Saturday, 27 June 2015

HABARI ZAIDI JUU YA MAJAMBAZI YALIOUA POLISI NA KUCHOTA MAMILIONI BENKI YA NMB MKURANGA



Mkuranga. Majambazi watatu, wakiwa na silaha aina ya SMG, jana asubuhi waliua askari mmoja na kujeruhi watu wengine wawili na baadaye kupora bunduki na mamilioni ya fedha kwenye benki ya NMB, Tawi la Mkuranga  mkoani hapa.

Tukio hilo lilitokea muda mfupi baada ya gari kuwasili na makasha ya fedha, huku shughuli za utoaji huduma kwenye tawi hilo zikiendelea.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Pwani, Jafar Ibrahimu alisema kuwa bado hajafahamu kiasi halisi cha fedha zilizoporwa kwani alikuwa hajafika eneo la tukio.
Hata hivyo alisema askari aliyeuawa hakuwa mmoja wa polisi waliokuwa lindo kwenye tawi hilo la NMB, bali alikuwa anapita kuelekea kazini ndipo akakumbana na tukio hilo
Kamanda Ibrahim alibainisha kuwa taarifa ya awali aliyonayo ni kwamba katika tukio hilo hakuna silaha wala risasi iliyoporwa na majambazi hayo.
“Ndio ninakwenda eneo la tukio, kwani awali ninaweza kusema kweli tukio la ujambazi limetokea hapo NMB na nimeelezwa kuna askari kauawa, lakini si mmoja wa wale waliokuwapo lindoni,” alisema Kamanda Ibrahim.
“Lakini pia hakuna silaha iliyoporwa, zilizochukuliwa ni fedha ambazo bado haijafahamia ni kiasi gani na ziliporwa zikiwa tayari zimefikishwa ndani ya ofisi hiyo. Askari waliokuwa wamezisindikiza siyo polisi wetu bali ni wa kampuni binafsi,” alisema Kamanda Ibrahim.
Alisema kwa sasa, polisi wa  Wilaya ya Mkuranga, Rufiji na Dar es Salaam wapo katika msako mkali kuwasaka watu waliohusika katika tukio hilo la ujambazi.
Akizungumzia tukio hilo, mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Abdalah Kihato alisema majambazi hao waliokuwa watatu walivamia benki wakati wafanyakazi wa benki hiyo wakiwa katika maandalizi ya kupokea fedha hizo.
“Inaonekana majambazi hao walikuwa na taarifa za ujio wa fedha hizo kwenye benki hiyo,” alisema.
Alisema polisi mmoja ameuawa kwa kupigwa risasi, na kwa mujibu wa Kihato, polisi huyo alikuwa akijiandaa kuingia kazini jana mchana, huku askari wawili waliokuwa zamu kituoni hapo  wakijeruhiwa kwa risasi.
Mwingine aliyejeruhiwa ni mtumishi mmoja wa benki hiyo ambaye alipigwa panga. Wote wamehamishwa Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga kwa matibabu.
Alisema baada ya tukio hilo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ilikutana kwa dharura kulijadili kwa kina na kwamba kwa sasa polisi pamoja na timu ya ulinzi na usalama ya wilaya iko kazini kutafuta taarifa zaidi za tukio hilo.
 Alipoulizwa iwapo uporaji wa fedha hizo ulifanikiwa kutokana na uzembe, Kihato alisema kuwa uchunguzi wa polisi unaendelea.
Kihato aliwaomba wananchi wa Mkuranga na wale wa jiji la Dar es Salaam kutoa ushirikiano kwa polisi ili kufanikisha kukamatwa kwa wezi hao ambao alisema wameonyesha unyama wa hali ya juu.
 Hata hivyo, chanzo cha habari kilidai kuwa polisi aliyeuawa alipigwa risasi wakati akitoka ndani ya benki ambamo alikwenda kupata huduma.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, majambazi watatu kati yatisa walifika hapo wakiwa kwenye pikipiki na walshuka na kuelekea kwenye mlango wa kuingilia ndani na kuingia kama wateja wengine.
Dakika kadhaa baada ya watu hao watatu kuingia ndani, walitoa silaha na kuwataka wote waliokuwamo ndani kusikiliza maelekezo na kwamba ambaye angekaidi angefumuliwa ubongo.
Mashuhuda hao walidai kuwa wateja walitii amri hiyo na ghafla ulisikika mlio wa risasi nje ya benki hiyo kisha mmoja wa majambazi alitoka na sanduku lililokuwa na fedha na akalipasua nje ya benki na kutoa fedha na kuziingiza kwenye mifuko mikubwa ya plastiki na kuondoka nazo kwa pikipiki waliokuja nayo.
Mlio ule wa risasi iliyosikika nje ya benki inadaiwa ilitoka kwa mmoja wa majambazi wengine ambao wao walikuja na gari dogo na kugawanyika wao wakabaki kufuatilia nyenendo za polisi waliokuwa zamu eneo hilo na askari wawili wa kampuni binafsi waliokuwa wamesindkiza fedha hizo zilipokuwa zimeshushwa kutoka kwenye gari na kuingizwa ndani ya ofisi. Imeelezwa kuwa majambazi hao waliokuwa nje askari aliyekuwa amevaa kiraia akiingia benki na akawa anafanya mawasiliano fulani, kitendo ambacho walihisi anatoa taarifa kwa wenzake na hivyo wakaamua kumuwahi kwa risasi ya kichwani.
Juni 11 mwaka huu, majambazi walivamia kituo cha polisi cha Mkuranga wakiwa na mapanga na kuua askari mmoja na kisha kupora bunduki mbili.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!