala moja walipokataa kutii amri ya kuwataka wachangie gharama za jeshi yake, aliamuru wakamatwe na kuuawa.
Kijana mmoja aliyeibia msafara ambao Mirambo alikuwa ametoa kibali, alikamatwa na alipofikishwa kwa Mirambo, Mirambo mwenyewe alimuua kijana huyo.
Mirambo alikufa mwaka 1884 akiwa na umri unakadiriwa kuwa miaka 44. Mwaka huo huo alikufa Nyungu ya Mawe na Kabaka Mutesa I.
Maelezo ya kifo cha Mirambo yana utata. Wazungu waliokuwepo katika eneo la Unyamwezi wakati wa kifo chake walisema alikufa kwa ugonjwa wa koo. Waliamini huenda ilikuwa ni saratani ya koo.
Masimulizi ya wenyeji waliokuwa karibu na Mirambo yanaonyesha kwamba kulikuwa na matukio mengine yanayoelezea upande wa pili wa kifo chake.



MIRAMBO kwa ushujaa wake na utaalamu wa mbinu za kivita aliamuru majeshi yake yasipigane kwa nguvu badala yake wawe wanarudi nyuma kama vile wamezidiwa.

Kwa mbinu hiyo aliweza kuwavuta wavamizi hadi karibu na eneo la Ulyankulu kwa upande wa kaskazini, baada ya kuona majeshi yote ya wavamizi yameingia katika himaya yake Mirambo aliamuru majeshi yake yaanze kushambulia. Baada ya mapambano makali ya ana kwa ana, jeshi la uvamizi lilivunjika na kusambaratika na kuanza kukimbia ovyo kurudi Unyanyembe bila ya mpangilio.
Mirambo aliwafuata na askari wengi wa wavamizi waliuawa. Alipofika Unyanyembe Mirambo aliharibu sehemu kubwa ya boma la Itetemia lakini hakuzingira sehemu alikojichimbia Mkasiwa wala sehemu  alikokuwepo Stanley.
Aidha, Mirambo hakuharibu ngome za Waarabu. Lakini ghafla Mirambo alisitisha mashambulizi ya Itetemia na kuamuru wanajeshi wake kurudi nyuma ingawa hakukuwa na upinzani mkali.
Hakuna maelezo yoyote kutoka kwa Mirambo kwa nini alisitisha mashambulizi ya Itetemia. Kuna mawazo tu kwamba huenda Mirambo hakutaka kusababisha madhara yoyote kwa Stanley aliyekuwepo kwenye boma hilo na pia hakutaka kuingia kwenye mgogoro wa moja kwa moja na Sultan wa Zanzibar kwa kuwaangamiza Waarabu wa Unyanyembe wakati huo.
Kwa nini Mirambo hakumuua Stanley?
Wakati majeshi ya Mirambo yanarudi nyuma mwarabu moja Khamisi bin Abdulla aliamurisha wafuasi wake kushambulia kwa kudhani majeshi ya Mirambo yalikuwa  yameshindwa.
Alijidanganya. Mara moja majeshi ya Mirambo yalizingira ngome ya Mwarabu huyo na kuua wafuasi wake wote  pamoja na yeye mwenyewe na kuharibu kabisa ngome yake. Kitendo cha kutomgusa Stanley ambaye alikuwa amekimbiwa na watu wake na kuwaacha Waarabu salama kinaonyesha jinsi Mirambo alivyokuwa mwerevu. Hakutaka kuharibu uhusiano wake na jamii ya kimataifa.
Stanley alichukizwa sana na udhaifu walionyesha Waarabu katika kampeni dhidi ya Mirambo ambaye alimwita ‘’Jambazi” na pia ‘’Bonaparte wa Africa,” akimlinganisha na mfalme Napoleon Bonaparte wa Ufaransa. Stanley alichukizwa na kitendo cha Waarabu kumwingiza kwenye mapambano na Mirambo wakati wanajua hawana uwezo.
Stanley aliondoka Unyanyembe kuelekea kusini ili kumkwepa Mirambo. Alipita Ukonongo kisha akaelekea magharibi na baadaye kaskazini hadi Ujiji alikomkuta Dk. David Livingstone mwaka 1871.
Ushindi wa Mirambo dhidi ya Waarabu wa Unyanyembe na washirika wao ulimfanya aonekane kama kiongozi asiye na mpinzani katika ukanda huu wa Afrika Mashariki. Yeye mwenyewe alijiita ”Sultan Mkuu wa Afrika”. Uhasama kati ya Mirambo na Waarabu wa Unyanyembe uliendelea kwa kipindi chote cha uhai wa Mirambo.
Ulevi wamkosesha ushindi Mirambo
Jaribio jingine la Mirambo la kuangamiza Unyanyembe na kuvunja kabisa nguvu za Waarabu lilishindwa. Septemba 1871 Mirambo alishambulia Unyanyembe kwa lengo la kuwasambaratisha Waarabu. Katika mapigano yaliyofanyika kijiji cha Mfuto jirani kabisa na Unyanyembe, Mirambo alishindwa vibaya. Baadaye iligundulika kuwa siku ile Mirambo aliongoza mapigano akiwa amelewa.
Inawezekana tukio hili ndilo lililomfanya Mirambo kuacha pombe kwani baadaye alimweleza mmisionari mmoja kuwa asingeweza kuendesha shughuli zote na kutawala watu wake vizuri kama angekuwa anakunywa pombe.
Kutokana na ushindi huo Waarabu wa Unyanyembe waliamua sasa kumwangamiza Mirambo. Waliandaa jeshi kubwa lililojumuisha Waarabu wa Unyanyembe, Mtemi Mulimanombe wa Ugunda, Mtemi Simba Kaung’ando wa Usawila, askari 300 walioletwa na Mwarabu wa Ujiji Said Bin Majid na msaada kutoka kwa Waarabu wa Usangu.
Said bin Majid alitaka kutumia mwanya huo kulipiza kisasi kutokana na Mirambo kumuua mtoto wake Soud bin Majid na Mwarabu mashuhuri wa Unyanyembe Khamis bin Abdulla. Khamis bid Abdulla ndiye aliyemuua Mnywa Sele (Msabila) ambaye Mirambo alimuona ndiye mtemi halali wa Unyanyembe na si Mkasiwa.
Kuongezea nguvu mtemi Mkasiwa alipeleka warugaruga kwenye jeshi la Waarabu na yeye mwenyewe alikuwepo kwenye mapambano yaliyoongozwa na Said bin Salim, liwali wa Unyanyembe kama mwakilishi wa Sultan wa Zanzabir.
Dk. David Livingstone akiwa Ujiji alipata habari kuwa jeshi la Waarabu lilikuwa na watu 2000. Katikati ya Mwaka 1872 Waarabu walishambulia. Mirambo alijua ukubwa wa jeshi la maadui lakini hakutishika sana. Walipokuwa wanasogelea Urambo, Mirambo alifanya shambulio kubwa na kuwashinda Waarabu na mara kikosi chote cha wavamizi kilisambaratika na kiongozi wao Said bin Salim akakimbia kurudi Unyanyembe. Wapiganaji baada ya kuachwa na kiongozi wao, kila moja alirudi kwao kwa njia aliyojua mwenyewe. Kushindwa kwa Waarabu katika kampeni hii ambayo ilionekana kuandaliwa vizuri, Mirambo alibaki bila tishio lolote katika udhibiti wake wa sehemu kubwa ya Unyamwezi.
Mirambo apata washirika zaidi
Baadaye Mirambo alipata washirika wakusaidiana nae .Wa kwanza ni Nyungu ya Mawe ambaye awali alikuwa anazunguka na jeshi lake katika misitu ya Ukimbu bila ya kuwa na makao maalumu. Kisha alishambulia tawala ya Ukimbu ya Kiwele na kuishinda na kujifanya mtemi wa Kiwele na kaburi lake liko huko hadi leo. Mwingine ni mtemi Mtinginya wa Usongo.
Mtinginya na Nyungu ya Mawe waliwahi kupigana lakini baadaye walipatana na kwa pamoja wakawa washirika wa Mirambo bila ya kuwa chini ya uongozi wa Mirambo dhidi ya Unyanyembe na Waarabu wake.
Mshirika wa tatu ni Simba Kaung’ando wa Usawila. Huyu pamoja na Mtemi wa Ugunda walimsaidia Mkasiwa na Waarabu wake kumshambulia Mirambo, lakini alibadilika na kufanya urafiki na Mirambo.
Kwa kushirikiana na Watemi hao watatu, Mtinginya, Nyungu ya Mawe na Simba Kaung’ando, Mirambo alidhibiti njia zote za kwenda ziwa Tanganyika na Kongo, na njia ya kaskazini kwenda Uganda.
Misafara yote iliyopita katika kipindi cha 1871 na 1879 ilifanya hivyo kwa idhini yake na aliwatoza kodi. Kulikuwa na njia tatu, moja ilitoka Pwani kupitia Ugogo na Unyamwezi kaskazini kwenda Uganda. Njia ya pili na maarufu ilipita Ugogo na Unyanyembe kwenda Ujiji na Kongo, na njia ya tatu ilipita Usagara, Usangu, Ukimbu hadi Karema katika Ziwa Tanganyika.
Mirambo na washirika wake Mtinginya na Nyungu ya Mawe walidhibiti njia ya kati ya kupita Ugogo na Unyanyembe na kaskazini kwenda Uganda. Kwa upande wa Kusini kwa kushirikiana na Nyungu ya Mawe na Simba Kaung’ando walidhibiti njia ya kupitia Ukimbu kwenda ziwa Tanganyika.

Wamisionari wawili Tom Cadenhead na Frederick Carter walipojaribu kumkwepa Mirambo kwa kupita njia ya kusini alipeleka jeshi lake kusini. Kwanza alishambulia Ugunda iliyokuwa imesaidia Waarabu wa Unyanyembe na kisha akaingia Usawila bila ya mapigano kwa kuwa Simba Kaung’ando alifanya mapatano na Mirambo.
Baadaye majeshi ya Mirambo yakisaidiwa na majeshi ya Simba Kaung’ando yalimshambulia Mtemi Kasogela wa Upimbwe aliyekuwa amewapokea wamisionari hao wawili Cadenhead na Carter.
Upimbwe iliangamizwa na wamisionari hao wawili wakauawa. Katika kampeni hiyo Mirambo alikuwa pamoja na majeshi yake. Kwa tukio hilo njia ya kupitia Usangu na Ukimbu ikafungwa. Kwa udhibiti huo Waarabu wa Unyanyembe hawakuwa na hiari isipokuwa kupata kibali cha Mirambo na kulipa kodi au ushuru wapate kufanya biashara katika eneo la Unyamwezi na hata kupitisha misafara kwenda Kongo.
Sultan wa Z’bar dhidi ya Mirambo
Waarabu wa Unyanyembe hawakukata tamaa katika harakati zao za kumwondoa Mirambo wapate uhuru wa kufanya biashara ya watumwa na pembe za tembo. Walimgeukia Sultan Barghash bin Said wa Zanzibar kumtaka apeleke jeshi kummaliza Mirambo. Barghash alikubali kujiingiza kwenye mgogoro wa Waarabu wa Unyanyembe na Mirambo siyo tu kwa sababu ya kuwasaidia lakini kwa sababu biashara ya pembe za tembo katika soko la Zanzibar ilianza kuyumba.
Soko la Zanzibar lilikuwa halipati pembe nyingi katika siku za nyuma. Agosti 1873 Jeshi la Bargash likiongozwa na Amir bin Sultan liliwasili Unyanyembe tayari kuungana na wenyeji wao kumkabili Mirambo. Kwa mshangao Waarabu wa Unyanyembe hawakupenda uteuzi wa Amir bin Sultan ambaye alishawahi kukaa Unyanyembe kabla ya kurejea Zanzibar na kusita kushirikiana nae.
Jeshi hilo ambalo liliundwa na Mabulushi kutoka Zanzibar na Waswahili kutoka Pwani,  baadaye  liligawanyika. Waswahili kutoka Pwani wakaendelea kumtii Amir bin Sultan na Mabulushi wakahamishia utii wao kwa Waarabu wawili wa Unyanyembe wenye ushawishi mkubwa Shaykh bin Nasibu na Abdulla bin Nasibu. Ndugu hao wawili walihofu kunyang’anywa madaraka na ushawishi waliokuwa nao katika Unyanyembe na Amir bin Sultan.
Katika mazingira ya mgawanyiko huo miongoni mwa Waarabu uwezekano wa kumshambulia Mirambo ukawa haupo. Mirambo alijua uwepo wa Jeshi la Sultan Barghash hapo Unyanyembe lakini hakushambulia aliwasubiri wathubutu. Sultan Barghash alimtuma Abdulla Mohammed kwenda Unyanyembe kuchunguza kwa nini Mirambo hajashambuliwa. Mjumbe alitoa taarifa kwa Barghash kwamba hakukuwa na umoja miongoni mwa Waarabu kiasi kwamba kumshambulia Mirambo isingewezekana.
Sultan arudisha majeshi Z’bar
Barghash kwa hasira akayaondoa majeshi yake kuyarudisha Zanzibar. Waarabu wa Unyanyembe walilalamika lakini Barghash akawajibu kuwa kama wanataka kuendeleza mgogoro na Mirambo wanaweza kufanya hivyo kwa wakati wao.
Baadaye Barghash alimwambia James Elton mwakilishi wa Uingereza Zanzibar kuwa hana uwezo wa kufanya zaidi ya alivyofanya na mtazamo wake ni kuwaacha wakoloni wa kiarabu waendeshe mapigano wao wenyewe. Kisha akaongeza kuwa “hana mamlaka katika nchi hiyo (Unyamwezi)".
Said bin Salim ambaye Wanyamwezi walimpa jina la Kissesa na ambaye Mirambo alikuwa hampendi kabisa alipeleka ombi kwa Kabaka Mutesa 1 wa Buganda kumtaka alete jeshi kumwondoa Mirambo. Mutesa 1 alikubali na kuandaa jeshi la watu 9000 kwenda Urambo.
Askari 9000 wakosa maji ya kunywa
Mirambo mwenyewe alimueleza mmisionari Dk. Ebenezar Southon aliyekuwa Urambo kuwa jeshi la Kabaka Mutesa 1 lilisitisha msafara na kurudi Buganda baada ya kukosa maji ya kunywa kwa watu 9000. Kushidwa kwa kampeni ya Mutesa 1 dhidi ya Mirambo kuliwaacha Waarabu wa Unyanyembe na  njia moja  tu, nayo ni kutafuta suluhu na Mirambo.
Mwaka 1875 Said bin Salim alipeleka ujumbe kwa Mirambo akitaka suluhu. Kilichozungumzwa na kukubalika hakikujulikana lakini matokeo yake ni kwa Mirambo kuruhusu misafara ya Waarabu kupita katika himaya yake kwa kulipa ushuru.
Kampeni za kivita za Mirambo katika sehemu kubwa ya Unyamwezi na kampeni za Nyungu ya Mawe katika eneo la Kusini na kusini mashariki ya Unyanyembe na harakati za Mtinginya Kaskazini Mashariki ya Unyanyembe zilifanya biashara ya pembe za ndovu katika soko la Zanzibar kudorora na Mkasiwa na Waarabu wake hapo Unyanyembe kubaki kama wafungwa.
Mkasiwa hakuweza kutoka Unyanyembe kwa hofu ya wababe hao watatu. Kwa kulinda soko la Zanzibar na kwa kutotaka mapambano ya kijeshi, Sultan Barghash aliamua kumwekea vikwazo vya biashara Mirambo hasa vifaa vya kijeshi kama bunduki, baruti, risasi na fataki.
