Dar es Salaam. Vikundi vya uhalifu nchini vyenye muundo ‘Panya Road’ vinazidi kuwapa hofu wananchi kutokana na vitendo vyao vya kutishia amani, utafiti wa Taasisi ya kiraia ya Twaweza umebainisha.
Matokeo ya utafiti huo yaliyotolewa jana, yalibainisha kuwa watu wanane kati ya 10 (asilimia 84) wanaamini kuna uwezekano mkubwa wa kuathiriwa na vijana wahalifu.
Utafiti huo unaoitwa ‘Je, tuko Salama?’ ulieleza kuwa wananchi watatu kati ya 10 wameshakumbana na wizi ndani ya kipindi cha mwaka jana, sawa na nusu ya Watanzania wote.
Takwimu za utafiti huo zilikusanywa kwa kuwahoji watu 1,401 kutoka Bara kati ya Februari na Machi mwaka huu.
Katika utafiti huo, wananchi sita kati ya 10 (asilimia 60), walisema wamewahi kusikia kuhusu ‘Panya Road’ wakati wananchi tisa kati ya 10 (asilimia 87) walidai hakuna kikundi kama hicho katika maeneo yao.
Matokeo hayo yanabainisha zaidi kuwa wananchi bado wanaamini kuwa mfumo wa sheria haufanyi kazi ipasavyo.
“Zaidi ya nusu ya wananchi (asilimia 53) wanaamini kuwa raia wa kawaida ataadhibiwa kwa mujibu wa sheria akitenda kosa, lakini kuadhibiwa kwa watu wenye kipato cha juu ni vigumu.
“Asilimia 14 wanaamini kuwa watu wenye kipato cha juu wanaweza kuadhibiwa iwapo watavunja sheria na wengine (asilimia 21) wanaona hilo pia linawezekana kwa watumishi wa umma,” ilisema sehemu ya ripoti hiyo.
Ilibainisha kuwa idadi hiyo imeshuka ikilinganishwa na ilivyokuwa mwaka 2013.
Katika kipindi hicho, asilimia 39 ya wananchi walidhani kuwa watumishi wa umma watakumbana na mkono wa sheria wakitenda kosa.
Ilieleza kuwa pamoja na hayo yote, wananchi sita kati ya 10 (asilimia 60), wanaamini Jeshi la Polisi linawahudumia zaidi watu wenye fedha kuliko wa kipato cha chini.
Utafiti huo wa maoni ya wananchi juu ya usalama na haki ni sehemu ya mfululizo wa tafiti zitokanazo na mradi wa Sauti za Wananchi.
Meneja wa Sauti za Wananchi, Elvis Mushi alisema wananchi wanakabiliwa hofu ya magenge ya wezi na kukosekana kwa usalama ifikapo kipindi cha uchaguzi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze alisema wananchi wengi wanajihisi kuwa salama katika maeneo yao, lakini wanakumbana na vitendo vya wizi.
Januari mwaka huu, vikundi vya Panya Road vilileta wasiwasi katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam kwa kufanya uhalifu na vurugu.
Vikundi hivyo vilidaiwa kuwapiga watu na kuharibu mali katika maeneo ya Wilaya ya Kindononi kiasi cha kuwafanya baadhi ya wakazi wa jiji kujeruhiwa.
Kutokana na uvunjifu huo wa amani, Jeshi la Polisi lilifanya msako katika baadhi ya mitaa iliyodaiwa kuwa na vijana hao wahalifu na kuwakamata zaidi ya 700
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment