Thursday, 25 June 2015

MUSWADA TATA WA HABARI WAONDOLEWA BUNGENI



Bunge limesikia maoni ya wadau ya kuuondoa Bungeni Muswada wa Sheria ya Haki ya Kupata Habari 2015 ambao ulitarajiwa kusomwa kwa mara ya pili Juni 27, mwaka huu.



Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, alithibitisha hayo jana kwenye viwanja vya Bunge alipozungumza na NIPASHE lililotaka kujua iwapo ushauri wa kamati umemfikia Spika na uamuzi juu ya suala hilo.
"Ushauri wa kamati umezingatiwa, Muswada umeondolewa Bungeni," alijibu Dk. Kashilillah.
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, akizungumza na NIPASHE, alisisitiza kuwa maoni ya wadau hayawezi kupuuzwa katika uandaaji wa Muswada wa Sheria ya Haki ya Kupata Habari, 2015.
"Hatutapuuza maoni ya wadau hasa yanayolenga kuboresha muswada husika. Utungaji wa sheria yoyote ni lazima uwe shirikishi, hivyo maoni ya wadau yamesikikizwa kama ilivyokuwa awali walishauri Muswada huo na ule wa Huduma kwa Vyombo vya Habari, usije kwa hati ya dharura, tulizingatia na uliondolewa," alibainisha.
Juni 22, mwaka huu, wadau mbalimbali wa habari waliokutana jijini Dar es Salaam, walipinga miswada hiyo kwa kile kinachoelezwa kuwa inakiuka sheria za kimataifa, Katiba ya nchi na kuwanyima haki raia kupata taarifa na kuua ndoto ya vijana wanaotarajia kunufaika na tasnia ya habari.
Wadau hao ni Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania ( Moat), Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jukwaa la Wahariri Tanzania (Tef), Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (Misa) Tawi la Tanzania na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu ( THRDC).
Mmiliki wa Kampuni ya New Habari Corperation, Rostam Aziz, alisema muswada huo ni mbaya kwani unazuia dhana nzima ya uwazi na ukweli hivyo kulirudisha taifa nyuma na kuitaka serikali kutopeleka bungeni hadi wadau wote wa tasnia ya habari watakapotoa maoni.
“Huu muswada ni mbaya…wala hakuna haja ya kuwa na ‘debate’ (mjadala). Tuisihi serikali isitishe kupeleka muswada huu bungeni maana ni mbaya na utazaa ‘bad laws’ (sheria mbaya),” alisema na kuongeza:
"Serikali isifanye haraka, muswada huu utaturudisha nyuma kama taifa. Usitishwe kupelekwa bungeni hadi pale wadau wote watakapotoa maoni yao,” alisema Rostam.
Akitangaza maazimio ya mkutano wa Moat na wadau, Mwenyekiti wa Moat, Dk. Reginald Mengi, alisema kupitishwa kwa muswada huo kutawanyima uhuru wa usambazaji wa habari kwa vyombo vinavyomilikiwa na watu binafsi, jambo ambalo ni kinyume cha Katiba ya nchi.
Dk. Mengi alieleza kushangazwa na utungwaji wa sheria hiyo ambayo kwa upande mmoja inatambua na kuheshimu misingi ya Katiba katika ibara ya 5 na upande mwingine ibara ya 18 ikikataza taarifa iliyotolewa chini ya ibara ya 5 (1) kwa umma na kutoa vitisho kwa atakayekiuka na kupatikana na hatia kufungwa jela kifungo cha miaka isiyopungua mitano.
Alitahadharisha kuwa muswada huo ukipitishwa, hakuna chombo cha habari cha binafsi kitakachokuwapo hivyo kuua ndoto za vijana waliokuwa wanatarajia kunufaika na tasnia hiyo.
“Muswada ukipitishwa, hakuna chombo chochote cha habari cha binafsi kitakachokuwapo, si redio wala TV (televisheni). Ikitekelezwa ndiyo mwisho wa vyombo binafsi.
MCT WAPINGA
Akizungumza na waandishi mjini Dodoma, Katibu Mtendaji wa MCT, Kajubi Mukajanga, alisema baraza hilo limetoa ombi hilo kwa sababu wadau wa habari hawakuwa na muda wa kutosha kutoa maoni yao baada ya kusomwa kwa mara ya kwanza wiki iliyopita.
THRDC: MUSWADA UNAMINYA HAKI
Mwakilishi wa THRDC, Mariagoreth Charles, amesema kipengele cha 18 kinakataza mpata taarifa kutosambaza taarifa na hivyo kuminya haki ya kutoa taarifa na kusambaza kwa maslahi ya umma.
JUKATA: UTUNGWAJI SHERIA NI LAZIMA USHIRIKISHE WADAU
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukata, Deus Kibamba, alisema katika muswada huo, ni vifungu viwili pekee vyenye unafuu na iwapo utapita, waandishi wengi watafungwa jela kwa makosa mbalimbali ya kuhabarisha umma.
"Msingi wa kutunga sheria ni kushirikisha wadau wote. Badala ya kuwa muswada wa kuwezesha upatikanaji huru wa habari kwa wananchi, umekuwa wa kubana taarifa na kuleta vitisho kwa wanaosaka na kusambaza taarifa.
Mwandishi anaweza kwenda jela miaka 15 kwa kufanya kitu ambacho sisi tunaona siyo kosa na hakuna mbadala wa faini," alisema.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!