Vikwazo vilimuathiri sana Mirambo ingawa alipata mahitaji yake kwa njia ya uvamizi na kwa kununua kupitia watu wengine. Mirambo alianza kushindwa katika baadhi ya mapambano aliyoyafanya mwishoni mwa miaka ya 1870 na mwanzoni mwa miaka ya 1880. Kwa mfano uvamizi aliofanya Mirambo katika tawala za Turu na Iramba ulishindwa na akalazimika kurudi nyuma. Mwaka 1877 Barghash alieneza vikwazo vya silaha kwa machifu wengine zaidi ya Mirambo katika eneo hili la Afrika Mashariki.
Mirambo ameelezwa kuwa alikuwa mjanja mwerevu na mwepesi wa kuchukua hatua. Wakati mwingine ilikuwa vigumu kumuelewa. Wangoni walipofika katika nchi ya Unyamwezi kuna wakati aliwatumia katika jeshi lake la rugaruga, na wakati mwingine alitofautiana nao na kupigana.
Inasemekana kuwepo kwao katika jeshi lake kulimsaidia sana Mirambo. Nyungu ya Mawe ambaye alikuwa mtawala anaejitegemea, kwanza Mirambo aliafiki harakati zake lakini baadaye alitamani Nyungu ya Mawe apunguzwe nguvu zake. Ingawa baada ya mapatano na Waarabu mwaka 1875 Mirambo alianza kuzungumzia amani na kwamba vita sasa basi, lakini aliendelea kushambulia maeneo ya Ukonongo hadi Ubende.
Mirambo hakuvumilia uasi na utovu wa nidhamu. Hali hiyo ilipojitokeza ilizimwa kwa ukatili mkubwa. Viongozi watawala moja waliokataa kutii amri ya kuwataka wachangie gharama za jeshi lake, aliamuru wakamatwe na kuuawa. Kijana moja aliyeibia msafara ambao Mirambo alikuwa ametoa kibali, alikamatwa na alipofikishwa kwa Mirambo, Mirambo mwenyewe alimuua kijana huyo.
Mirambo alikufa mwaka 1884 akiwa na umri unaokadiriwa kuwa miaka 44. Mwaka huo huo alikufa Nyungu ya Mawe wa Ukimbu na Kabaka Mutesa 1 wa Buganda.
Utata kifo cha Mirambo
Maelezo ya kifo cha Mirambo yana utata. Wazungu waliokuwepo katika eneo la Unyamwezi wakati wa kifo chake walisema alikufa kwa ugonjwa wa koo. Waliamini huenda ilikuwa ni saratani ya koo. Masimulizi ya wenyeji waliokuwa karibu na Mirambo yanaonyesha kwamba kulikuwa na matukio mengine yanayoelezea upande wa pili wa kifo chake.
Kuanzia mwaka 1883 Mirambo aliendesha mapambano makubwa dhidi ya Urundi (Burundi) lakini akashindwa. Baadaye Mirambo alipigana na washirika wake wa zamani, Wangoni akawaadhibu vibaya. Wangoni walikuwa wameomba msaada kwa Mtemi Isike aliyekuwa mtawala wa Unyanyembe baada ya kufa Mkasiwa. Ingawa Isike alikuwa adui wa Mirambo katika mapigano ya Wangoni na Mirambo, Isike hakusaidia upande wowote.
Baada ya mafanikio katika mapigano yake na Wangoni, Mirambo alimgeukia Kapela Malunde, maarufu Kapela, Mtemi wa Ukune. Kapela alikuwa mjomba wa Mirambo. Kapela alimsihi Mirambo asimshambulie, lakini hakukubali ombi hilo. Baadaye Kapela alilalamika kwa Nyakasi, mama yake Mirambo kwamba Mirambo alikuwa anaanzisha vita dhidi yake.
