Askofu wa Kanisa la Anglikana Jimbo la Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa amesema kazi ya uandikishaji wa Daftari la Wapigakura liwe endelevu kwa sababu kila siku watu wenye sifa ya kuandikishwa wanaongezeka.
Dk Mokiwa aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa maandalizi ya maadhimisho ya miaka 50 ya kuanzishwa kwa Dayosisi ya Kanisa la Anglikana yatakayofanyika Julai 5, mwaka huu.
Alisema endapo Serikali itafanya kazi hiyo kuwa endelevu, itasaidia kunusuru uvunjifu wa ndoa kwa sababu kazi hiyo imeonekana kuwa moja ya sababu ya wanandoa kuchelewa kurudi nyumbani kwa sababu ya foleni ya kwenye vituo vya uandikishiaji.
Askofu huyo aliitaka Serikali iongeze mashine za BVR na kuzihakiki ubora wake kabla ya hazijaanza kutumika ili kupunguza kero inayotokea katika familia nyingi.
Akizungumzia Uchaguzi Mkuu ujao, Dk Mokiwa alisema sifa ya rais bora ni yule atakayeshughulikia matatizo sugu ya wananchi.
“Kwanza nawapongeza kila mmoja aliyetangaza nia ya kugombea urais, wote hawa wanazo sifa nawapenda sana, lakini natamani Rais ajaye aje na ajenda ya kuwakomboa Watanzania kutoka katika hali waliyonayo sasa ya umaskini uliokithiri,” alisema Dk Mokiwa.
Alisema anachukizwa na baadhi ya viongozi wanaokwenda nje ya nchi kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya zao wakati fedha zinazotumika kuwapeleka zingetosha kuwatafuta wataalamu wakaja kutibu wananchi wote.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment