Sunday, 21 June 2015

WAGOMBEA WANAOTUKAANGA KWA UMASKINI, TUWAKATAE

Makamu wa rais wa Tanzania Mheshimiwa Ghalib Bilali akionyesha fomu ya kugombea urais.

UMASKINI siyo chungwa kwamba ukilishika kila mtu atajua kwamba hili ni tunda fulani; hapana, ni zaidi ya hapo. Kila mgombea aliyetangaza nia na kuchukua fomu za kuwania urais mwaka huu hakuna ambaye hakuzungumzia tatizo hili, wote wamesema watauondoa.

Hoja yangu kwa wagombea wetu wa nafasi hii nyeti katika taifa letu ni je, wanasiasa hawa wanaujua umaskini wetu au wanatutia chumvi majeraha yetu kwa mtindo wa kutukejeli kupitia dhiki zetu ambazo kimsingi baadhi yao wamechangia kuzifanya ziwepo?
Waziri wa kilimo na chakula mheshimiwa Steven Wasira akichukua fomu yakugombea uraisi.
Maana najua kuwa umaskini siyo jiwe, kwamba atatokea shupavu mmoja siku moja na kuliinua kisha kulitupa mtoni na asubuhi wananchi tukaamka na kukuta kero hazipo na maisha ya furaha yametokea.  Ni mchakato unaohitaji akili ya mtu kujua aendako.
Uliza watu kadiri ujuavyo, wakuambie maana ya umaskini, wataishia kusema ni ukata, ufukara au hali ya mtu kukosa mali au kipato. Ni wachache watakaovuka uelewa huu, siyo wananchi wa kawaida tu, hata hao wanaotangaza nia ya urais wengi mawazo yao ni hayo!
Waziri wa ushirikiano wa kimataifa Mheshimiwa Benard Membe akionyesha fomu yake aliochukua ya  kugombea urais.
Nimewasikia baadhi wakijinasibu kuwa wanaufahamu umaskini kwa vitendo kwamba wameuishi kwa kukosa chakula, fedha na wakati mwingine walilala njaa walipokuwa wakitafuta elimu.  Kwao, kulala njaa ni umaskini, kuuza njugu, kupika mama-ntilie na kutembeza barafu mitanii.  Huo kwao ndiyo umaskini wanaotangaza kuuondoa na sisi bila kujihoji tunawapigia makofi.
Tangu lini umaskini limekuwa vazi kwamba kila mtu anayetaka kujisitiri maungo yake lazima alivae?  Kwenye ulimwengu huu wa sayansi unawezaje kulitafsiri tatizo hili kwa ulinganifu wa watu wote; nani aliyetuambia, aliyewaambia hao watangaza nia kuwa dhiki ni kitu kimoja?
Maana inashangaza sana kusikia mgombea anasimama kwenye jukwaa na kueleza kwamba kipaumbele chake cha kwanza ni kuondoa umaskini halafu kipaumbele cha pili anataja kuwa ni elimu kana kwamba tatizo la elimu siyo sehemu ya umaskini!  Hawajiulizi fedha bila elimu mtu atatajirikaje?
Dunia inaendelea, mambo yanabadilika, teknolojia inakua, upembuzi yakinifu juu ya uelewa wa dunia na shida zetu unavuka fahamu za miaka ya 1940, ajabu viongozi wetu bado wanawaza yaleyale waliyokuwa nayo wakati wanatafuta uhuru wa nchi yetu.
Rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Nyerere, alifikiri kuwa nchi yake ilikuwa na maadui watatu yaani Umaskini, Ujinga na Maradhi, akashindwa kabisa kujiongezea tafsiri kwamba maadui hao aliotangaza vita nao walikuwa kitu kimoja kilichogawanyika; ni kama mti wenye mizizi, shina na matawi.
Nchi zilizoendelea na zinazoendelea zimesogea mbele katika kuutafsiri umaskini na kubaini kuwa ni tatizo pacha; tafsiri yao juu ya neno hili siyo hali ya mtu kukosa noti mfukoni za kununua sembe, wanaamini maana sahihi ya umaskini ni;  Muunganiko wa Mambo Yanayosababisha Ukosefu wa Mahitaji Muhimu Katika Maisha ya Binadamu.
Cuba kwa mfano, baada ya mapinduzi Rais Fidel Castro wa nchi hiyo pamoja na hali duni ya wananchi wake, hakuuangalia umaskini kama tatizo la msingi, alitangaza mkakati wa kutokomeza njaa na kuimarisha afya ya watu wake, akiamini mambo hayo mawili yakiimarika yanaweza kuleta mapinduzi ya kweli ya uchumi wa nchi.
Hakuhangaika na wakosa fedha za kula, alijua uzalishaji unahitaji shibe na afya, alipofaulu hayo uchumi uliimarika; Cuba ya leo siyo ya kuchezea, Marekani pamoja na ubabe wake inajua uwezo wake.
Hoja hapa ni kwamba wanaojua kuwa umaskini ni mkusanyiko wa mambo yanayomzuia mtu kupata huduma muhimu ndiyo wanaoweza kuushinda.
