Monday, 6 July 2015

MICHEZO: CHA JUU KISA CHA WACHEZAJI VIMEO BONGO


Miaka zaidi ya 20 iliyopita mashabiki wa soka wamekuwa wakishuhudia ujio wa nyota mbalimbali wa kigeni wanaomiminika nchini kwa ajili ya kuja kucheza soka la kulipwa katika klabu kadhaa za soka Tanzania.

Kwa miaka hiyo yote tumeshuhudia wachezaji wa kila aina wakiminika Tanzania iwe kwa kuletwa na mawakala wa ndani na nje ya nchi na wengine wakijilitea wenyewe kwa ajili ya kusaka malisho.
Katika ujio huo wapo baadhi ya wachezaji ambao wamekuwa kivutio kwa uwezo wao kisoka dimbani, kiasi cha kuwa tegemeo na hata ikitokea wachezaji hao kuumia au kuhama mapengo yao yalionekana dhahiri.
Wachezaji wa awali kucheza soka la kulipwa nchini ni kama Mayaula Mayoni, aliyekuwa nyota wa muziki aliyeichezea Yanga kisha wakaja wengine kama akina Nonda Shaaban ‘Papii’ na William Fahnbuller.
Pia kuna wakali kama Constantine Kimanda, Sammy Bitumba Iyella, Pascal Ochieng, Ngandou Ramadhani, Moses Odhiambo, Doyi Moke, Mackenzie Ramadhani, Ramadhani Wasso na Boniface Ambani.
Kadhalika wakali kama Edwin Mukenya, Wisdom Ndlovu, Steve Bengo, Jerry Santo, Davies Mwape, Hamis Kiiza, Robert Jama Mba, Kabongo Honore, George Owino, Yaw Berko au Robert Ssentengo.
Kuna akina Orji Obinna, Eme Ezechukwu, George Odhiambo ‘Blackberry’, Joseph Njoroge, Genilson Santos ‘Jaja’ na Kenneth Asamoah waliokimbiza katika soka la Tanzania kwa nyakati tofauti.
Kisha wakaibuka akina Kipre Tchetche, Amissi Tambwe, Emmanuel Okwi, Haruna Niyonzima, Mbuyu Twite, Humphrey Mieno, Brian Umony, Kipre Balou, Pascal Wawa, Simon na Dan Sserunkuma, Joseph Owino na wengine.
Wakali
Miongoni mwa wachezaji hao wa kigeni maarufu kama ‘mapro’ wapo wachache walioweza kuwasisimua mashabiki kwa uwezo wao mkubwa uwanjani katika kusakata kandanda kiasi cha kuwa vipenzi nchini.
Hii ni kwa sababu walikuwa wakizisaidia timu hiyo kiasi kwamba hata ilipokuwa wakikosekana uwanjani mapengo yao yalionekana dhahiri.
Kwa mfano leo hii utawaambia nini mashabiki na wanachama wa Simba kuhusu Okwi au Yanga utawaeleza lipi juu ya Niyonzima au Twite ama Azam kwa Pascal Wawa au Kipre Tchetche na sasa Brian Majwega!
Kadhalika wapo wengine ambao walikuwa waligeuka vituko ama kwa kuwa na viwango duni vya kucheza soka au kwa kushindwa kuzoea mazingira ya soka la Tanzania kama ilivyomkuta Dan Sserunkuma.
Vimeo
Wachezaji kama Jama Mba, Daniel Akuffor, Lino Musombo au Kanu Mbiyavanga waliowahi kusajiliwa Simba na Yanga kwa nyakati tofauti ni baadhi ya wachezaji walioonekana mizigo na vimeo haswa.
Hiyo ilikuwa ni tofauti na namna walivyokuwa wakipambwa na baadhii ya vyombo vya habari kana kwamba klabu hizo zilikuwa zimewsajili nyota wanaotamba Ulaya kama akina Lionel Messi, Cristiano Ronaldo au Neymar Jr.
Kwa kuwa soka ni mchezo wa hadharani, yale yaliyokuwa yakitajwa juu ya wasifu wa wachezaji hao yalidhihirisha tofauti baada ya kushindwa kucheza kwa kiwango kilichotakiwa na kutupiwa virago vyao mapema.
Tatizo
Wakala wa zamani nchini, Said Tully anasema kuwa kutofahamika kwa Ligi ya Tanzania ni tatizo linalokwamisha kuja kwa wachezaji wa kiwango cha juu na wenye malengo kwa kuhofu ya kupoteza muelekeo hapa nchini.
“Changamoto kubwa ni kutojulikana kwa ligi yetu na pia kubwa linalofanya wachezaji wengi vimeo kuja nchini au kujileta wenyewe ni klabu kutokuwa na mawakala au wang’amuzi wa vipaji wa kuwafuatilia wachezaji nje,” anasema Tully.
Tully anasema usajili wa wachezaji wa kigeni unafanywa na kila mtu na hivyo kuletwa hata wasio na sifa ilimradi watu wapige fedha na mwishowe mambo huja kuwa mabaya wakiwa wameisha saini.
Wakala mwingine ambaye hakupenda kuandikwa jina lake gazetini anasema kuwa usajili wa wachezaji wa kigeni ni mradi wa watu ndiyo maana mawakala waliopo Tanzania hawashirikishwi sana.
“Hatuaminiki na viongozi wa klabu, hivyo jukumu hilo hufanywa na viongozi wa klabu kwa vile wanataka mapato ya asilimia kumi ya usajili wa mchezaji wa kigeni, lakini hawajui kazi hivyo hujikuta wakileta wachezaji bomu na kuingia hasara bila kupenda,”anasema wakala huyo.
Suala hilo la kutoaminika kwa mawakala wa ndani, hata Tully ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba anakiri na kudai viongozi wa klabu hawawaamini mawakala wa Tanzania kama wanaweza kazi hiyo.
Kipi kifanyike
Tully anasema wachezaji wengi wanaotoka Ukanda wa Afrika Magharibi kuja kucheza soka nchini ni wa viwango vya kawaida sana na wanalingana na wachezaji wa Tanzania, ila wanakuja kwa ajili ya kusaka maisha.
“Wao ni wajanja na wajitambua hivyo hata kama huwa ni wachezaji wa kawaida, lakini wanajituma na kutimiza wajibu wao uwanjani kusudi kutimiza malengo yao ya kusaka maisha ughaibuni,” anasema Tully.
Hata hivyo kuweza kuhakikisha mapro hasa baada ya TFF kuongeza idadi ya wachezaji hao kutoka watano mpaka saba ni kuwaacha wenye jukumu na kazi ya uwakala kufanya kazi zao bila kuingiliwa au kutiliwa shaka.
“Hii itasaidia kama mambo yakiharibika wakala abebe lawama kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa uaminifu, lakini mtindo huu wa kila mtu kusajili wageni ni mtihani mkubwa kwa klabu,” anasema Tully.
Tully anasema kazi ya uwakala ni taaluma ambayo hufanywa kama kazi nyingine na ndiyo maana Jorge Mendes raia wa Ureno anasifika duniani katika dili za wachezaji na makocha kutokana na kubobea katika fani hiyo.
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!