Friday, 10 July 2015

"KWAHERINI"

RAIS Jakaya Kikwete ameaga Bunge kwa kushukuru Watanzania huku akisema anaondoka akijivunia amani, utulivu na kusisitiza kuwa nchi iko salama.

Pia, amesema anafurahi kuondoka madarakani akiwa ametimiza kwa asilimia 88 ya ahadi zake zilizopo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kusema atawakumbuka sana Watanzania, ingawa ‘atawamisi’.
Rais Kikwete ambaye amesema wanaoitakia mabaya nchi washindwe na walegee, alisema nchi na mipaka yake iko salama. Akihutubia Bunge la 10 jana, alisema zipo changamoto mbalimbali ambazo hakuzimaliza na ana imani zitafanyiwa kazi na serikali ijayo.
“Kwa ndugu zangu Watanzania wenzangu, nawashukuruni kwa kuniamini na kunichagua mara mbili kuwa kiongozi wa nchi yetu. Nawashukuru kwa kuniunga mkono wakati wote wa uongozi wangu. Nitawamisi “Mmenipa heshima kubwa ambayo sitakaa nisahau maishani mwangu. Namaliza kipindi changu cha uongozi nikiwa nawapenda sana na nitaendelea kuwapenda mpaka siku Mwenyezi Mungu atakaponiita. Nitawa miss kama mtumishi na kiongozi wenu mkuu, lakini tutakutana kwa urahisi zaidi nikiwa raia,” alisema.
Msininunie
Pia alishukuru viongozi wote walioonesha nia ya kuwania urais na kuwataka wote wanaotaka nafasi hiyo, wasimnunie kwani ana kazi ngumu katika kupunguza majina ya wanaowania kupitia CCM hadi kufikia majina matano.
Alisema hata wakati wa Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa zilikuwepo changamoto mbalimbali.
Amani na usalama Akizungumzia suala la amani, alisema aliiahidi Tanzania kuendelea kuwa nchi moja na watu wake wanaendelea kuwa wamoja, wanaopendana na kushirikiana licha ya tofauti zao za rangi, dini, makabila, mahali watokako na ufuasi wa vyama vya siasa.
“Pia, kwamba nchi yetu inaendelea kuwa yenye amani, usalama na utulivu. Leo tunapoagana, ninyi na mimi, ni mashuhuda kuwa Tanzania na Watanzania tumebakia kuwa wamoja,” alisema.
Hata hivyo, alisema yalikuwapo matukio ya hapa na pale madogo na makubwa, yaliyotishia umoja wa nchi na watu wake.
“ Yapo mambo yaliyopandikizwa kuleta chuki baina ya Tanzania Bara na Zanzibar, baina ya Wakristo na Waislamu na baina ya maeneo fulani ya nchi na wengine. Bahati nzuri, msimamo thabiti wa viongozi wakuu wa Serikali zetu mbili wakisaidiwa na viongozi wengine pamoja na ushirikiano na viongozi wa dini na wa jamii na uelewa wa wananchi, vimeliwezesha taifa letu kushinda changamoto hizo na matishio yote hayo,” alisema Rais Kikwete.
Alishukuru viongozi wenzake wa serikali, viongozi wa dini, viongozi wa jamii na wananchi wote kwa nafanikio yaliyopatikana katika kudumisha umoja wa nchi. Nchi iko salama Kuhusu ulinzi wa nchi, alisema hali ni nzuri na kwamba nchi ipo salama.
Alisema Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limeendelea kutimiza ipasavyo jukumu lake la kulinda uhuru na mipaka ya nchi. Alisema katika kipindi hiki, tumewekeza sana katika kuliimarisha Jeshi letu kwa vifaa na zana za kisasa za kivita na mafunzo.
"Tumeimarisha Kamandi za Nchi Kavu, Anga na Majini. Utayari wa jeshi letu kivita ni mzuri tena wa hali ya juu. “Weledi na nidhamu ya wanajeshi wetu ni ya hali ya juu. Tumeboresha maslahi na makazi ya wanajeshi kwa kujenga nyumba mpya za kuishi. Namaliza kipindi changu cha kuwa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama kwa kujiamini kwamba tupo vizuri,” alisema Rais Kikwete.
Muungano
Alisema anafurahi kumaliza kipindi chake cha miaka 10 ya kuwa Rais wa Tanzania kukiwa muungano umedumishwa na kuimarika kwa kiasi kikubwa.
“Mtakumbuka kuwa katika hotuba yangu ya kufungua Bunge la Tisa nilisisitiza umuhimu wa viongozi wa pande zetu mbili kukutana mara kwa mara kuzungumzia ustawi wa Muungano wetu,” alisema.
