Kwenye mipango ya afya, moja ya kanuni ni kuhakikisha kila mtoto anayezaliwa anakuwa na hali bora kiafya, ikijumuisha akili na mwili.
Mazingira hayo yamekuwa yakiwafanya wanasayansi kuendesha tafiti mbalimbali ili kukabili tatizo la watoto kuzaliwa wakiwa na ama na ukosefu wa viungo au athari za kiakili.
Moja ya tafiti zilizofanyika zilionyesha kuwa ili mtoto azaliwe akiwa na afya njema inapaswa azaliwe na wazazi ambao angalau umri wao uwe wa kiwango fulani.
Mratibu wa Afya ya Akili mkoa wa Dodoma, Dk Alphoncina Mahano anasema kitaalamu ili mwanamke ajifungue mtoto aliye katika hali njema, anapaswa abebeb mimba wakati akiwa na umri zaidi ya miaka 18 na asizidi miaka 38.
Anasema tafiti zinaonyesha anayebeba mimba katika umri chini ya miaka 18 na zaidi ya miaka 38, ana uwezekano wa kujifungua mtoto mwenye ulemavu wa akili au kama inavyojulikana; mtindio wa ubongo.
Ulemavu, ugonjwa wa akili
Mahano anaeleza kuwa afya ya akili ni ile hali ya mtu kuwa mzima kimwili, kiakili, kihisia, kiroho na uhusiano na watu wengine.
“Hii inaimanisha kuwa mojawapo kati ya mambo yaliyotajwa kukiwa na hitilafu, mtu hawezi kuwa yupo vizuri kiakili.”
Mahano anasema kuna tofauti kati ya mgonjwa wa akili na mlemavu wa akili. Anafafanua kuwa ugonjwa wa akili ni hali au ugonjwa ambao unaweza kumpata mtu yeyote na kumsababishia mabadiliko ya tabia katika kufikiri, hisia na matendo kwa umri wowote ilhali ulemavu hutokea kwa kuzaliwa nao au kuupata baada ya kuzaliwa.
“Ulemavu wa akili hutokea kwa watoto kuzaliwa nao au anaweza kupata baada ya kuzaliwa na dalili zake ni kuchelewa katika ukuaji kiakili, yaani kila hatua ya maendeleo ya ukuaji, uwezo wa mtoto huyu unakuwa ni mdogo ukilinganishwa na watoto wenye umri kama wake,” anaeleza Dk Mahano.
Mtaalamu huyu aliyebobea katika afya ya akili anaongeza kuwa ulemavu mwingine wa akili ni mtindio wa ubongo (Paralysis) na mtoto anaweza kupata hali ya kupooza upande mmoja wa mkono na mguu.
Mahano, ambaye ni mratibu wa afya ya akili mkoa wa Dodoma anasema kuwa ulemavu mwingine ni ule wa kuzaliwa na kichwa kidogo (Mongolisim).
Chanzo cha ulemavu wa akili
Dk Mahano anaeleza kuwa kinamama wajawazito walio chini ya umri wa miaka 18 na wale wenye umri zaidi ya miaka 38 wana uwezekano wa kujifungua kwa shida na matokeo yake mtoto anaweza kupata athari kwenye ubongo ( Brain asphyxsia) na kuathiri maendeleo ya ukuaji wa akili. Hii husababisha mtoto husika kupatwa na ulemavu wa akili.
“Unywaji wa pombe na uvutaji sigara wakati wa ujauzito unaweza kuathiri ubongo wa mtoto tumboni. Magojwa kama vile kaswende malaria pamoja na lishe duni kwa mama mjamzito, pia husababisha au kuchangia kwa kiasi kikubwa kujifungua mtoto mwenye ulemavu wa akili,” anaeleza Dk Mahano.
Mtaalamu huyu anafafanua kuwa ukosefu wa lishe stahiki kwa mama mjamzito huweza kuathiri ukuaji wa mtoto tumboni au mama kukosa nguvu wakati wa kujifungua.
