Monday, 22 June 2015

WABUNGE WA VITI MAALUM WALALAMIKA KUDHARAULIWA



Baadhi ya wabunge wa Viti Maalum, wamelalamika kwamba wamekuwa wakidharauliwa na jamii kutokana na uteuzi wao.



 
Waliyatoa malalamiko hayo walipokuwa wakiingia kwenye semina ya uelewa wa mchakato wa uchaguzi mjini hapa jana.
 
Semina hiyo ipo chini ya uwezeshaji wabunge ambayo iliandaliwa na Bunge kwa ufadhili wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP).
 
Mbunge wa Viti Maalum (Cuf), Zahara Ali Hamad, alisema Katiba imetoa viti maalum kwa mkono mmoja, lakini imekataa kwa upande mwingine.
 
Alitoa mfano kwa sheria inayotaka waziri mkuu atokane na jimbo la uchaguzi wakati mawaziri wengine wanaweza kutokana na jimbo ama viti maalum.
 
Naye Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Taulida Nyimbo, alisema wanawake wa viti maalum wanadharauliwa na kutopendana.
“Siamini kuwa wanawake hatupendani, ukiweka mtu hauziki hawezi kupata hata kura za wanawake wenzake,” alisema.
 
Aidha, alisema viti maalum vimekuwa vikisumbua kwa sababu watu hawafahamu jinsi gani vinapatikana.
 
Mbunge wa Kilwa Kusini (CUF), Suleiman Bundara, alisema taabu kubwa ni wanawake wenyewe kutopendana.
 
Mwenyekiti wa semina hiyo, Anna Abdallah (pichani), alitaka vyama vikubwa vya siasa kuonyesha mfano kwa kuwapa wanawake vyeo katika vyama.
 
Hata hivyo, Mbunge wa Manyovu (CCM), Albert Ntabaliba, alisema ni vyema wanawake wakaanzisha vyama vyao vya siasa ili nafasi ya juu ziwe zao.
 
“Sijaona wanawake walioanzisha vyama vya siasa na sheria inaruhusu kufanya hivyo. Waanzishe ili wachukue nafasi zote za juu,” alisema.
 
Akijibu hoja za wabunge hao, Mkurugenzi wa Utetezi wa Kituo cha Haki za Binadamu Nchini (LHRC), Harold Sungusia, alisema ili kuondoa dharau kwa viti maalum, mambo ya msingi ya kuyafanya ni kuweka utaratibu muafaka utakaowekwa katika sheria wa jinsi ya kuwapata wabunge.
 
“Pia majukumu ya wabunge yajulikane kisheria ili wawajibike katika eneo hilo walilopangiwa,” alisema.
 
Aidha, alitaka elimu itolewe kwa umma ili waelewe upatikanaji wa wabunge hao na majukumu yao.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!