Aliendelea kusema kwamba mafanikio yaliyopatikana ni makubwa ikiwamo masuala mbalimbali ya zamani na mapya, yaliyoshughulikiwa na kupatiwa ufumbuzi.
Alitoa mfano kwamba hadi mwaka 2005, zilikuwa zimebakia kero 13 za Muungano, zilizoainishwa na Tume ya Shelukindo, na sasa zimebaki kero nne.
“Tayari ufumbuzi wa kero moja unakamilishwa kiutawala na tatu zimeshughulikiwa katika Katiba Inayopendekezwa. Kama kura ya maoni ingekuwa imefanyika na Katiba hiyo kupitishwa kungekuwa hakuna kiporo cha kero za Tume ya Shelukindo. Lakini kwa vile kura ya maoni haijafanyika ndiyo maana tunaendelea kuzitaja,” alisema.
Alieleza kuwa Serikali zote mbili zimezungumza na kukubaliana itafutwe njia ya kumaliza suala la rasilimali ya mafuta na gesi.
“Ndiyo maana katika Muswada wa Petroli, hoja ya Zanzibar kuwa na mamlaka kamili ya kusimamia uchimbaji wa mafuta na kumiliki mapato yake ilijumuishwa. “Natoa shukrani nyingi kwa Bunge lako tukufu kwa kupitisha Muswada huo. Moja ya kero kubwa katika Muungano tumeimaliza,” alisema Rais Kikwete.
Mpasuko Zanzibar
Pia alizungumzia mpasuko wa kisiasa Zanzibar na kwamba anashukuru viongozi wa vyama vya CCM na CUF, waliofanya mazungumzo na kufikia mwafaka uliozaa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
“Ni matumaini yangu kuwa ndugu zetu wa Zanzibar watayadumisha mafanikio haya ili waendelee kuishi kwa amani, upendo na udugu. Natambua kuwepo kwa changamoto za hapa na pale katika uendeshaji wa Serikali hiyo,” alisema.
Alisema jambo linalompa faraja ni kwamba matatizo yenyewe, hayahusu muundo wa Serikali, bali yanaletwa na watu kupishana kauli au kutofautiana katika uendeshaji wa baadhi ya mambo.
Kikwete alisema anaamini hayo ni mambo yanayoweza kumalizwa kwa wadau kukaa kitako na kuzungumza kama ilivyokuwa kabla.
Uhalifu umepungua
Alisema katika kipindi chake cha miaka 10, wamefanya jitihada kubwa kupambana na uhalifu ikizingatiwa kwamba, aliahidi na kutekeleza kwamba hataacha majambazi watambe.
“Niliahidi wakati wa kampeni na katika hotuba yangu bungeni kwamba hatutawaacha majambazi waendelee kutamba. Hali ile imedhibitiwa. Ingawaje matukio ya ujambazi hayajaisha, lakini hayako kama ilivyokuwa wakati ule,” alisema.
Aliwashukuru Inspekta Jenerali wastaafu Omar Mahita na Said Mwema pamoja na wa sasa, Ernest Mangu, kwa uongozi mzuri katika kuhakikisha wahalifu wanadhibitiwa.
Alisema Polisi inaendelea kuwezeshwa kwa zana, vifaa na mafunzo na kwamba taratibu zimekamilika za kupatia jeshi hilo magari ya kutosha kuongeza ufanisi na kwamba wameendelea kuboresha maslahi na mazingira ya kuishi maafisa na askari.
Pia, alisema Jeshi la Magereza nalo limeendelea kutekeleza vizuri majukumu yake ya kulinda wafungwa na kurekebisha tabia zao. Alisema huduma za malazi, mavazi, chakula na usafiri kwa wafungwa zimeendelea kuboreshwa na changamoto kubwa ni msongamano wa wafungwa Magerezani.
“Naamini mipango ya kujenga magereza mapya na kupanua yaliyopo ikitekelezwa tatizo litaisha,” alisema Rais Kikwete.
Utawala bora
Alisema katika kipindi chake ametekeleza dhamira ya kujenga na kuimarisha utawala bora kwa sera, sheria, mifumo, taasisi na kwa rasilimali watu.
Alisema yamefanyika hayo katika maeneo yote muhimu yakiwemo yahusuyo haki za binadamu, demokrasia, mapambano dhidi ya rushwa, maadili ya viongozi, ukusanyaji wa mapato na nidhamu ya matumizi ya fedha za umma na mgawano wa madaraka kati ya mihimili.
