Thursday, 21 May 2015

WAKIMBIZI WA BURUNDI WANAHITAJI MSAADA ZAIDI WA DAWA NA CHAKULA


Kuna taarifa za kuhuzunisha kuhusiana na tishio la kiafya linalowakabili maelfu ya wakimbizi wa Burundi wanaoingia nchini kila uchao kukimbia machafuko ya kisiasa nchini mwao. 


Inaelezwa kuwa mrundikano wa wakimbizi hao katika eneo la Kagunga mkoani Kigoma umesababisha kuwapo kwa kipindupindu na magonjwa mengine ya mlipuko. Hadi kufikia juzi, wakimbizi 20 walishafariki dunia kutokana na matatizo hayo, 12 kati yao wakithibitika kuwa vifo vyao vimetokana na kipindupindu. Wapo wakimbizi wengine zaidi ya 2,000 wanaendelea kuugua kipindupindu na magonjwa mengine yanayohusiana na uchafuzi wa mazingira. 
Inaelezwa kuwa maafa hayo, kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakisababishwa na idadi kubwa ya wakimbizi wasioendana na rasilimali zilizopo katika kuwahudumia kwenye eneo hilo la mpaka unaotenganisha nchi yao na Tanzania. Kwamba, eneo la Kijiji cha Lusolo katika kitongoji hicho cha Kagunga ni dogo. 
Ni hili ndilo hutumiwa zaidi na wakimbizi kuingia nchini na kupewa hifadhi ya muda kabla ya kupelekwa katika kambi rasmi ya Nyarugusu iliyopo wilayani Kasulu mkoani humo. Kwa kawaida, eneo hilo hukaliwa na wakazi wake takriban 2,000 tu. Hata hivyo, kufikia juzi, tayari lilishapokea wakimbizi 120,000 na wengi wamebaki hapo wakisubiri kupelekwa Kigoma na baadaye Nyarugusu. 
Kadhalika, inaelezwa kuwa uwezo wa meli inayowasafirisha kutoka walipo sasa ni kubeba watu 600 tu. Na meli hii hutumia wastani wa masaa manane kutoka Kagunga kwenda Kigoma na kurudi ili kuanza safari nyingine. Kwa sababu hiyo, ni dhahiri kuwa bado kuna changamoto kubwa katika kuwahamisha wakimbizi kutoka Kagunga kwa kasi inayotarajiwa.
Kutokana na tatizo hilo, ndipo sasa maelfu ya wakimbizi wamejikuta wakinasa katika eneo hilo dogo la Kagunga, wakikabiliwa na wakati mgumu katika kunusuru maisha yao. Ni kwa sababu hadi sasa, Kagunga hakuna chakula cha kutosha kwa ajili ya maelfu ya wakimbizi hao. 
Wala hakuna huduma nyingine muhimu kama maji safi na salama, na pia huduma za afya. Kuna tatizo kubwa vilevile la uchafuzi wa mazingira. Ikumbukwe kuwa eneo hilo halina vyoo vya kutosha kwa ajili ya kuwahudumia wakimbizi. Matokeo yake, wakimbizi hujisaidia hovyo na kusababisha kuwapo kwa tishio kubwa zaidi la kuwapo kwa mlipuko wa magonjwa, kama kipindupindu ambacho tayari kimeshatua na kuwaua baadhi yao.
Ni katika mazingira kama hayo, ndipo NIPASHE tunapoona kuwa sasa kuna kila sababu kwa jumuiya ya kimataifa kuingilia kati na kushirikiana kwa karibu zaidi na serikali ya Tanzania katika kuwaokoa wakimbizi hawa. Na hatua mojawapo ya haraka inayopaswa kuchukuliwa ni pamoja na kuongeza kasi ya kuwaondosha wakimbizi waliopo Kagunga ili wapelekwe Nyarugusu na kwingineko kunakopatikana huduma muhimu za kibinadamu kwa ajili yao. 
Hatua nyingine muhimu na inayopaswa kuchukuliwa haraka zaidi ni kuwapelekea huduma muhimu wakimbizi walioko Kagunga. Itafutwe namna ya kuwapatia huduma ya choo, maji, chakula na dawa. Wataalam wa afya wawezeshwe kufika eneo hilo ili kusaidiana na mashirika mengine ya hiari kwa nia ya kuwahudumia wagonjwa.
Sisi tunashauri yote haya huku tukijua kuwa kazi hii siyo ndogo, ina changamoto nyingi. Hivyo, hatua hizi zinapaswa kuchukuliwa haraka iwezekanavyo. Vinginevyo, wala haitashangaza kuona kuwa mlipuko huu wa kipindupindu na magonjwa mengine ya kuhara ukiongezeka kwa kasi zaidi na kusababisha maafa makubwa kwa wakimbizi hawa wa Burundi. Na hili halipaswi kutokea.
 Vifo vya watu hawa wasio na hatia, na ambao walijitahidi kadri walivyoweza kukimbilia nchini kwa nia ya kujinusuru maisha yao, vitakuwa ni pigo kubwa kwa wanaothamini haki ya kuishi aliyo nayo kila binadamu. Isitoshe, kama vifo vya kipindupindu na maradhi mengine vitaachwa viendelee kuua maelfu ya wakimbizi hawa wa Burundi, itakuwa ni fedheha kubwa kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Afrika na jumuiya yote ya kimataifa. 
Shime, wakati mazungumzo ya amani yakiendelea, wakimbizi wa Burundi wasaidiwe haraka chakula, maji na dawa ili kuwanusuru na tishio la maafa yatokanayo na magonjwa ya mlipuko. 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!