Serikali imeanzisha mfumo mpya wa maombi ya kazi kwa njia ya mtandao, utakao anza Julai mosi mwaka huu, ili kuondokana na dhana ya upendeleo, ucheleweshwaji na uwazi katika uombaji wa kazi, kwenye Sekretarieti ya Ajira, Utumishi wa Umma.
Aidha, mfumo huo utamuwezesha muombaji kupata majibu yake kupitia kompyuta na simu ya mkononi.
Hayo aliyasema jijini Dar es Salaam jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi), Celina Kombani kwenye uzinduzi wa baraza la wafanyakazi wa ofisi hiyo. Alisema mfumo huo utaondoa changamoto mbalimbali ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kwenye taasisi hiyo.
Alisema mfumo huo utasaidia pia upungufu wa rasilimali fedha pamoja na mrundikano wa mafaili katika ofisi hizo.
“Nikiwa kama waziri mwenye dhamana ninaelewa pia kuwa ili kuondokana na dhana za upendeleo, ucheleweshwaji wa majibu na uwazi nimebuni njia na kuanzisha mfumo huu mpya wa maombi kwa njia ya mtandao utakaoanza Julai mosi mwaka huu ambao utamsaidia muombaji wa kazi kupata majibu haraka,”alisema.
Aliongeza kuwa ubunifu huu mpya sio tu utaleta mapinduzi kwenye eneo la ajira, bali pia utaongeza ufanisi wa utendaji kazi katika taasisi yenu na serikali kwa ujumla.
Pia aliwataka kufuata taratibu na sheria zinazotakiwa wakati wa kuajiri ili kupunguza manunguniko ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara kwenye taasisi hiyo, maana msipofanya hivyo mtaingia kwenye migogoro isiyokuwa na maana.
Naye Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Xavier Daudi, alisema kwa kipindi cha miaka mitano taasisi hiyo imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo udanganyifu wa sifa kwa waombaji wa kazi pamoja na ukosefu wa rasilimali fedha ambao umekuwa ukipeleka ucheleweshwaji wa majibu kwa waombaji wa kazi.













No comments:
Post a Comment