Aidha, alisema katika kipindi chake, vyama vya siasa vikiendelea kuimarika na kujijenga nchini na kwamba idadi ya vyama vya siasa imeongezeka kutoka 18 hadi 24.
“Vyama vya siasa vimefanya shughuli zake kwa uhuru. Viongozi na wanachama wao wamefanya mikutano mingi na hata maandamano kote nchini. Baraza la Vyama vya Siasa na TCD vimekuwa vyombo muhimu vilivyofanya kazi nzuri ya kujenga ushirikiano miongoni mwa vyama vya siasa. Ni matumaini yangu kuwa vyombo hivi viwili vitaendelezwa na kuimarishwa miaka ijayo. “Huu ni mwaka wa uchaguzi, na vyama vya siasa ndiyo wahusika wakuu. Ni matumaini yangu kuwa vyama vya siasa vitaheshimu na kuzingatia maadili ya uchaguzi. Hii itasaidia kuwepo kwa utulivu na amani katika mchakato wa uchaguzi,” alisema.
Uchaguzi Mkuu
Alisema maandalizi ya uchaguzi huo, yanaendelea vizuri na Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea na uandikishaji wa wapiga kura kwa mfumo mpya wa teknolojia ya Biometric Voters Register (BVR). Alisema hadi sasa uandikishaji umekamilika katika mikoa 13 na inaendelea katika mikoa 11.
Katika mkoa wa Dar es Salaam na Zanzibar, uandikishaji unategemea kuanza mwezi huu. Tayari wapiga kura milioni 11 wameandikishwa, kati ya lengo la kuandikisha wapiga kura kati ya milioni 21 hadi 23.
Uhuru wa habari
Alisema katika kipindi chake, uhuru wa habari umeimarika kutokana na uwapo wa magazeti ya kila siku 16, ambayo kati yake, mawili pekee ndiyo ya serikali; Daily News na HabariLeo.
Alisema pia magazeti ya kila wiki yapo 62 na vipo vituo vya redio kutoka 115 na vya televisheni 29. Alisisitiza katika kuhakikisha uhuru upo, Serikali haifanyi uhakiki wa habari kabla ya kuchapishwa au kuandikwa.
“Tumeamua hivyo kwa imani yangu kwamba ustawi wa demokrasia hutegemea sana uhuru wa vyombo vya habari. Pili, kwa vile tunatambua manufaa ya vyombo vya habari kuelimisha jamii, kupambana na maovu na kuhimiza uwajibikaji,” alisema.
Vita dhidi ya rushwa
Alisema rushwa ni eneo jingine ambalo alilivalia njuga katika uongozi wake na kupata mafanikio ya kuridhisha.
“Tumefanya mambo matatu. Kwanza, tumetunga Sheria Na. 11 ya mwaka 2007 ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ambayo imeongeza nguvu ya mapambano dhidi ya uovu huu. Idadi ya makosa ya rushwa iliongezwa kutoka 4 mpaka 24 na wigo wa wakosaji pia, kwa kuhusisha watu katika sekta binafsi. Mifumo ya upelelezi na uendeshaji mashitaka nayo imeimarishwa. “Tumeunda chombo kipya Takukuru badala ya Takuru ambacho kimepewa majukumu ya kuzuia na kupambana na rushwa badala ya kuzuia peke yake. Tumeiwezesha Takukuru kufungua ofisi katika Mikoa na Wilaya zote.
Mapato
Alisema aliahidi kutoa kipaumbele juu kwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali na nidhamu ya matumizi ya Serikali na kwamba anaona fahari amepata mafanikio makubwa.
“Mapato ya Serikali yameongezeka kutoka Sh bilioni 177.1 mwaka 2005 kwa mwezi hadi takriban Sh bilioni 850. Hii imewezesha bajeti ya Serikali kukua kutoka Sh trilioni 4.13 mwaka 2005/2006 hadi Sh trilioni 22.49 mwaka 2015/2016.
“Isitoshe imetuwezesha kupunguza misaada na mikopo ya washirika wa maendeleo kutoka asilimia 42 ya Bajeti ya Serikali mwaka 2005 hadi asilimia 15 mwaka 2014/2015 na tumejipa lengo la kushusha zaidi hadi asilimia 8 mwaka huu wa fedha wa 2015/2016,” alisema.
Maadili ya viongozi
Alisema katika miaka 10 hii ameimarisha mfumo wa kusimamia maadili ya viongozi amefanya hivyo kwa kutambua kuwa maadili mema ni sifa ya msingi ya kiongozi na huiletea heshima Serikali.
Alisema katika uongozi wake ameunda Kamati ya Maadili na kuunda Baraza la Maadili kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma namba 13 ya 1995.
