Wednesday 13 May 2015

WAZEE WAPATIWA VITAMBULISHO VYA MATIBABU BURE MKOA WA PWANI



Mji wa Kibaha mkoani Pwani, umegawa vitambulisho maalum vya matibabu kwa wazee wenye umri wa kuanzia  miaka 60 na kuendelea vitakavyowawezesha kupatiwa  matibabu bure.


Ugawaji wa vitambulisho hivyo ulizinduliwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Jeniffer Omolo, mjini hapa jana.
Hatua hiyo inafuatia siku chache baada ya serikali kutoa agizo kwa halmashauri  zote nchini kuwatambua wazee wastaafu hususan wenye umri wa kuanzia miaka 60 na kuendelea na kuwapa vitambulisho vitakavyowafanya watibiwe bure ikiwa ni njia sahihi ya kutambua juhudi zao za kulitumikia taifa wakiwa na nguvu.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Dk. Issessanda Kaniki, alisema uorodheshaji wa wazee wote kwa kupita nyumba kwa nyumba ulifanyika kwa kusaidiana na Kitengo cha Ustawi wa Jamii na Good Samaritan ‘Help Age’ International ambapo jumla ya wazee 4,672 waliandikishwa.
Aidha, Dk. Kaniki aliongeza kuwa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012, inaonyesha kuwa Halmashauri ya Mji Kibaha ina wazee 5,111.
"Hivyo baada uzinduzi  huu wa leo (jana), ofisi yangu itapita tena kwenye mitaa yote 73 kuwahamisisha wazee ambao hawakupiga picha za vitambulisho wapige ili wapate vitambulisho vya matibabu bure," alisema.
Aidha, Omolo aliyemwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, aliwataka watumishi wa Idara ya Afya kuzingatia maadili ya kazi yao na kuwahudumia wazee hao kikamilifu. 
Pia aliwataka kuandaa madirisha maalum kwa ajili yao na kwamba hatarajii kusikia manung’uniko na malalamiko kutoka kwa wazee hao. 
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na Huduma za Jamii Mheshimiwa Tuaje Ponza, aliwataka wazee nchini kutambua juhudi za Serikali kuwajali na  kuwa wao ni watu muhimu kwani maendeleo yaliyopo leo wameyachangia kwa kiasi kikubwa na wao.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wazee wenzake, Eleuter Kigodi, alisema wamefarijika mno kuona serikali inatambua utumishi na uzalendo wao kwa nchi yao na kuahidi kuunga mkono juhudi zozote za serikali.
Halmashauri ya Mji wa Kibaha kwa kutumia fedha ya mapato yake ya ndani, ilitenga Sh. 11,650,000.00 zilizotumika kutengeneza vitambulisho 4,672 kwa ajili ya wazee.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!