Saturday, 4 July 2015

JK: WAFADHILI WAMEIPA KISOGO SEKTA YA MAJI

TANZANIA imefanikiwa katika sekta mbalimbali kutokana na misaada kutoka Benki ya Dunia, lakini haijafanikiwa katika sekta ya maji kutokana na sekta hiyo kutopewa kipaumbele na wafadhili.
Hayo yalisemwa jana na Rais Jakaya Kikwete wakati wa uzinduzi wa chapisho kuhusu Maadhimisho ya Miaka 50 ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Benki ya Dunia.
Alisema ushirikiano wa Tanzania na Benki ya Dunia, umefanya kazi kwa miaka 50 ambayo ni ya mafanikio, lakini maji bado yamekuwa changamoto katika maeneo mbalimbali ikiwemo vijijini na mijini.
Aliongeza kuwa ni vyema wafadhili ikiwemo benki ya dunia kusaidia sekta ya maji kutokana na maji kuwa hitaji muhimu na kubwa.
Alisema wananchi wengi wamekuwa wakihangaika na kuacha kufanya mambo ya maendeleo matokeo yake wanahangaikia maji, hivyo ni vyema sekta ya maji isaidiwe.
“Ukosefu wa maji unasababisha mambo mengi yakiwemo magonjwa na kama jamii itakosa maji basi magonjwa mengi yataibuka ikiwemo vichocho, wanawake wengi wanateseka kutokana na kutafuta maji umbali mrefu,” alisema Kikwete.
Pia alisema kwa upande wa sekta ya kilimo Tanzania imeweza kufanikiwa japo bado kuna changamoto ya sehemu za kuhifadhia mazao pamoja na uhaba wa masoko.
“Na imani mtaendelea kushirikiana nasi kwa upande wa masoko ili uchumi wetu uzidi kukua yapo mengi ya kufanya lakini haya yakifanikiwa tutafika mbali,” aliongeza Kikwete.
Aliongeza kuwa Tanzania imeendelea na kupambana na rushwa kwani mpaka sasa rushwa imedhibitiwa kwa kiasi kikubwa huku lengo likiwa ni kufikia asilimia sifuri.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia Afrika Makhtar Diop alisema, ni furaha kuona ubia kati ya benki ya dunia na Tanzania umefikia miaka 50 ambayo ni miaka ya mafanikio kwa pande zote mbili.
Alisema unapozungumzia miaka 50 ya Benki ya Dunia ni vyema kutambua mchango wa Rais wa Awamu ya Kwanza Mwalimu Julius Nyerere kwani alikuwa na uhusiano wa karibu sana na Mc Namara wote wakiwa na dhamira ya pamoja ya kukidhi mahitaji ya msingi ya kila mtanzania.
“Baada ya kukaribia kuanguka kabisa kwa uchumi wa Tanzania miaka ya 80 Tanzania iliamua kuanza kutumia zaidi mbinu zenye mtazamo wa soko nah ii ndio ilianzisha ubia kati ya Tanzania na Taasisi ya Benki ya Dunia,” alisema Diop.


Alisema kupitia miaka 1980 na 1990 benki ya dunia iliweza kusaidia Tanzania kufufua uchumi na kuwa wa wazi zaidi na nguzo ya uchumi imara.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!