Hali ya uchumi
Alisema wakati anaingia madarakani mwaka 2005, aliwaahidi Watanzania kuwa atafanya kila awezalo kujenga uchumi ulio imara na shirikishi.
“Katika miaka kumi iliyopita tumeendelea kusimamia kwa kiwango kizuri sera za uchumi jumla na sera za uchumi katika ngazi ya chini zinazogusa wananchi wa kawaida. “Jitihada zetu hizo zimezaa matunda ya kutia moyo. Katika kipindi hiki, Pato la Taifa lilikua kwa wastani wa takriban asilimia 7.
Nchi yetu ni miongoni mwa mataifa 10 ya Afrika na 20 duniani ambayo uchumi wake unakua kwa kasi kubwa. Pato ghafi la Taifa limeongezeka zaidi ya mara tatu kutoka shilingi trilioni 14.1 mwaka 2005 hadi kufikia trilioni 79.4 mwaka 2014.,” alisema.
Gesi
Alisema serikali imepata mafanikio katika utafutaji wa mafuta na gesi asilia, ambapo kuanzia mwaka 2010 nchi imepata bahati ya ugunduzi wa kiasi kikubwa cha gesi bahari kuu na mpaka sasa zimegundulika futi za ujazo trilioni 47.08.
“Ukijumlisha na futi za ujazo trilioni 8 zilizogunduliwa takriban miaka 40 iliyopita kule Songo Songo na Msimbati jumla ya rasilimali ya gesi asilia nchini ni futi za ujazo trilioni 55.08. Kazi ya utafutaji inaendelea na wataalamu wanasema kuwa Tanzania inaweza kuwa na akiba ya futi za ujazo trilioni 200. Kiasi cha gesi kilichogunduliwa mpaka sasa ni kikubwa na kufanya Tanzania kuwa mahala papya pa kuipatia dunia nishati hii,” alisema.
Elimu
Alisema anaondoka akifurahia kwamba Tanzania imepiga hatua kubwa katika elimu na kwamba ametimiza ahadi kwani katika kipindi chote cha miaka kumi bajeti ya sekta ya elimu ndiyo iliyokuwa kubwa kuliko za sekta nyingine zote.
Alisema mwaka huu 2015, bajeti ya elimu imefikia shilingi trilioni 3.4 ikilinganishwa na shilingi bilioni 669.5 za mwaka 2005.
“Mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya elimu ndani ya miaka 10 hii ni ya kutia moyo. Tumeongeza shule za msingi kutoka 14,257 mwaka 2005 hadi 16,538 mwaka 2015 na wanafunzi wameongezeka kutoka 7,541,208 hadi 8,202,892.
Upanuzi huu umewezesha asilimia 98 ya watoto wanostahili kupata elimu ya msingi sasa kuandikishwa. “Katika kipindi hiki pia tumeshuhudia upanuzi mkubwa wa elimu ya juu nchini. Idadi ya vyuo vikuu imeongezeka kutoka vyuo 26 mwaka 2005 hadi 52 mwaka 2015,” alisema.
Pinda, Makinda waaga
Awali, Waziri Mkuu , Mizengo Pinda, akisoma hotuba yake bungeni kabla ya Rais Kikwete kuwasili, aliomba radhi wabunge kwa kusema kama kuna mahali aliwakosea, wamuwie radhi.
Kwa upande wake, Spika Anne Makinda aliwaaga wabunge na kusisitiza kauli aliyowahi kuitoa kwamba hatagombea tena katika uchaguzi ujao jimboni kwake Njombe Kaskazini.
Hata hivyo, Rais Kikwete alisema Bunge bado lina uhai hadi Agosti 20 mwaka huu atakapotangaza kwenye gazeti la serikali.
Akimshukuru Rais Kikwete kwa hotuba yake, Makinda alisema hotuba yake imeweka bayana kazi zilizofanywa katika nchi na rais, wabunge na viongozi wengine.
Alisema watanzania wenye nia njema wamesikia na kupata ukweli kwa kuwa katika akili ya kibinadamu, wapo waliokuwa wakiamini kwamba hakuna kilichofanywa na serikali.
Makinda alimsifia Rais Kikwete kwa kuwa mtu wa watu. Alishukuru utaratibu wa marais kuachiana madaraka na kusema unawafanya waishi kwa raha.
“Tulicho nacho tuimarishe, tabia tulizo nazo nzuri tuzijenge,” alisema Makinda na kushutumu vitendo vya vurugu wakati wa kupiga kura na hata uandikishaji katika BVR. Habari hii imeandikwa na Amir Mhando na Namsembaeli Mduma, Dodoma.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!