Friday, 24 July 2015

HABARI ZAIDI JUU YA AJALI YA BASI LA SIMIYU ILIYOUA WATU 10 NA MAJERUHI 53

mail.google.com
Watu kumi wamekufa kwenye ajali ya basi la Simiyu lenye namba za usajili T.318 ABM iliyotokea juzi maeneo ya Chalinze wilayani Chamwino mkoani hapa huku majeruhi na mashuhuda wakisema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva.


 
Basi hilo ambalo lilikuwa likitokea Mwanza kuelekea Dar es Salaam ilitokea juzi  saa 12:30 jioni.
 
NIPASHE lilizungumza na baadhi ya majeruhi hao ambao walisema ajali hiyo ilitokana na mwendo kasi ya dereva.
 
Mmoja wa majeruhi hao, Sawika Saganda (40), alisema watu wengi waliumia na kufa kutokana na kubanwa na viti.
 
Aidha, alisema wakati gari likiwa kwenye mwendo mkali tairi lilipasuka na ndipo gari lilisererekea msituni na kugonga mbuyu.
 
Naye, Rai Khatib (21), alisema dereva alikuwa kwenye mwendo kasi ndipo tairi lilipopasuka na kagi kuelekea msituni na kugonga mbuyu.
 
Majeruhi Edgar Simpito (39), alisema alipanda gari hilo Dodoma ambapo walipofika maeneo ya Mtumba na Chamwino Ikulu, madereva walibadilishana magari.
 
Alisema dereva wa Simiyu lilipopata ajali walibadilishana na basi la Happy Nation ambalo lilikuwa likitokea Dar es Salaam kuja Dodoma ambapo dereva huyo hakwenda muda mrefu na ajali kutokea.
 
Kwa upande wa mashuhuda wa ajali hiyo, walisema ajali hiyo ilitokana na mwendo kasi wa dereva uliyochangia kwa kiasi kikubwa gari kupoteza muelekeo na kuingia porini na kugonga mti.
 
Lucy Kalulu alisema chanzo kikubwa cha ajali hiyo kilisababishwa na mwendo kasi na ndiyo maana tairi likapasuka na gari kupoteza muelekeo.
 
Alisema gari lisingekuwa na mwendo kasi lingeyumba kidogo na kutulia bila ya kuingia msituni.
 
Naye Pius Augustino alisema ajali hiyo inawezekana tairi zilikuwa zimechoka na ndiyo maana likapasuka.
 
Alisema madereva wa magari wanatakiwa kuwa makini na kuyachunguza magari yao kabla ya kuanza safari.
 
Akizungumza na waandishi wa habari, Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk. Ezekiel Mpuya alithibitisha kupokea maiti nane na majeruhi 55.
 
Alisema maiti mbili ziliongezeka kutoka kwa majeruhi 55 ambao walikuwa kwenye matibabu.
 
Alisema waliokufa wakiwa hospitalini hapo ni mwanamke mjamzito, Rukia Mkupe na Mussa Kashinde.
 
Mbali na hao, wengine ni Elias Mibawa, Mfungo Matutu, Emmanuel Binamungu, Salum Ramadhan, Nestory Ambloz, Shimba Masungu, Maduhu Lushanga na Charles Mahushi.
 
Alisema hali ya majeruhi hao zinaendelea vizuri ambapo 27 wameruhusiwa, huku mmoja akipewa rufaa ya kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na wengine 28 wakiendelea kutibiwa hospitalini hapo.
 
Akizungumzia ajali hiyo, Kaimu Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, David Mnyambugha alikiri kutokea kwa ajali hiyo saa 12:30 jioni.
 
Alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika hospital ya rufaa ya mkoa wa Dodoma.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!