Kwa sababu hiyo, mtoto kuchelewa kutoka wakati wa kuzaliwa na kupata athari kwenye ubongo jambo ambalo husababisha kuwa na ulemavu wa akili.
Mahano anazitaja sababu nyingine zinazoweza kuchangia ulemavu wa akili kuwa ni mama mjamzito kutumia dawa bila ushauri wa daktari.
Anasema matumizi holela ya dawa ni hatari kwa mtoto ambaye hajazaliwa kwani huweza kuathiri ubongo wake tangu akiwa tumboni (drug intoxication) hivyo kusababisha azaliwe akiwa na ulemavu wa akili.
Anaeleza pia kuwa kitendo cha mama kuzalia nyumbani bila mtaalamu/mkunga ni hatari kwa mama na mtoto pia kwani kwa namna moja ama nyingine kunaweza kuchangia mtoto aliyezaliwa kupata ulemavu wa akili.
Mahano anasema mtoto anaweza kuzaliwa na ulemavu wa akili kutokana na mama kujifungua kwa shida na hivyo kusababisha jeraha la ubongo hasa kwa wale wanaobeba mimba chini ya umri wa miaka 18 au zaidi ya umri wa miaka 38 kutokana na kupata uzazi pingamizi.
“Homa kali zinazoambatana na degedege mara kwa mara bila tiba sahihi na hali ya kurithi pia huchangia mtoto kuzaliwa akiwa na ulemavu wa akili,” anasema.
Mahano anaeleza kuwa kuna watoto huweza kuzaliwa salama lakini wakiwa na umri kati ya miaka sifuri hadi mitano huweza kupatwa na ulemavu wa akili
“Kama nilivyosema, asilimia kubwa ulemavu wa akili unazuilika kwa kuzingatia maelekezo ya wataalamu. Kama mtoto akizaliwa vizuri akiwa amekingwa vizuri toka tumboni, na akapelekwa kliniki na kupata chanjo zote, akipata homa anawahishwa hospitali kwa matibabu na ushauri wa daktari, hawezi kupata ulemavu wa akil,” anasema Dk Mahano, akifafanua:
“Lakini mtoto anaweza kupata taahira ya akili kutokana na wazazi au walezi kutozingatia umuhimu wa kuwahi matibabu hospitali na badala yake wanamchelewesha kwa waganga wa kienyeji hususani kwa mtoto mwenye homa kali inayoambatana na degedege na ikijirudi mara kwa mara chembechembe za ubongo huharibika na kusababisha mtoto kupata taahira ya akili.”
Tofauti na ugonjwa wa akili ambao huweza kutibika, ulemavu wa akili hautibiki kwa maana hiyo Dk Mahano anasema ni vema jamii kujiepusha na mambo yanaweza kusababisha hali hiyo.
Anayataja mambo ya kuzingatia ili kuiepusha jamii na ongezeko au uwezekano wa kuwa na wenye ulemavu wa akili katika familia zetu kuwa ni pamoja na kuzingatia umri wa kubeba mimba na kuzaa. Anasema elimu ya afya ya uzazi na uzazi salama ifundishwe katika shule za msingi, sekondari na kliniki za afya ya uzazi na mtoto.
Anasema kinamama waelimishwe umuhimu wa kuhudhuria kliniki mara tu wanapojigundua kuwa wana ujauzito,ili kupimwa afya zao , kupata chanjo stahili lishe bora na dawa za kuzuia malaria.
Ulemavu wa akili hauna tiba wala wasipoteze fedha kwa waganga wa kienyeji kutafuta tiba, ila mtoto anaweza kusaidiwa kujitegemea kiakili kwa msaada wa wataalamu wa afya ya akili.
Maoni au maswali tuma afya@mwananchi.co.tz au 0713247889
No comments:
Post a Comment