Tuesday, 9 June 2015

JK: SINA MGOMBEA URAIS

Rais Jakaya Kikwete
LICHA ya idadi kubwa ya makada wa CCM waliojitokeza na wanaoendelea kujitokeza kuomba ridhaa ya kuteuliwa kuwania urais kupitia chama hicho tawala, Rais Jakaya Kikwete anayemaliza muda wake amesema hana mgombea, hivyo asihusishwe nao.


Amesema baadhi wamekuwa wakiomba ridhaa yake, lakini hakuna aliyemkatisha tamaa huku akimtakia kila la heri anayejiona ana ubavu wa kutaka kumrithi baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Aidha, amesisitiza ana imani na chama anachokiongoza, kitafanya chaguo sahihi na mgombea wa urais atakayepeperusha vyema bendera ya CCM katika mchakato wa kumpata Rais wa Awamu ya Tano wa Tanzania baadaye mwaka huu.
Rais Kikwete alisema hayo juzi usiku katika mkutano wake na Jumuiya ya Watanzania waishio Uholanzi, uliofanyika katika hoteli ya Crownie Plaza mjini hapa.
Alisema hayo alipokuwa anaelezea hali ya kisiasa nchini na pia maandalizi yanayoendelea ya uchaguzi mkuu ujao na pia mchakato wa Kura za Maoni ya Katiba Inayopendekezwa.
Hana mgombea
Akizungumzia mbio za urais zinazoendelea kushika kasi, alisema hali ya kisiasa ya Tanzania ni shwari, licha ya kuwa kumekuwa na kishindo katika kuwania kumrithi.
“Nyumbani hali ni shwari, lakini kwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi kuna mengi yanayoendelea, hasa mchakato wa kuwania Urais… huko CCM mpaka leo (juzi) watu 15 walishachukua fomu, na wengine zaidi ya 15 ama wametangaza nia au wanakusudia kufanya hivyo. “Ndiyo demokrasia ndani ya CCM, lakini niwahakikishie acheni waumane, lakini mimi binafsi sina chaguo langu. Chama ndicho kitakachoamua na ninaamini kitatupatia kiongozi sahihi kwa saizi na hadhi ya CCM na huyu atatuvusha mpaka Ikulu,” alisema.
Aidha, alisema wapo wanaojipitisha kwake wakiomba kuungwa mkono, lakini pamoja na hayo, akasisitiza hana mgombea. “Jana (Jumapili), kuna mtu alinitumia ujumbe akisema anakusudia kutia nia hivyo nimpe baraka zangu…nikamwambia `Goodluck’ (Kila la heri), sasa kama alitafsiri ndiyo tayari mambo safi, aah…sijui bwana, ila mimi sina mgombea. “Nasisitiza chama chetu ni makini na kitatupatia mgombea makini. Mwenyezi Mungu atuepushie mbali ili tusipate kiongozi atakayeipeleka nchi pabaya,” alisema na kuwataka Watanzania hao kutokuwa na hofu juu ya mchakato huo ndani ya CCM.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!