Lakini Mirambo alipuuza ombi la mama yake la kumtaka asifanye vita dhidi ya mjomba wake Kapela. Mirambo alipeleka jeshi lake Ukune. Kapela aliomba msaada kutoka kwa Isike wa Unyanyembe na kwa Wangoni. Isike na Wangoni walipeleka msaada kwa Kapela hali iliyobadili mapigano na Mirambo akalazimika kurudi nyuma.
Mirambo hakuamini tawala ndogo kama Ukune imzuie. Akajipanga upya na kuanza kushambulia Ukune. Safari hii Mirambo alifanikiwa kuzingira ngome ya Kapela lakini ikawa vigumu kwake kulivunja boma na kuingia ndani. Ghafla Mirambo aliamuru majeshi yake kuacha kushambulia na kurudi nyuma.
Masimulizi yanaeleza kwamba mambo ya kimazingaombwe au kiushirikina yalifanyika. Mirambo alichukuliwa kiushirikina kwenda kwa Kapela ambako alilishwa nyama ya Mbwa na aliporudi kwenye kambi yake alianza kuumwa. Simuluzi nyingine zinaeleza kwamba Kapela alimpelekea nyama Mirambo kama ishara ya kutaka mapatano. Kumbe nyama hiyo ilikuwa ya mbwa na Mirambo alipokula alianza kuumwa. Afya ya Mirambo iliendelea kudhoofu hadi kuanza kuelekeza mapigano akiwa kitandani na ilipofika Desemba 2, mwaka 1884 akafariki.
Baada ya kufa himaya aliyokuwa ameijenga katika Unyamwezi ilisambaratika. Masimulizi mengine ya kifo cha Mirambo yanadai kuwa huenda alipewa sumu na majasusi kutoka Unyanyembe. Mbali ya haya yote chanzo cha kifo cha Mirambo kinachojulikana ni ugonjwa wa koo.
Umaarufu wa Mirambo
Mirambo ni miongoni mwa viongozi wachache wa Afrika waliojulikana sana ndani na nje ya Afrika. Mapambano yake na Waarabu wa Unyanyembe yaliyomhusisha na Henry Morton Stanley yalimfanya ajulikane  Amerika na Ulaya. Wazungu wengi na Waarabu walikutana naye na kuandika habari zake. Kwa hiyo kuna mambo mengi yanayoweza kuandikwa kuhusu Mirambo.
Yaliyoandikwa hapa ni muhstari tu wa mambo yanayomhusu Mirambo katika juhudi zake za kutaka Mwafrika ajitawale mwenyewe. Leo hii hapa nchini tumeadhimisha miaka 50 ya Uhuru wa iliyokuwa Tanganyika tunajifunza nini kutoka kwa Mirambo?
Tunachoweza kujifunza kwa Mirambo
Kwanza tunajifunza jinsi Mirambo alivyokuwa hataki kutawaliwa na wageni. Alipambana na mgeni yeyote awe Mzungu, Mwarabu au Mngoni. Alipigana kulinda heshima ya Wanyamwezi dhidi ya kutawaliwa.
Mirambo aligundua mapema kuwa kupambana na kushinda dhidi ya wavamizi kulihitaji umoja na ushirikiano miongoni mwa Wanyamwezi, na alipoona hawawezi kuungana kwa hiari aliwalazimisha kwa nguvu za kijeshi. Hapa tunajifunza kwamba umoja ni nguvu na ujenzi wa taifa unahitaji mbinu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutumia nguvu. Soma historia ya Ujerumani wakati wa Chancellor Otto Von Bismarch na Marekani wakati wa Rais Abraham Lincoln.
Jambo la tatu tunajifunza kutoka kwa Mirambo ni uzalendo wake wa kutaka maliasili na biashara za Unyamwezi zimilikiwe na Wanyamwezi wenyewe. Mirambo hakuwachukia wageni bali alitaka wafanye biashara kwa idhini na kwa kushirikiana na Wanyamwezi wenyewe.
Msingi wa ugomvi wa Mirambo na Waarabu wa Unyanyembe ulikuwa ni nani anadhibiti biashara ya pembe za tembo katika Unyamwezi. Aidha Mirambo alitaka Waarabu watambue kuwa Unyamwezi ina wenyewe. Alitaka Wanyamwezi wafaidi biashara itokanayo na maliasili ya nchi yao.
