Monday, 1 June 2015
SHILINGI MILION 800 ZAYEYUKA BANDARINI
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad, amebaini kuyeyuka kwa fedha za kodi Sh bilioni 835.974, katika mizigo iliyofika katika Bandari ya Dar es Salaam na kutakiwa kwenda katika nchi nyingine.
Kwa mujibu wa taarifa yake iliyotolewa bungeni wiki hii, ukaguzi wake katika mapitio ya mfumo wa kutunzia taarifa za forodha (Asycuda++), umebaini kuwa mizigo 6,316 iliyopaswa kufika katika Bandari ya Dar es Salaam kwa muda, haina ushahidi wa kuondolewa katika bandari hiyo.
Kwa kuwa hakuna ushahidi wa mizigo hiyo kuondoshwa kwenda katika nchi ilikokusudiwa, CAG amebainisha kuwa kama imeingizwa nchini, itakuwa imeikosesha Serikali kodi yenye thamani ya Sh bilioni 835.974.
“Mizigo hiyo iliyoingizwa kwa muda, ina kodi ya jumla ya Sh 835,974,894,995. Mali na mitambo mingine, inayoingizwa nchini kwa muda, inaweza kutumika nchini kinyume na matakwa ya sheria hivyo kuikosesha Serikali mapato,” alisema Profesa Assad.
Kutokana na hali hiyo, Profesa Assad ameishauri Serikali kwa kupitia Mamlaka ya MapatoTanzania (TRA), kufanya uchunguzi juu ya bidhaa na vifaa vilivyoingizwa kwa muda kwa lengo la kukusanya kiasi cha kodi husika.
“Pia nashauri Serikali iweke udhibiti imara, utakaowezesha kusimamia maingizo yote ya muda na utakaohakikisha kuwa bidhaa hizo hazitumiki hapa nchini,” ameshauri Profesa Assad.
Wizi misamaha ya kodi CAG pia katika ukaguzi wake, alibaini wizi unaofanyika katika misamaha hiyo na kunufaisha watu binafsi, ambao wamekuwa wakiagiza vitu binafsi ikiwemo magari na kuyapitisha kwa jina la kampuni na asasi zenye misamaha ya kodi na baadaye kuirejesha.
Kwa wamiliki binafsi. Moja ya ufisadi wa aina hiyo, umekutwa katika Kampuni ya Kiliwarrior Expedition Ltd yenye msamaha wa kodi, ambayo iliagiza magari 28 bila kulipa kodi.
Hata hivyo, wakaguzi walipofanya ziara katika eneo la mradi kukagua magari hayo, ilikuta magari mawili tu, moja likiwa na namba za usajili T 721 AFM na lingine namba ya usajili T 461 AUU, tena ikabainika yote mawili si miongoni mwa magari hayo 28 yaliyoingia bila kulipa kodi.
Wakaguzi hao walipowabana viongozi wa TRA mkoani Arusha, walitoa maelezo kuwa baadhi ya magari yaliyoingizwa, yalisajiliwa na kutumiwa na watu wasiostahili msamaha huo. “Mamlaka (TRA), iliweza kuzuia usajili wa leseni za magari matano ambapo ilifanikiwa kuokoa kodi ya Sh milioni 72.53.
“Hata hivyo, suala kuu ni kwa nini Mamlaka haikuweza kuzuia uandikishaji wa magari kwa watumiaji wasiokuwa waagizaji wa magari hayo. “Kwa maoni yetu, udhaifu katika mazingira ya mifumo ya udhibiti (Mfumo wa Usimamizi wa Misamaha ya Kodi) na njama ndio sababu za wafanyabiashara wasio waaminifu, kutumia vibaya misamaha ya kodi kwa manufaa yao binafsi na hivyo kudhoofisha malengo ya kiuchumi ya motisha wa misamaha hiyo,” alisema.
Ufisadi wa aina hiyo, pia umefanyika katika kampuni ya Kilimakyaro Mountain Lodge Limited, ambayo iliomba na kupewa msamaha wa kodi, ili ipanue nyumba za kulala wageni wilayani Karatu katika mkoa huo huo wa Arusha.
Kwa kutumia msamaha huo, kampuni hiyo ikaingiza magari matatu, moja aina ya BMW X5 iliyotumika namba T 647 BYB, lingine Toyota Land Cruiser Prado iliyotumika namba T 630 CBB na nyingine Hyundai Santa mpya namba T 680 CHX kwa ajili ya mradi huo.
“Ziara yetu katika eneo la mradi haikukuta magari husika na menejimenti ya kampuni ikaifahamisha timu ya ukaguzi kuwa kampuni hiyo iliingiza nchini gari mpya moja tu aina ya Hyundai Santa, ambayo wakati wa ziara ilikuwa jijini Dar es Salaam na kwamba menejimenti ya kampuni, haijui chochote kuhusu magari mengine mawili.
“Naishauri menejimenti ya Mamlaka ya Mapato (TRA), kuchunguza na kukusanya kodi ya magari yote mawili, kisha ifungue mashitaka kwa wahalifu waliohusika,” ameshauri Profesa Assad.
Msamaha moja mara mbili Katika ukaguzi huo, Profesa Assad pia amebaini kutolewa kwa nafuu maalumu ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) mara mbili, kwenye ankara moja katika kampuni ya Swala Oil and Gas (T) Limited.
Msamaha huo wa dola za Marekani 163,039 sawa na zaidi ya Sh milioni 300, ulitolewa mara mbili wakati wa ununuzi wa mradi wa 20 Seismic-Seismic Data Line, kwa kutumia ankara kifani moja yenye namba 478 iliyotolewa Septemba 30, 2013.
Kwa mujibu wa Profesa Assad, hali hiyo si ya kawaida hivyo “kiasi cha Dola za Marekani 163,039, kilichotolewa kwa kampuni hii kinatakiwa kurudishwa.
“Hivyo nashauri kwamba menejimenti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, ikusanye Dola za Marekani 163,039 ambazo zilitolewa kwa kampuni ya Swala Oil and Gas (T) Limited na kuhakikisha kuwepo kwa udhibiti stahiki utakaozuia jambo kama hili kujirudia,” alisema Profesa Assad.
Chanzo: Habari Leo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment