Friday 29 May 2015

MALORI YA TANZANIA YASABABISHA AJALI 227 NCHINI ZAMBIA


Wakati Serikali na wadau wa usafiri wakiendelea kutafuta mwarobaini wa ajali nchini, imeelezwa kuwa malori ya Tanzania yamesababisha ajali 227 nchini Zambia kati ya Januari na Mei.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa kwenye Gazeti la Lusaka Times la Zambia, imeelezwa kuwa Tanzania inatakiwa kutafuta suluhisho la kudumu la kudhibiti ajali zinazosababishwa na malori ya Tanzania wanayokwenda nchini humo.
Likikariri ripoti iliyotolewa na Kikosi cha Usalama Barabarani cha Zambia mwezi huu, gazeti hilo limesema katika ajali hizo 227, ajali 37 zilipoteza maisha ya watu 42.
“Kati ya ajali hizo waliopata majeraha makubwa walikuwa 51, wenye majeraha madogo walikuwa 59 huku ajali 133 zilisababisha uharibifu wa magari na mali,” inasema ripoti hiyo.
Ripoti hiyo ilitaja sababu kubwa ya ajali hizo kuwa ni mwendo kasi, vizuizi barabarani, uchovu wa safari ambao umekuwa ukisababisha baadhi ya madereva kuegesha malori yao vibaya na kusababisha madhara kwa watumiaji wengine wa barabara.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usafirishaji na Usalama Barabarani (RTSA) Zambia, Zindaba Soko akizungumza katika mkutano uliomkutanisha na Mkurugenzi wa Usafirishaji kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini Tanzania (Sumatra), Leo Ngowi mjini Ndola Zambia, alisema Serikali ya nchi hiyo itaondoa vikwazo barabarani ambavyo vimekuwa vikisababisha ajali.
Mkurugenzi huyo alisema iwapo nchi za Kusini mwa Afrika zitatekeleza utaratibu wa kuondoa urasimu utasaidia kupunguza muda wa kukaa mipakani, kupunguza gharama za kufanya biashara na kufanya safari nyingi kuliko ilivyo sasa kama pia watazingatia sheria za usalama barabarani.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Johansen Kahatano kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani akizungumzia suala hilo alisema Polisi ilituma mwakilishi katika mkutano huo nchini Zambia ambapo walipata taarifa za ajali hizo.
Kahatano alisema Serikali ilipendekeza madereva wenye leseni daraja E wasome kila wanapotaka kupata daraja C, pia madereva wote wakasome kila baada ya miaka mitatu, lakini suala halikuwezekana baada ya kupingwa na madereva.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!