Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), limevifutia usajili vyuo vitatu na kuvishusha hadhi vyuo 16 kwa kushindwa kurekebisha kasoro zilizobainishwa na baraza hilo.
Baraza hilo pia limeviruhusu vyuo vingine sita kuendelea na usajili, 42 kuendelea na taratibu za ithibati huku kimoja kikizuiliwa kudahili wanafunzi kwa kuendesha mafunzo bila kusajiliwa.
Vyuo vilivyofutiwa usajili na kuzuiliwa kudahili wanafunzi wapya ni Dar es Salaam College Clinical Medicine, Ndatele School of Medical Laboratory Science na Institute for Information Technology, vyote vya jijini humo.
Baraza hilo pia limekizuia chuo cha Darmiki College of Educational Studies, kudahili wanafunzi kwa sababu ya kuanza kutoa mafunzo bila kusajiliwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Katibu Mtendaji wa Nacte, Dk. Adolf Rutayuga (pichani), alisema, baraza hilo limefikia hatua ya kuvifutia usajili vyuo hivyo kutokana na kukiuka taratibu na kuwa na mapungufu makubwa ya usajili na ithibati chini ya Sheria ya Bunge namba 129, kanuni za Baraza za usajili na ithibati za mwaka 2001.
“Kwa kutumia Sheria ya Bunge, sura namba 129 na Kanuni za Baraza za Usajili, Ithibati na Utambuzi za mwaka 2001, Februari 20 mwaka huu, Baraza lilitoa ‘notisi’ ya siku 30 kwa taasisi na vyuo vilivyokiuka taratibu na vyenye mapungufu makubwa ya usajili na ithibati. Notisi hii ililenga kuzipa taasisi na vyuo hivyo nafasi ya kujitetea na kufanya marekebisho yaliyobainishwa,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Rutayuga, baada ya kutolewa kwa notisi hiyo, taasisi na vyuo vingi ambavyo vilipewa maelekezo ya kufanya marekebisho, vilifanya hivyo lakini hadi kufikia Juni 24 mwaka huu, baadhi ya vyuo havikuchukua hatua yoyote.
Dk. Rutayuga pia alisema, vyuo 16 vimeshushwa hadhi, 42 vimeruhusiwa kuendelea na taratibu za ithibati huku sita vikiendelea na usajili.
Alitaja vyuo vilivyoshushwa hadhi kuwa ni Sura Technologies, Institute of Management and Information Technology, Techno-Brain, KCMC AMO Ophthamology School, KCMC AMO Anaesthesia School, KCMC AMO General School (Moshi) na AMO Training Centre (Tanga).
Vingine ni CATC (Songea), CATC (Sumbawanga), COTC Maswa, COTC (Musoma, Dental Therapists Training Centre, Ngudu School of Environmental Health Sciences, Ministry of Agriculture Training Institute cha Igurusi na Mbozi School of Nursing.
Vyuo vilivyoruhusiwa kuendelea na usajili ni Regional Aviation College, Zoom Polytechnic College, Gataraye Research and Training Centre, Modern Commercial Institute, Evin School of Management na Agape School of Management vyote vya jijini humo.
Baadhi ya vyuo vilivyoruhusiwa kuendelea na taratibu za ithibati ni Mabughai Community Development Technical Training, Kizimbani Agricultural Training Institute (Zanzibar), Civil Aviation Training Centre, Bandari College, Law School of Tanzania, Royal College of Tanzania, Morogoro School of Journalism naTaasisi ya Sanaa na Utamaduni.
Aliongeza kuwa, hadi sasa baraza hilo limesajili vyuo vya mafunzo 531, kuanzia ngazi ya cheti hadi shahada.
Aidha, aliwaasa wazazi na wanafunzi wanaotaka kupeleka watoto wao au kujiunga na vyuo vya mafunzo ambavyo havijasajiliwa na NACTE wala havikidhi vigezo vya ithibati.
No comments:
Post a Comment