RAIS Jakaya Kikwete leo anaongoza waombolezaji, wakiwemo viongozi mbalimbali wa nchi za Kusini mwa Afrika, katika maziko ya Brigedia Jenerali mstaafu, Hashim Mbita yatakayofanyika jijini Dar es Salaam.
Viongozi hao wa nje wameanza kuwasili nchini tangu jana, ambapo watashiriki katika maziko yanayofanyika katika makaburi ya Kisutu.
Akizungumza juzi msibani hapo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe alisema wameshapokea uthibitisho wa ushiriki wa Waziri wa Mambo ya Nje na wakuu wa majeshi wa Namibia, maofisa wa juu wa Jeshi la Zimbabwe na viongozi wengine.
“Nadhani atakayeongoza ni Mheshimiwa Rais na ndiyo sababu ya haya mazishi kufanyika siku ya Jumatano kwa sababu kesho (jana) amebanwa na kazi nyingi na ndiyo sababu ya kuomba,” alisema Membe.
Aidha, alisema, wageni wengine ni wajumbe wa Kamati Kuu ya chama tawala cha Msumbiji cha Frelimo na wajumbe wa nchi za Zambia, Afrika Kusini na Umoja wa Afrika (AU).
Akimzungumzia Mbita, Membe alisema atakumbukwa kama mkombozi wa nchi nyingi za Afrika hasa za Kusini, hali iliyomjengea umaarufu kwa kuwa katika miaka ya 1990 nchi zote za Afrika zilikuwa huru, isipokuwa Afrika Magharibi.
Alisema jambo la faraja ni kwamba Brigedia Mbita ameacha matoleo nane ya vitabu vinavyozungumzia masuala ya ukombozi wa nchi za Afrika, ambavyo vitaendelea kuweka historia yake kwa vizazi vijavyo.
“Ni mtu mwenye heshima kubwa sana, na ndiyo sababu yeye kutunukiwa tuzo ya Monomotapa ya Msumbiji ambayo ni kubwa sana, hapa Tanzania alipata yeye na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere,” alisema.
Alisema, wizara yake itaanza kuchapisha makala za Brigedia Mbita ili jamii na vizazi vijavyo viweze kumfahamu shujaa huyo. Kwa upande wake, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alisema kila Mtanzania anapaswa kumtambua Brigedia Mbita, kutokana na mchango wake katika ukombozi wa nchi nyingi.
“Ni mtu ambaye Mungu amemwezesha kutimiza mambo magumu ambayo wengine hawawezi kuyatimiza, ametuachia funzo kubwa sana juu ya kuwa wazalendo na nchi zetu,” alisema Zitto.
Zitto alishauri Barabara ya Kilwa iitwe jina la Mbita, ikiwa ni hatua ya kuendelea kumuenzi kwa kuwa inaelekea nchi ambazo alishiriki ukombozi wake.
Brigedia Mbita alifariki Jumapili katika Hospitali ya Jeshi ya Lugalo, alikokuwa amelazwa kwa matibabu bada ya kuugua kwa muda mrefu.
Wasifu Kwa mujibu wa wasifu uliotolewa na Kurugenzi ya Habari na Mahusiano Makao Makuu ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Dar es Salaam, Mbita alizaliwa Novemba 2, 1933 katika mtaa wa Songoro, kata ya Gongoni, wilaya ya Tabora Mjini.
Mwanasiasa huyu mkongwe aliyeacha mke na watoto, mwili wake unaagwa katika Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo kabla ya maziko kufanyika makaburi ya Kisutu
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment