Friday, 1 May 2015

RAIS KIKWETE KUAGA WAFANYAKAZI LEO

Rais Jakaya Kikwete,  leo, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye kilele cha maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), huku Mkoa wa Mwanza ukiahidi kumuenzi na kukumbuka mchango wake katika utumishi wake wa miaka 10 katika uongozi wake.

Rais Kikwete anatarajia kustaafu mwaka huu baada ya kuwatumikia Watanzania, kwa miaka 10, na sherehe za leo zitakuwa za mwisho kwake akiwa kiongozi mkuu wa nchi.
Akifungua maonyesho ya Mei Mosi yanayofikia kilele chake leo kwenye Viwanja vya Furahisha katika Manispaa ya Ilemela juzi jioni, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo alisema maandalizi yameshakamilika na amewataka wakazi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi.
Mulongo alisema Mwanza imepewa heshima kubwa ya kuandaa sherehe hizo, kwani wakati Rais Kikwete anaingia madarakani, sherehe zake za kwanza za Mei Mosi zilifanyika mkoani humo.
“Serikali ya mkoa tutatumia fursa hii ya maadhimisho ya Mei Mosi vizuri, kwani tunatambua Rais Kikwete anatarajia kustaafu na ameifanyia mambo makubwa Mwanza. Tutamuenzi na kumkumbuka kupitia sherehe hizi,” alisema Mulongo.
Aliwataka waajiri wote mkoani humo na wa maeneo ya jirani, kuwaruhusu wafanyakazi wao kushiriki sherehe hizo kwa kuwa ni muhimu kwao.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) Mkoa wa Mwanza, Yusuf Simbaulanga alisema sherehe hizo zitatumika pia kumuaga Rais Kikwete na kuwakumbusha wafanyakazi wote kuona umuhimu wa kura zao katika kufanya uamuzi sahihi wakati wa Uchaguzi Mkuu na kujitokeza kujiandikisha kwenye Daftari la Kupiga kura.
Pia, Simbaulanga alisema wafanyakazi watatumia nafasi hiyo kutaka kujua utekelezaji wa ahadi za Rais Kikwete alizotoa kwao tangu alipoingia madarakani.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!