Monday, 29 June 2015

WASHUKIWA WA UGAIDI WANASWA MOROGORO

POLISI mkoani Morogoro kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama imekamata washukiwa wa ugaidi waliokuwa na mifuko mikubwa iliyokuwa na majambia na bunduki kadhaa aina ya Shot gun.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Mussa Marambo, alisema hayo jana mjini hapa na kufafanua kwamba ni washukiwa sita kati ya 50 waliotiwa mbaroni, huku msako ukiendelea kuwatafuta wengine.
Kwa mujibu wa Kamanda Marambo, Jumatano iliyopita Polisi iliarifiwa na raia wema kuhusu uwepo wa watu hao katika Msitu wa Njeula katika kijiji cha Njeula tarafa ya Turiani, wilayani Mvomero.
Kukamatwa
Baada ya taarifa hiyo, Kamanda Marambo alisema Polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama, walifika eneo la msitu huo kufuatilia nyendo zao ili kuwakamata.
Hata hivyo, katika harakati za kuwakamata Kamanda Marambo alisema washukiwa hao walifanikiwa kutoroka, isipokuwa mmoja ambaye alitiwa mbaroni.
Katika purukushani hiyo msituni, Kamanda Marambo alisema mshukiwa huyo aliyekamatwa, alijaribu kumjeruhi askari kwa kumkata na jambia mkononi, lakini umakini wa askari Polisi ulisaidia kumuepusha mwenzao asijeruhiwe na kukamata mshukiwa.
Msako wa watu hao uliendelea ambapo Kamanda Marambo alisema baada ya muda, washukiwa wengine watano kati ya 49 waliokuwa wametoroka, walitiwa mbaroni huku wengine 44 wakitokomea porini.
Walikotokea Uchunguzi wa awali wa Polisi, umebaini kuwa washukiwa hao wakiwa na mifuko hiyo mikubwa iliyohifadhi majambia na bunduki, walitokea wilayani Bagamoyo mkoani Pwani, kupitia Tanga huku wakitumia mabasi ya kuunganisha.
Kutoka Bagamoyo, Kamanda Marambo alisema washukiwa hao walizunguka kwa kwenda mpaka Segera mkoani Tanga, wakaingia Handeni ndipo wakatokea katika kijiji cha Njeula tarafa ya Turiani wilayani Mvomero.
Msako shirikishi Kwa mujibu wa Kamanda Marambo, msako mkali unaendeshwa katika msitu huo na mahali pengine ili kufanikisha kutiwa mbaroni kwa washukiwa waliobaki.
“Ninachoweza kusema kwa kushirikiana na wenzetu wa Tanga, bado tunaendelea na msako kwenye msitu huo uliopo mpakani lakini siwezi kujata majina yao kwa sasa wala kueleza wanatoka wapi au nia yao ni nini,” alisema.
Kamanda Marambo pia alikataa kutaja idadi ya majambia wala bunduki hadi watakapokamilisha uchunguzi na upelelezi wa suala hilo.
Hivyo aliwataka wananchi wenye mapenzi mema na Taifa lao, kuendelea kutoa ushirikiano kwa vyombo vya ulinzi na usalama ili kufichua watu wanaowatilia shaka wanapowakuta misituni na mitaani, ili hatua za haraka zichukuliwe.
Hii ni mara ya tatu kwa wanaoshukiwa na vitendo vya kigaidi kukamatwa mkoani Morogoro, ambapo hivi karibuni washukiwa wengine 25 walikamatwa kwa nyakati tofauti katika eneo la Kidatu wilayani Kilombero na wameshafikishwa mahakamani

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!