Suala lingine tunalojifunza ni jinsi Mirambo alivyowachukia viongozi aliowaona kuwa ni wasaliti kwa wananchi wao kama vile Mtemi Mkasaiwa wa Unyanyembe. Mkasiwa alipata utawala na alitawala Unyanyembe kwa msaada wa Waarabu. Tangu wakati wa Mtemi Fundikira 1 Waarabu walikuwa na kauli kubwa katika Unyanyembe.
Mirambo alimchukia Mkasiwa kwa kuwa alimuona kama kibaraka wa Waarabu. Leo tuna viongozi katika Bara la Afrika wanaochaguliwa kwa msaada kutoka nje ya Afrika na hata kuendelea kwao kuwepo madarakani kunatokana na misaada kutoka nje ya Afrika. Hawa lazima watazisaliti nchi zao na Bara la Afrika kwa ujumla.
Suala la tano ni biasharaMirambo alitambua maana na umuhimu wa biashara kwa ustawi wa dola yake. Alipeleka misafara mingi ya kibiashara Pwani kuuza pembe za tembo na kununua bidhaa muhimu kwa ajili yake na watu wake. Hata leo tunaambiwa kuwa taifa haliwezi kuendelea na kustawi bila ya kufanya na kukuza biashara baina yake na mataifa mengine. Mirambo alihakikisha biashara inamilikiwa na Wanyamwezi.
Jambo la sita, tunajifunza kutoka kwa Mirambo kwamba uongozi imara ni wa lazima ili kudumisha umoja wa kitaifa, nidhamu na amani, na kuwa na mwelekeo kitaifa. Hili linajidhihirisha pale Mirambo alipokufa himaya yake yote ilisambaratika. Aliyemrithi Mirambo hakuwa na uwezo na nguvu kama Mirambo na hivyo kusababisha dola kuanguka.
Kwa upande wa pili Mirambo hakujenga taasisi za kiutawala ambazo zingewezesha dola kudumu hata bila ya Mirambo. Dola ya Mirambo ilitawaliwa moja kwa moja kutoka Urambo na uasi ulipotokea ulizimwa na vikosi vinavyoongozwa na Mirambo mwenyewe. Hapa tunajifunza mambo mengine mawili. La kwanza ni kwamba utawala wa nchi lazima uwe na misingi yake kwenye taasisi za dola.
Taasisi ndiyo kuzuizi  kwa mtawala asiye na maadili mema asiendeshe nchi kama anavyotaka. La pili kwa mazingira ya sasa lazima  tuchague viongozi imara wakati wa uchaguzi. Tusichague viongozi kwa kurubuniwa kwa fedha na vishawishi vingine. Kutokuwa waangalifu katika chaguzi ama kutaliangamiza taifa au kutalitumbukiza katika machafuko na vurugu. Lazima kuchagua viongozi bora na imara.
Dola ya Mirambo ilianguka kwa kuwa aliyemfuatia Mirambo alikuwa ni mtawala dhaifu. Mtawala mpya wa Urambo Mpandashalo hakuwa na uwezo wa aina ya Mirambo na alikuwa mlevi. Miezi mitatu tu baada ya kifo cha Mirambo uasi ulianza kutokea sehemu mbalimbali katika dola na Mpandashalo alishindwa kudhibiti na huo ukawa mwisho wa himaya ya Mirambo.
Mirambo kama ilivyo kwa viongozi wengine wa Afrika wa enzi zake, ni miongoni mwa watu waliopigania uhuru, heshima na utu wa Mwafrika. Alifanya mengi mazuri na ya kujivunia. Hakika tunapoadhimisha miaka 50 ya uhuru Mirambo anastahili kukumbukwa na kuenziwa. Je, Urambo na Unyamwezi kwa ujumla wanamkumbukaje Mirambo miaka 127 baada ya kifo chake?

KWA HISANI YA RAIA MWEMA

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!