Machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini Burundi, yamesababisha mamia ya raia wa nchi hiyo kukimbilia Tanzania kama wakimbizi.
Raia hao walianza kuingia nchini jana kwa ajili ya kutafuta hifadhi mkoani Kigoma.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ilithibitisha kuingia kwa wakimbizi zaidi ya 200. Msemaji wa wizara hiyo, Isaack Nantanga, aliliambia NIPASHE kuwa wakimbizi hao waliingia mkoani Kigoma kupitia vijiji vya Kagunga, Kakonko, Kijaje na Chakeoya.
Nantanga alisema kuwa baada ya wakimbizi yao kuingia katika maeneo hayo, maofisa wa Idara ya Uhamiaji walikuwa wanaendelea na taratibu za kawaida za kuwapokea wakimbizi.
Hata hivyo, mwandishi wa NIPASHE alipofika katika eneo la mpaka wa Tanzania na Burundi, Manyovu na kuzungumza na maofisa mbalimbali wa Serikali, walimthibitishia kwamba kuna wakimbizi walioingia mkoani Kigoma na wengine wanaendelea kuingia.
Mmoja wa maofisa Uhamiaji ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa maelezo kuwa siyo msemaji, alisema kuwa wakimbizi 150 kutoka Burundi waliingia mkoani humo na walikuwa katika kijiji cha Kagunga, wilaya ya Kigoma Vijijini.
Alisema kuwa maofisa wa Idara ya Uhamiaji waliondoka jana kwenda Kagunga kuwachukua wakimbizi hao kwa boti na kuwapeleka katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu kwa ajili ya kuwahifadhi.
Alisema kuwa watakaa kambini hapo hadi hali ya utulivu itakaporejea nchini Burundi.
Awali kabla ya kuthibitisha taarifa kuwa kuna kundi la wakimbizi waliokuwa wameingia nchini kutoka Burundi, Nantanga aliliambia gazeti hili kuwa serikali ilikuwa imeimarisha ulinzi na usalama katika maeneo ya mipakani katika mikoa ya Kigoma na Kagera kufuatia hofu ya baadhi ya wakazi wa mikoa hiyo kwamba kuna wakimbizi kutoka Burundi ambao wataingia nchini bila kufuata taratibu.
Nantanga alisema pamoja na kuwapo taarifa kuwa kuna baadhi ya wakimbizi katika maeneo ya mipakani, hakuna taarifa ya wakimbizi walioingia na watakaoingia nchini bila kibali.
“Hali ni shwari katika maeneo ya mpakani na hakuna matatizo wala tukio la mkimbizi au wakimbizi kuingia nchini bila kufuata taratibu, inawezekana wakawapo wawili au mmoja ambao wamepita njia za porini kwa kuwa kuna mapori,” alisema Nantanga. Alisema iwapo kuna wakimbizi ambao wataingia nchini, vipo vituo maalum ambavyo ni kwa ajili ya kupitia wakimbizi.
MACHAFUKO BURUNDI
Burundi imekumbwa na ghasia kutokana na maandamano yanayofanyika katika mji mkuu, Bujumbura na wafuasi wa vyama vya upinzani wanaopinga hatua ya Rais wa nchi hiyo, Pierre Nkurunziza, kutaka kugombea tena urais, baada ya kumaliza muda wake wa mihula miwili.
Katiba ya Burundi inatajwa muda wa urais kuwa vipindi viwili, lakini Rais Nkurunziza anasema kwa mujibu wa makubaliano ya mkataba wa Arusha, kipindi chake kinaanza pale mkataba wa Arusha uliposainiwa, hivyo muda aliokuwa madarakani kabla ya kusainiwa usihesabike.
Anasema kuwa hiki kitakuwa kipindi chake cha pili na cha mwisho.
Hata hivyo, upinzani unapinga na yamekuwapo maandamano kuanzia Jumamosi ya kupinga hatua hiyo na tayari watu kadhaa wametiwa nguvuni na baadhi wanadaiwa kupoteza maisha
No comments:
Post a Comment