Friday, 26 June 2015

WANAFUNZI WAWILI WA MAFUNZO YA AWALI YA JKT WAFARIKI NA WENGINE 14 KUJERUHIWA KATIKA AJALI YA GARI


Wanafunzi wawili wa mafunzo ya awali wa Jeshi la Kujenga Taifa Kambi ya Chita mkoani Morogoro, wamefariki dunia na wengine 14 kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kupinduka eneo la mto Wami Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.


 
Wanafunzi hao walikuwa wakienda kambi ya Oldjoro mkoani Arusha kwa ajili ya kumalizia mafunzo yao  ya awali.
Marehemu hao wametajwa kuwa ni Edgar Kapunga na Adam Nassoro.
 
 Kwa mujibu wa taarifa ilitolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani jana, Jafar Ibrahim, ajali hiyo ilitokea juzi saa 12:00 jioni katika tarafa na kata ya Msata barabara ya Chalinze - Segera.
 
Kamanda Ibrahim alisema katika taarifa yake hiyo kuwa  wanafunzi hao walikuwa katika gari la kukodi lenye namba za usajili T510 Alu aina ya Scania likitokea Chita kwenda Oldjoro kumalizia mafunzo yao.
 
Alifafanua kuwa gari lililokuwa limewabeba askari hao wanafunzi, liliacha njia baada ya breki zake kufeli katika mteremko na kona za mto Wami na hivyo kupinduka.
 
Kamanda Ibrahim alisema majeruhi hao 14 wanaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali Kuu nya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Lugalo jijini Dar es Salaam.
 
Aidha, alisema dereva wa gari hilo alikimbia baada ya ajali hiyo na polisi wanaendelea kumtafuta huku miili ya marehemu ikiwa imehifadhiwa katika Hosipitali ya Lugalo.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!