Wednesday 29 July 2015

ELIMU YA MADINI KUTOLEWA KWA WAKUU WA WILAYA KANDA YA KASKAZINI AGOSTI,12

RE1
Afisa Madini Mkazi, Mkoa wa Kilimanjaro, Fatuma Kyando akielezea  sheria na kanuni za uchimbaji wa madini  nchini katika mafunzo  yaliyoshirikisha wachimbaji wa madini Mirerani kuanzia  tarehe 25 hadi 26 Julai, 2015. Lengo la mafunzo hayo lilikuwa ni kuwapa uelewa juu ya  huduma za leseni kwa njia ya mtandao.


RE2
Mtaalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Kitengo cha Leseni Charles Gombe (kulia) akihakiki leseni  ya mmoja wa wachimbaji (katikati) Kushoto ni Afisa Madini katika Ofisi ya Madini, Mirerani, Denis Mrengo
RE3
Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda ya Kaskazini Alex Magayane (kulia) akifungua mafunzo hayo.
RE4
Baadhi ya washiriki wa  semina hiyo wakifuatilia kwa makini mada zilizokuwa zinawasilishwa kwa  nyakati  tofauti.
RE5
Mjiolojia katika Ofisi ya Afisa Madini Mkazi -Mirerani, Amir Chande Ramadhani (kushoto) na Mtaalam kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Kitengo cha Leseni Charles Gombe (kulia) wakifuatilia tovuti  ya huduma za leseni  kwa njia ya mtandao (online mining cadastre transactional portal) kwenye mafunzo hayo.
……………………………………………………………………
Na Greyson Mwase, Arusha
Imeelezwa kuwa  ili kuondokana na migongano kwenye usimamizi wa sekta ya madini Kanda  ya Kaskazini, Wizara ya Nishati na Madini  imeandaa mafunzo kuhusu sekta ya madini  yatakayoshirikisha  viongozi mbalimbali katika mikoa ya Manyara, Arusha na Kilimanjaro yanayotarajiwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu.
Akizungumza katika mahojiano maalum jijini Arusha jana, Afisa Madini Mkazi, Mkoa wa Kilimanjaro, Fatuma Kyando alisema kuwa mafunzo hayo yatashirikisha wakuu wa wilaya,  wakurugenzi wa halmashauri,  maafisa tawala wa wilaya, watendaji na wenyeviti wa vijiji na kata na wawakilishi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA)
Alieleza kuwa katika usimamizi wa sekta ya madini katika kanda hiyo, kumekuwepo na mgongano wa mamlaka ambapo kila upande umekuwa ukiona una nguvu kuliko  mwingine kwenye utoaji na usimamizi wa leseni za madini.
Alisema ni vyema kila mamlaka ikafahamu  majukumu na mipaka yake katika usimamizi wa  shughuli za madini ili kuzuia migogoro  inayoweza kujitokeza.
Alisisitiza kuwa  kati ya mambo watakayojifunza ni pamoja na sheria na kanuni za madini, utunzaji wa mazingira katika shughuli za madini na  fursa za madini  yaliyopo.
Akielezea changamoto  nyingine katika usimamizi wa shughuli za utafutaji na uchimbaji wa madini katika kanda hiyo, Kyando alisema kumekuwepo na  migongano kwenye tozo  la kodi kwenye mapato yatokanayo na madini.
Alisema mapato  wanayokusanya  wamekuwa wakiwasilisha  serikali huu  ambapo  fedha hizo  hurudishwa tena kwenye  halmashauri  kwa ajili ya kuimarisha  huduma za jamii lakini bado watu wamekuwa wakihoji kwanini  fedha hizo zisilipwe  moja kwa moja tu kwenye halmashauri na kutumika kwa maendeleo moja kwa moja.
Aliongeza kuwa hali hii inatokana na wananchi na   viongozi kutokuwa na uelewa wa sheria na kanuni za madini  na ndio maana ofisi  yake imeandaa mafunzo hayo.
Alisema kuwa mafunzo hayo yatawawezesha  mamlaka zote kuwa na lugha moja na kufanya kazi kwa pamoja na kuzuia migogoro inayoweza kujitokeza.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!