Sunday, 12 July 2015

JK ATAKUMBUKWA KWA TAKWIMU ZA UTENDAJI

UONGOZI wa Rais Jakaya Kikwete unaotarajiwa kuondoka madarakani mwishoni mwa mwaka huu, pamoja na changamoto mbalimbali, utakumbukwa kwa mafanikio yaliyojidhihirisha kitakwimu na katika maisha ya watu.

Takwimu alizotangaza juzi katika hotuba yake ya kuaga wabunge, zimeonesha kuwa mafanikio ya uongozi huo wa Awamu ya Nne, yameanzia katika kupunguza baadhi ya gharama za maisha na kuongeza kipato cha wananchi.
Mbali na hatua hizo, ubora wa maisha ya Watanzania katika wakati wa uongozi huo ulioongozwa na kauli mbiu ya ‘Maisha Bora kwa Kila Mtanzania’, umeonekana kuanzia katika ongezeko la umri wa kuishi kwa watanzania, kupungua kwa udumavu wa watoto na ubora wa makazi ya wananchi.
Gharama za maisha
Moja ya mbinu ya kupunguza gharama za maisha duniani ni kuongeza kipato cha watu, ambapo Rais Kikwete katika hotuba yake ya juzi, alieleza namna alivyoongeza mshahara wa wafanyakazi na kupunguza kodi inayokatwa katika mishahara hiyo.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, wakati alipoingia madarakani mwaka 2005, alikuta mshahara wa kima cha chini ni Sh 65,000, huku kodi inayokatwa katika mshahara huo (PAYE), ikiwa asilimia 18.
Katika jitihada za kumpunguzia mwananchi gharama za maisha, Rais Kikwete alisema Serikali yake ilianza kuongeza mshahara wa kima cha chini ambapo sasa anaondoka ukiwa Sh 300,000 kwa mwezi, huku kodi hiyo ikiwa asilimia 11.
Mbali na hatua hiyo iliyogusa moja kwa moja kundi kubwa la wananchi wanaofanya kazi, jitihada za uongozi huo zilisababisha pato la Taifa kuongezeka kwa asilimia saba na kuwa miongoni mwa nchi 10 Afrika na nchi 20 duniani zenye uchumi unaokua kwa kasi.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, pato ghafi la Taifa (GDP), limeongezeka zaidi ya mara tatu kutoka Sh trilioni 14.1 mwaka 2005, hadi kufikia trilioni 79.4 mwaka 2014.
Kwa mafanikio hayo, kitakwimu pato la wastani la Mtanzania nalo limeongezeka kutoka Sh 441,030 mwaka 2005 hadi Sh 1,724,416 mwaka 2014.
Shughuli za kiuchumi zilizofanyika ndani ya nchi, ikiwemo katika uzalishaji wa mazao ghafi mpaka mazao ya viwandani na kuuzwa kama huduma na bidhaa nje ya nchi, wameongezeka kutoka mauzo ya dola za Marekani bilioni 1.6 mwaka 2005, mpaka Dola za Marekani bilioni 8.67, mwaka jana.
Katika kilimo kinachotegemewa na Watanzania wengi kwa chakula, Rais Kikwete alisema uzalishaji wa chakula umeongezeka kutoka tani milioni 9.66 mwaka 2005 hadi tani milioni 16.01 mwaka 2014.
Ongezeko hilo limeliwezesha taifa kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 125 mwaka 2014 ikilinganishwa na asilimia 95 mwaka 2005.
Katika matumizi ya simu, ambayo yameleta mapinduzi katika uchumi, kijamii na hata kisiasa, Rais Kikwete alisema gharama za simu zilipungua ikilinganishwa na mwaka 2005, kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika Mkongo wa Taifa.
Kutokana na uwekezaji huo, gharama za kupiga simu zimeshuka kutoka Sh 115 kwa dakika mwaka 2005, hadi Sh 34.92 mwaka 2014, huku gharama za intaneti zikishuka kutoka wastani wa Sh 36,000 kwa Gigabyte moja mwaka 2005, hadi wastani wa Sh 9,000 kwa Gigabyte moja (GB 1) mwaka 2014.
Umri wa kuishi, makazi bora
Mbali na jitihada hizo chache kati ya nyingi za kuongeza kipato cha Watanzania na kupunguza gharama zao za maisha, uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tatu, umeshuhudia ubora wa maisha ya Watanzania ukiongezeka.
Kwa mfano kwa takwimu zilizotokana na Sensa ya Makazi na Watu, zimethibitisha kuwa idadi ya nyumba zilizoezekwa kwa bati zimeongezeka kutoka asilimia 46 mwaka 2002 hadi asilimia 65 mwaka 2012.
Katika kufafanua hili, Rais Kikwete alisema tafsiri yake ni kwamba mbali na kuongeza kipato na kupunguza gharama za maisha, nyumba za Watanzania zilizoezekwa kwa makuti na nyasi zimezidi kupungua.
Mbali na kuongezeka kwa nyumba zilizoezekwa kwa bati, Watanzania wanaotumia umeme nchini, pia wameongezeka na hivyo kuongeza ubora wa maisha yao kutoka asilimia 10 mwaka 2005, hadi asilimia 40 mwaka 2015.
Vyombo vya usafiri wa pikipiki, bajaji na magari ambavyo vinaleta ufanisi wa huduma muhimu ya usafiri nchini, navyo vimeongezeka kutoka 1,696,088 mwaka 2005 hadi 3,313,254 mwaka huu.
“Ongezeko hili linalotokana na hali ya kiuchumi ya watu wengi kuwa nzuri, lakini limezua tatizo la msongamano wa magari katika miji mingi nchini,” alisema Rais Kikwete.
Afya bora
Katika ubora wa afya ya Watanzania, takwimu zimethibitisha kuwa vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka vifo 68 kwa kila vizazi hai 1000 mwaka 2005, hadi vifo 21 kwa kila vizazi hai 1,000 mwaka 2014.
Vifo vya watoto chini ya miaka mitano pia vimepungua kutoka vifo 112 kwa kila vizazi hai 1000 mwaka 2005 hadi vifo 54 kwa kila vizazi hai 1000 mwaka 2014, na vifo vya wajawazito vimepungua kutoka vifo 578 kwa vizazi hai 100,000 hadi vifo 432 kwa vizazi hai 100,000 mwaka 2012.
Aidha, udumavu wa watoto umepungua kutoka asilimia 44 mwaka 2005 hadi asilimia 35 mwaka 2014 na uzito pungufu kutoka asilimia 17 hadi asilimia 13.

HABARI LEO

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!