Kwa tafsiri hiyo ukosefu wa elimu hauwezi kutofautishwa na umaskini, mahitaji ya ajira ni sehemu ya umaskini, maradhi, njaa vyote kwa orodha yake ni matawi yatokanayo na tatizo hili ambalo serikali imepambana nalo kwa miaka mingi lakini imefeli kuliangamiza.
Rais Nyerere angekuwepo angekiri hiki ninachoandika; alipojaribu kutenganisha mambo yanayochangia ukosefu wa upatikaji wa mahitaji muhimu kwa wananchi wake hakufanikiwa, alijikuta akipiga mbizi mahali alipopangua maji ili avuke, alipopita yalirejea kwa kasi.
Simsemei; lakini naamini wakati Nyerere anaanzisha vita dhidi ya ujinga kwa kufungua madarasa ya watu wazima (ngumbaru) alijua atapata ushindi, lakini leo tunashuhudia maprofesa wanakamatwa kwa ufisadi, wanabuni vitu vya kijinga sawa na watu wasiokuwa na elimu! Maana yake ni kwamba umaskini umezaa vitukuu vya adui zetu, sasa vita imekuwa nzito hakuna mfano wake, tunapigwa kila upande.
Tumefika mahali kama taifa tunapambana na tatizo la ajira kama sehemu ya vita ya umaskini wetu, mafisadi wanaajiri maelfu ya wafanyakazi hewa na wanawalipa mishahara inayoingia kweye matumbo yao. Tunajitutumua kuongeza mapato kwenye serikali kwa kuminyana kodi, wahujumu uchumi wanayafyonza.
Vipi tuamini kuwa umaskini ni ukosefu wa kipato ilhali kuna wanaopata fedha lakini hawaendelei?  Hakuna ubishi, tatizo hili limekuwa kubwa kama tembo, hatuwezi kuliondoa kwa kulimeza, tunahitaji akili mpya, mipango mipya na tafsiri mpya itakayoweza kutuchambulia umaskini wetu kwa mfumo wa hesabu.
Huo ndiyo msingi waliotakiwa kuujenga wasaka urais wetu, wasipofanya hivyo tuwapuuze! Maana huwezi kukana ukweli kwamba umaskini wa mwanafunzi aliyemaliza chuo kikuu na kupata shahada yake ya mambo ya kibenki ni ajira siyo kitu kingine; jambo hili linahitaji shule?
Hata ukiangalia wazo la Kilimo Kwanza lililofeli ambalo viongozi wa serikali waliamini lingeondoa umaskini kwa wananchi walio wengi vijijini wanaotegemea kilimo, halikufanyiwa utafiti. Kuna baadhi ya mikoa ambayo haihitaji mapinduzi ya kilimo kwa sababu wananchi wake walishayafanya, umaskini wao mkubwa kwa sasa ni soko, miundombinu ya kusafirishia mazao yao mpaka kwa wateja.
Hii ina maana kwamba, shida ya wakazi wa Mkoa wa Singida na Dodoma kwa mfano, huwezi kuilinganisha na ya wananchi wa Mbeya, Iringa, Katavi kwa maana ya jiografia ilivyo, hivyo wanaosema wataziondoa lazima waseme kwa mgawanyo siyo kwa jumla. 
Hoja yangu kwa wagombea hawa ni kwamba wanapozungumzia umaskini wanakuwa wamelenga jambo gani? Je, ni umaskini wa elimu au kitu kipi; maana wapo watu ambao wanamiliki ng’ombe 3,000, lakini wanalala kwenye ngozi,  unawezaje kuwaita maskini?
Hapo kuna suala la mchanganuo wa namna ya kukabiliana na hali duni, wanaposema wataondoa tatizo hili wanapaswa watuambie wanawajua wanaotaka kuwasaidia kwa idadi na makundi yao?
Waseme ni maskini wangapi wa ajira wanaotaka kuwaondolea kadhia hiyo, ni wakulima wangapi wanataka Kilimo Kwanza kwenye maeneo yao, ni kiasi gani ni wahitaji wa elimu, idadi gani wanakwazwa na miundombinu kupata huduma muhimu za jamii, yote yafanyike kwa namba kwa sababu ulimwengu wa leo hauhitaji mambo ya kubahatisha.
Miaka 50 tangu uhuru tumepigana vita ya umaskini gizani, hatujapata mafanikio, kila mbinu tuliyojaribu tumefeli. Serikali ya awamu ya nne ilisema kipaumbele chake katika kuondoa umaskini ni kuwawezesha wakulima; imeshindikana! Wakasema mikopo waliyoiita ‘Mabilioni ya Kikwete’  (rais), imepotea kusikojulikana. Aibu yao!
Tumeshindwa kupata tija kwa sababu wanaotuongoza hawaujui umaskini wetu, wanatudhihaki, wanacheza na hisia zetu kwa miaka nenda rudi, jambo hili halikubaliki! Hatuwezi kuwa na wanasiasa wanaotumia shida za watu kuingia ikulu kila mwaka na baada ya hapo hakuna kinachofanyika.
Wananchi tukatae kukaangwa kwa umaskini wetu na kuzipiga teke siasa nyepesi. Baada ya kuchuja haya kwenye chujio, naomba kutoa hoja.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!