JESHI la Polisi nchini jana liliwaaga kwa heshima zote za kijeshi askari wake wawili kati ya wanne waliouawa wakiwa katika kituo cha kazi cha Stakishari, Ukonga jijini Dar es Salaam, huku likiahidi kufanya mapinduzi kadhaa ya kiutendaji.
Aidha, limeapa kuwanasa wahusika wa tukio hilo lililosababisha vifo vya watu saba, wakiwemo raia watatu, kwa kusema kamwe damu zao hazitamwagika bure.
Hayo yalisemwa jana na Kamishna wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova wakati wa kuaga miili ya Koplo Peter Sabuni (51) na Sajenti Adam Nyamuhanga (50) katika viwanja vya polisi, barabara ya Kilwa, Dar es Salaam.
Alisema jeshi la Polisi litafanya mabadiliko ya utendaji kazi wao kuto kana na kubaini kuna watu wanaotumia vibaya dhana ya polisi shirikishi.
Akizungumzia tukio hilo, alisema kuna siri iliyojificha na kwamba lina kila dalili za ugaidi kutokana na majambazi waliohusika kuua askari na raia katika kituo hicho idadi yao kuwa 16, tofauti na wanane walioripotiwa awali, tena wote wakiwa na silaha.
“Kwa kawaida majambazi hutafuta mali na fedha, lakini hawa walivamia kituo kwa lengo la kuchukua silaha na kuua… “Polisi waliokuwepo kituoni ni majasiri na wenye nguvu ndiyo maana majambazi hao walijiimarisha kwa nguvu ambazo siyo za ziada na kuwashinda…lazima kuna kitu hapa,“ alisema na kuapa kuwatia mbaroni wahusika ndani ya mwezi mmoja.
Aliongeza kuwa, kikosi maalumu kimeundwa kwa ajili ya tukio la Stakishari na kwamba tayari kimeshaanza kazi. Alisema tukio hilo limeumiza hisia za wengi, na hasa jeshi la polisi ambalo linalazimika kufikia mara mbili kama kuna haja ya kuendelea au kuacha kutumia utendaji kazi wa polisi shirikishi.
Kova, akizungumza kwa hisia kali, alikatishwa baada ya umati wa askari na raia waliojumuika kuaga askari hao kujibu “Hakuna Haja”. Akaendelea kusema: “Sasa lazima tubadilike na siyo kwamba tutawahudumia vibaya wananchi, lakini lazima polisi tuwe na msimamo, kwani Polisi ni Polisi, hatuwezi kukubali kuacha familia zetu zikiteseka.“
Aliongeza kuwa, jambazi aliyeuawa katika tukio hilo anafahamika na ndiye anayehusishwa kusuka mpango mzima wa uvamizi na kuwapeleka majambazi wenzake kituoni hapo.
Mbinu mpya Akizungumzia kuongezeka kwa matukio ya uhalifu nchini, alisema kama nchi imefikia kiwango cha sasa cha uhalifu, kuna ulazima wa jeshi la Polisi kubadilika na kwenda sambamba kukabiliana na uhalifu mpya wa aina tofauti.
“Hatutalala, tutakula nao sahani moja na jeshi la litapambana na majambazi hao kwa uwezo wote, kwani damu ya askari hao haitamwagika bure. “Ole wao…tutajibu kwa vitendo.
Tunaomba wananchi watuamini kwani tutaonesha ujasiri kwa kuwakamata wote baada ya kuunda kikosi kazi chenye mafunzo ya ndani na nje ya nchi kwa ajili ya matukio hayo na mwelekeo umeanza kuonekana,” alisema.
Dau la mil. 50/- Pamoja na juhudi za Polisi kusaka wahusika, Kova ameongeza kuwa, dau la Sh milioni 50 lililotangazwa kutolewa kwa watakaosaidia kukamatwa kwa wauaji wa shambulio la Stakishari, taarifa zimekuwa zikimiminika, hivyo kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa tukio hilo alilosisitiza mwelekeo wake ni mzuri na kuna kila dalili za kufanikisha kukamatwa kwa wahusika wote.
Awali, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Lucas Mkondya aliahidi kuwa polisi katika kanda hiyo watafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha walioshiriki uhalifu wanatiwa mbaroni na kusisitiza hakuna atakayebaki salama.
Mwili wa Sabuni aliyekuwa na Shahada ya Sheria aliyoipata Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), ulisafirishwa jana kwenda mkoani Mara kwa maziko. Ameacha mjane na watoto wanne. Mwili wa askari mwingine, Adam Nyamuhanga ambaye pia ameacha mjane na watoto watatu, nao umesafirishwa kwenda Mwanza.
Miili ya askari wengine wawili waliokufa katika tukio la Stakishari ilisafirishwa mapema kwenda Bukoba mkoa Kagera na mwingine Moshi mkoani Kilimanjaro.
Gautin Kakoko mwili wake umesafirishwa kwenda Bukoba ili ndugu waweze kuwahi pia maziko ya mama mzazi wa askari huyo aliyekufa kutokana na mshituko wa kifo cha mtoto wake. Aidha, mwili wa Anthony Komu ukisafirishwa kwenda Moshi kutokana na ombi la wanafamilia.
Katika tukio la uvamizi wa kituo cha Stakishari lililotokea usiku wa kuamkia Jumatatu, majambazi waliua watu saba wakiwemo askari wanne na baada ya kufanikisha mauaji, walivunja ghala na kuiba silaha ambazo idadi yake haijajulikana.
No comments:
Post a Comment