Watu kumi wamefariki dunia jana katika matukio tofauti ya ajali ya gari na kuteketea kwa moto kwenye matukio yaliyotokea wilayani Siha na Bukoka.
Tukio la Bukoba, watu watano wa familia moja wamefariki dunia kwa kuteketezwa na moto na watu wenye hasira kwa madai ya kumuua mfanyabiashara mmoja, wilayani Kyerwa, mkoa wa Kagera.
Aidha, tukio lililotokea wilayani Siha, watu watano wamekufa papo hapo na wengine 11 wakiwa mahututi, baada ya lori la mizigo Mitsubish Fusso, kuigonga Hiace linalofanya safari zake kati ya miji ya Sanya Juu, Wilaya ya Siha na Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro.
Ajali hiyo iliyotokea jana saa 12:40 asubuhi katika daraja la mto Kikavu, Wilaya ya Hai, iliyahusisha Fusso lenye namba za usajili T 430 AAQ na Toyota Hiace, T 196 AAW lililokuwa linaendeshwa na dereva anayefahamika kwa jina la ‘Baba D’.
Habari zilizopatikana katika eneo la tukio na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kilimanjaro (SACP), Fulgence Ngonyani, zinaeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa lori ambaye hata hivyo, alitokomea baada ya kusababisha ajali hiyo.
Alisema baadhi ya majeruhi walikimbizwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC na wengine walipelekwa Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Kilimanjaro (Mawenzi) kwa matibabu. Kamanda Ngonyani alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Mawenzi ikisubiri kutambuliwa na ndugu na jamaa zao.
Hata hivyo, watu walioshuhudia ajali hiyo, waliieleza NIPASHE kwamba, dereva wa lori hilo aliligonga kwa nyuma basi dogo la abiria katikati ya daraja, wakati akitokea katika mji mdogo wa Kwa Sadala na kusababisha vifo hivyo.
Grayson Kweka, mkazi wa Kwa Sadala, wilayani hapa alisema, “Huyu dereva wa Fusso alikuwa amepakia mchele na alikuwa akielekea Moshi Mjini, alipofika karibu na daraja la mto Kikavu, lori lilimshinda kutokana na mwendo kasi aliokuwa nao na hivyo kuigonga Hiace na kuua abiria watano papo hapo, akiwamo kondakta wa basi hilo.”
Afisa habari na mahusiano wa KCMC, Gabriel Chisseo aliiambia NIPASHE kuwa walipokea majeruhi saba wa ajali hiyo, wakiwa katika hali mbaya na kulazimika kuingizwa katika chumba maalum cha upasuaji.
Aliwataja majeruhi waliolazwa hospitalini hapo kuwa ni Haji Mdangiwa, Fred Urassa, Levina Mnyampanda, Jenista Unonu, Antonia Msaki, Hawa Hamis na Julieth Massawe.
Katika tukio la kuteketezwa kwa familia ya watu watano huko Kyerwa, mbali na wananchi hao kuwaua wanafamilia hao, pia wameteketeza mashamba yao yenye ukubwa wa ekari 15 na nyumba nane na mali zote zilizokuwemo ndani.
Wakizungumza jana kwenye eneo la tukio wananchi, walisema kuwa watu wasiojulikana walipandwa na hasira baada ya kuwapo kwa taarifa za mfanyabiashara, Jovinary Morandi, kuuawa na kuzikwa kwenye shamba la Datusi Paulo.
Walisema watu hao waliwahisi wanafamilia hao kuwa ndiyo wamehusika na mauaji hayo kutokana na Paulo kuwa wakala wa marehemu na pikipiki ya marehemu kukutwa nyumbani kwake.
Waliouawa wametajwa kuwa ni Datusi Paulo (36), Lakius Paulo (30), Launtina Henericko (68), Sabiniani Henerico (35) na mtoto anayedhaniwa kuteketea ndani ya nyumba.
Waliobahatika kutoroka ni Adriani Henerico na familia yake ambaye ni mwalimu katika Shule ya Msingi Mugaba.
Akizungumzia tukio hilo, Frolian Henerico, mwanafamilia aliyekutwa na kuachwa hai na wananchi hao, alisema kuwa wananchi wa kijiji hicho na maeneo jirani walikuwa wamechoshwa na vitendo vya ushirikina na ujambazi walivyokuwa wanafanya wanafamilia hao.
Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Mugaba, Justinian Clemence, alisema alifuatwa nyumbani na wananchi na ndugu wa mfanyabiashara aliyeuawa wakiwa na mwenyekiti wa kitongoji cha Omukicherenje wakitaka kuanza msako wa kumtafuta ndugu yao baada ya kutoonekana nyumbani.
Clemence alisema kuwa aliwakubalia kwenda kwa mtuhumiwa ambaye alikuwa wakala wa mazao wa mfanyabiashara huyo, na kuwa baada ya kufika nyumbani kwa mtuhumiwa wakiwa kwenye mahojiano mafupi waliona damu na kuanza kufuatilia ilikoelekea ndipo waliona sehemu ikiwa imechimbuliwa na walipofukua waliona mwili wa mtu ndipo hasira za wananchi zilipoanza.
Mkuu wa wilaya ya Kyerwa, Luteni Edward Ole Lenga, akiongea na wananchi katika eneo la tukio baada ya kujionea hali halisi aliwataka kutojichukulia sheria mkononi kwani kufanya hivyo vyombo vya usalama vitakosa taarifa muhimu za kiuchunguzi.
*Imeandikwa na Godfrey Mushi na Lilian Lugakingira, Bukoba.
No comments:
Post a Comment